Janeth Jackson anayedaiwa kula njama za kumuua mume wake, Simon Jakson na mtoto wake wa kambo. |
Arusha. Mwanamke anayedaiwa kupanga njama za kumuua mumewe wa
ndoa na mtoto wa mume huyo, amepandishwa mahakamani akiwa na mtuhumiwa
mwingine wa mauaji hayo.
Janeth Jackson (32), mkazi wa Moshono, Arusha na
Novatus Elias, walifikishwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
Mahakama ya Wilaya ya Arusha /Arumeru, Devotha Kamuzora, wakisomewa
makosa mawili ya kula njama ya kutaka kumuua Simon Jackson ambaye ndiye
mume wa Janeth.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Edna Kasala,
alidai mahakamani hapo kuwa washtakiwa wote walitenda kosa la pili la
kula njama na kutaka kumuua Desderi Sabas, ambaye ni mtoto wa mke
mwingine kwa mume huyo anayeishi Bukoba, mkoani Kagera.
Washtakiwa wote hawakutakiwa kujibu lolote kwa sababu Mahakama hiyo kisheria haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.
Kasala iliomba mahakama kuwanyima dhamana
washtakiwa, kwa sababu watuhumiwa wengine wawili wanatafutwa hivyo na
upelelezi haujakamilika.
Alidai kutokana na uzito wa tuhuma hizo, maombi
hayo ya kuwanyima dhamana washtakiwa yameambatana na hati ya kiapo ya
Mkuu wa Upelelezi Makosa ya Jinai Mkoa wa Arusha.
“Mheshimiwa tunafahamu kwamba dhamana ni haki ya
washtakiwa kikatiba, lakini kutokana na mazingira ya kesi hii kuwa
magumu, tunaomba dhamana isitolewe ili kuwatafuta watuhumiwa wengine wa
kesi hii,” alidai Kasala.
Kwa upande wake,Wakili wa utetezi, Fidelis Peter,
alipinga maombi hayo na kutaka mahakama itoe dhamana kwa washtakiwa kwa
sababu ni haki yao ya kikatiba na kwamba hilo ni kosa lao la kwanza.
Sababu nyingine ya kupinga maombi ya upande wa
mashtaka, ni kwamba washtakiwa wanaweza kuvuruga upepelezi wakiachiwa
siyo za msingi kwani ni watu wanaoaminika katika jamii.
“Mheshimiwa sababu za kuwanyima dhamana washtakiwa
hazina uzito wowote, pia mshtakiwa wa kwanza (Janeth) ana mtoto wa
miezi sita na tangu akamatwe alhamisi iliyopita hajamwona wala
kumnyonyesha hivyo anastahili kupewa dhamana,”alidai Wakili Peter.
Hata hivyo, baada ya kusikiliza maombi ya pande
zote mbili, Hakimu Kamuzora, alikubaliana na maombi ya upande wa
mashtaka na kuamuru watuhumiwa wapelekwe mahabusu hadi Agosti 5, mwaka
huu kesi hiyo itakapotajwa tena.
Katika kesi hiyo iliyovuta hisia za watu wengi
jijini hapa, inadaiwa Janeth alitaka kumuua mumewe ambaye ni
mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite na mwanaye wa kiume, ili arithi
mali na utajiri alionao mfanyabiashara huyo.
No comments:
Post a Comment