Hata kabla ya maziko askari wa Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ), waliouawa Darfur, Sudan hayajafanyika,
mchumba wa mmoja wa wapiganaji hao, Amina Juma ameonja chungu nyingine
baada ya kutimuliwa kwenye nyumba aliyokuwa akiishi na marehemu mwenza
wake.
Amina ambaye inadaiwa kuwa alikuwa akiishi na
Fortunatus Msofe aliyekuwa askari katika Kambi ya Msangani, 36KJ Pwani
alisema jana: “Kumekuwa na mzozo wa hali ya juu na ndiyo maana
tumeshindwa hata kufika Uwanja wa Ndege kuupokea mwili na hata kesho
(leo) sidhani kama nitakwenda... kuna mtafaruku mkubwa wa kifamilia.”
Baada ya kutimuliwa, Amina ambaye hawakuwahi
kupata mtoto na marehemu Msofe, alilazimika kuondoka kwenye nyumba hiyo
na kwenda Mlandizi kwa wazazi wake.
“Nimeishi na Msofe kwa miaka mitatu, akiwa kambini
mimi niko hapa na wakati mwingine alikuwa analala huku... lakini leo
wamenitimua,” alisema huku akilia.
Habari zilizothibitishwa na baadhi ya waombolezaji
waliokuwa nyumbani kwa marehemu Visiga, Kibaha zinasema baadhi ya
wanandugu walimkana Amina siku chache baada ya kutangazwa vifo hivyo.
Ilidaiwa kwamba Amina alitimuliwa katika nyumba
hiyo Ijumaa iliyopita, saa saba mchana baada ya ndugu watatu wa marehemu
kufika hapo wakitokea Tanga.
Walipofika inadaiwa kuwa walitangaza kusitishwa msiba huo katika nyumba hiyo na kutangaza kutomtambua mke huyo.
Watu hao waliwaeleza waombolezaji kuwa walitumwa
na baba mzazi wa marehemu, Willbad Msofe kutoka Kange, Tanga kufika
Kibaha kusitisha msiba uliokuwa ukiendelea nyumbani kwa mtoto wake huyo.
Inadaiwa pia kuwa katika msafara huo, alikuwapo mdogo wa marehemu ambaye aliwahi kuishi kwa miaka miwili na Amina hapo Visiga.
Ilidaiwa kuwa walipofika nyumbani hapo walionana
na mfiwa, Amina na wazazi wake ambao pamoja na majirani na watu wengine
wengi, walikuwa wakimfariji binti yao huyo.
Mmoja wa waombolezaji alisema baada ya salamu
wanandugu hao walianza kuulizia mali za marehemu na walikuwa wakimuuliza
Amina ambaye aliwaleza kila kitu kilipo na baada ya hapo ndipo
walipomweleza kuwa wametumwa na baba wa marehemu kuwa watu hawatakiwi
kuomboleza kwenye eneo hilo kwani msiba upo Tanga tu ambako ndiko iliko
familia yake.
Alipoulizwa baba wa marehemu, Mzee Msofe alisema:
“Mimi ndiye niliyeagiza nyumba ifungwe na ukweli ninamfahamu Amina,
lakini simtambui kama mkewe kwa kuwa hawajafunga ndoa... Hata wewe si
unayafahamu haya? Uchumba si ndoa na ukifunga ndoa ndipo unatambulika
rasmi,” alisema.
No comments:
Post a Comment