Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Tuesday, July 2, 2013

Kwanini Obama amechagua kuitembelea Tanzania?

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe


Swali kubwa ambalo limekuwa likiulizwa na watu wengi kuhusiana na ziara ya Rais wa Marekani, Barack Obama katika bara la Afrika ukiacha Senegal na Afrika Kusini alikotembelea, ni kwanini ameichagua Tanzania.

Swali hilo linajibiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt, kwa nyakati tofauti wiki iliyopita, wakitaja sababu zilizomfanya Rais huyo kuichagua Tanzania kuwa moja ya nchi za bara la Afrika kuitembelea na hivyo kufuta dhana potofu iliyokuwa ikienezwa na baadhi ya watu kwamba ziara hiyo imelenga kupora rasilimali za taifa.

Waziri Membe, alitaja moja ya sababu ni kuwapo kwa demokrasia na utawala bora hapa nchini.

Alisema Tanzania kwa kiwango kikubwa Tanzania imekuwa inatekeleza misingi ya utawala bora, uhuru wa kupata habari na haki za binadamu.

Alisema hata kama kumekuwa na malalamiko juu ya suala la utekelezaji wa haki za binadamu na utawala bora, bado Tanzania iko katika nafasi nzuri zaidi katika takwimu kidunia ikilinganishwa na nchi nyingine barani Afrika.

Waziri Membe alisema Tanzania pia inafanya vizuri katika kigezo cha demokrasia ikilinganishwa na nchi nyingine Afrika.

Alisema katika kiwango cha amani, Tanzania inashika nafasi ya 53 duniani, Kenya ikiwa nafasi ya 135, Rwanda 136 na Burundi 144.

Sababu nyingine alisema ni nafasi ya Tanzania Ukanda wa Maziwa Makuu na kimataifa.

Kwa mujibu wa Waziri Membe, Tanzania imekuwa kinara katika utatuzi wa migogoro katika nchi jirani akitaja mfano kuwa ni Kenya, Zimbabwe, Comoro pamoja na Madagascar.

Alisema msimamo wa Tanzania katika masuala ya kimataifa umekuwa unaeleweka bayana.

Sababu nyingine alisema ni kuwapo kwa miradi ya Shirika la Millenium Challenge (MCC) Tanzania inayofadhiliwa na Marekani.

Alisema Tanzania ni nchi ya pili baada ya Morocco katika kupokea fedha za akaunti ya changamoto za milenia kutoka Serikali ya Marekani.

Alisema katika awamu ya kwanza, Tanzania ilipokea Dola za Marekani milioni 698 ili kutekeleza miradi ya maendeleo.

Alisema Marekani kupitia MCC inagharimia miradi mbalimbali, ikiwamo ya maji, umeme na barabara.

Pia alisema urafiki mkubwa uliopo baina ya Tanzania na Marekani na umechangia kiongozi huyo wa taifa kubwa la Marekani kuja nchini.

Alisema Marekani na Tanzania zimekuwa na urafiki wa karibu katika kipindi cha muongo mmoja na nusu (miaka 15) na kwamba, ushirikiano huo umeimarika zaidi katika miaka ya hivi karibuni hasa baada ya kulipuliwa kwa Ubalozi wa Marekani nchini mwaka 1998.

Waziri Membe alisema baada ya kutokea mlipuko katika ubalozi huo jijini Dar es Salaam, Tanzania ilishirikiana kwa karibu na Marekani kuhakisha kwamba, watuhumiwa wanasakwa, kukamatwa na kushtakiwa, wakati katika mataifa mengine haikufanyika hivyo.

Alisema kitendo hicho cha serikali ya Tanzania, kiliongeza uaminifu kwa Serikali ya Marekani, ambayo katika kipindi hicho ilikuwa ikiongozwa na Rais Bill Clinton.

Membe alisema ukarimu wa Watanzania umeifanya pia Tanzania kupendwa na utawala wa Rais Mstaafu wa Marekani, George Bush, na sasa Rais Obama.

Kwa upande wake, Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt, alisema sababu za Rais Obama kuja Tanzania ni kuwapo kwa utawala bora, demokrasia na ushirikishaji wa watu wake wakati wa kufanya uamuzi unaogusa maisha yao ya kila siku.

Alisema Tanzania ni nchi ya mfano linapokuja suala la uongozi bora na ndiyo maana imekuwa na amani na utulivu kwa muda mrefu ikilinganishwa na nchi nyingi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Balozi Lenhardt alisema sababu nyingine inayomfanya Rais Obama kuja Tanzania ni kutokana na jitihada za Serikali ya Marekani kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji na kasi ya ukuaji wa uchumi Tanzania.

Alitaja sababu nyingine kuwa ni kuisaidia Tanzania kuendeleza fursa mbalimbali za kujiletea maendeleo.

Alisema uendelezaji huo wa fursa, una lengo la kuisaidia Serikali ya Tanzania kukabiliana na tatizo la umaskini.

Balozi Lenhardt alisema Marekani ni moja ya nchi zinazoongoza kwa kutoa fedha nyingi za misaada kwa Tanzania, akitoa mfano kuwa mwaka 2012 pekee ilitoa Dola za Marekani milioni 750.

No comments:

Post a Comment