Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Friday, July 12, 2013

Ufafanuzi waTFDA kuhusu matumizi ya Mafuta ya Ubuyu

Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ni taasisi iliyoundwa chini ya Sheria ya Chakula Dawa na Vipodozi Sura ya 219, ili kudhibiti ubora na usalama wa vyakula, dawa, vipodozi, na vifaa tiba kwa lengo la kulinda afya ya jamii dhidi ya madhara yatokanayo na matumizi ya bidhaa hizo. Imefahamika kuwa mafuta yatokanayo na mimea hupendwa zaidi kuliko mafuta ya wanyama kutokana na manufaa yake kiafya. Ili mafuta ya mimea yaweze kukidhi vigezo vya ubora na usalama ni lazima yafanyiwe usafishaji (refining) wakati wa usindikaji.

Hivi karibuni kumekuwepo na ongezeko kubwa la matumizi ya bidhaa zinazotokana na ubuyu ikiwa ni pamoja na mafuta yanayotokana na mbegu, unga wa mbegu na majani ya mbuyu.
Taarifa za kisayansi zinaonesha kuwa mafuta ya ubuyu yana kiwango kikubwa cha tindikali ya mafuta aina ya cyclopropenoic fatty acids ambayo huweza kusababisha athari ya kiafya endapo mafuta hayo yatatumika kama chakula. Kiwango cha tindikali ya cyclopropenoic fatty acids huweza tu kupunguzwa katika mafuta ya mbegu za ubuyu kwa kuchemsha mafuta hayo katika nyuzi joto 180 kwa muda wa saa nane (8) au kwa kutumia teknolojia ya kutengeneza mafuta mgando (hydrogenation). Kwa sasa hapa nchini hakuna aina ya usindikaji unaofanyika wenye uwezo wa kuondoa tindikali ya cyclopropenoic fatty acids katika mafuta ya mbegu za ubuyu.


Baadhi ya athari zinazoweza kutokana na matumizi ya mafuta ya ubuyu yenye tindikali ya cyclopropenoic fatty acids ni pamoja na kuathiri vimeng’enyo (enzymes) vinavyosaidia katika uchakataji wa tindikali za mafuta mwilini (fatty acid biosynthesis).
Aidha, taarifa za kisayansi zinaonesha kuwa matumizi ya mafuta yenye kiasi kikubwa cha cyclopropenoic fatty acids sanjari na matumizi ya vyakula vilivyochafuliwa na sumu kuvu aina ya aflatoxin B1 ambayo inazalishwa na ukungu (fungus) katika baadhi ya vyakula kama vile mahindi na karanga huongeza uwezekano wa kuugua saratani.
Hadi sasa hakuna kiwango chochote cha ubora na usalama cha kitaifa au kimataifa cha mafuta yatokanayo na mbegu za ubuyu. Ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya mafuta ya mbegu za ubuyu, jamii inashauriwa kuepuka ulaji wa mafuta hayo.
Hata hivyo, tafiti za kisayansi hazijabainisha athari za kiafya zinazoweza kutokana na ulaji wa bidhaa nyingine zitokanazo na ubuyu kama vile unga wa ubuyu na majani ya mbuyu.
TFDA inatoa wito kwa wananchi na jamii kwa ujumla kushirikiana katika jukumu la kulinda afya za walaji kwa kutoa taarifa pale wanapouziwa au kuhisi kuwepo kwa chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba duni na bandia ambavyo havikidhi viwango vya usalama na ubora au pale sheria inapovunjwa ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wahusika.
Kwa maelezo zaidi usisite kuwasiliana nasi kupitia;
Mkurugenzi Mkuu,
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)
Barabara ya Mandela, Mabibo External,
S.L.P 77150
Dar Es Salaam, Tanzania
Simu: +255 22 2450512/2450751/2452108
Barua pepe: info@tfda.or.tz
Tovuti: www.tfda.or.tz

No comments:

Post a Comment