Raisi wa Tanzania Mh. Jakaya Mrisho Kikwete
Dar es Salaam. Siku chache baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya
Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe kutaja hadharani mishahara ya Rais
Kikwete na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, serikali imekataa kuizungumzia
mishahara hiyo.
Msimamo wa Serikali kutotaja mishahara ya viongozi
wakuu unatofautiana na utamaduni wa nchi nyingine kama Marekani, Afrika
Kusini, Ufaransa na Kenya ambazo mishahara ya wakuu wake huwekwa wazi
kwa umma.
Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema
akiwa wilayani Igunga Mkoani Tabora, alisema Rais Kikwete anapokea zaidi
ya Sh30 milioni kwa mwezi (sawa na Sh360 milioni kwa mwaka) ikiwa ni
marupuru na mshahara kwa mwezi bila kodi, huku Pinda akipokea Sh 26
milioni kwa mwezi.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani
alisema kiongozi yeyote haruhusiwi kutaja mshahara wa mtu mwingine kwa
kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria ya utumishi wa umma.
“Kuutaja mshahara wa mtu mwingine ni kinyume cha
sheria na kosa, siyo utaratibu. Kwani wewe upo tayari watu waujue
mshahara wako?” alihoji.
Aliongeza kuwa ingawa mishahara ya viongozi hao
inatokana na kodi za wananchi, sheria ndiyo inayozuia watu kuyataja
malipo hayo hadharani na kwamba hayupo tayari kuutaja mshahara wa rais
au kiongozi mwingine labda mtu huyo autaje yeye mwenyewe.
“Siwezi kutaja mshahara wa bosi wangu wala wa kwangu mwenyewe. Wewe unaujua mshahara wa Obama (Rais wa Marekani)?” alihoji tena.
Akizungumzia mishahara ya marais wa nchi nyingine
duniani kuwekwa wazi, Kombani alisema kila nchi ina utaratibu wake na
kwamba Tanzania haijafikia hatua hiyo.
Alipotafutwa kulizungumzia suala hilo, Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue simu yake ya mkononi iliita bila
kupokewa. Gazeti hili pia liliwasiliana na Naibu Mtendaji Mkuu mwenye
jukumu la kuanzisha na kuongoza Idara ya Mageuzi ya Kilimo Ofisi ya Rais
Ikulu, Peniel Lyimo ambaye alisema yeye si mhusika. “Masuala yote
yanayohusu utumishi yapo Wizara ya Utumishi,” alisema Lyimo.
Akianika mshahara wa Waziri Mkuu, Zitto alisema
kwamba kiongozi huyo analipwa Sh11.2 milioni kama mbunge, Sh8 milioni
kama waziri na Sh7 milioni kwa nafasi yake ya Waziri Mkuu, hivyo,
kumfanya kupokea zaidi ya Sh300 milioni kwa mwaka.
Hata hivyo, Kombani alilionya gazeti hili kuandika taarifa za mishahara ya watu kwa kuwa kufanya hivyo ni kosa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk
Bashiru Ally alisema Mwalimu Nyerere aliwahi kutaja mshahara wake
hadharani na kuhoji viongozi wanaotaka mishahara yao isitajwe wanaficha
nini.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment