THE UNITED REPUBLIC
OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL
COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512,
2116898
E-mail: ikulumawasiliano@yahoo.com
Fax: 255-22-2113425 |
|
PRESIDENT’S
OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O. BOX
9120,
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Maisha
Bora hayaji kwa kucheza pool – Rais Kikwete
·
Vile
vile aahidi kukomesha watu kusikilizia simu mitini Njombe
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Maisha Bora kwa Watanzania hayawezi kuja kwa watu
kushinda wanacheza mchezo wa pool badala ya kujihangaisha kwa kufanya kazi na
shughuli nyingine za kujiingizia mapato.
Aidha, Rais Kikwete ameahidi kuwa Serikali
yake itakomesha haraka iwezekanavyo kero ya wananchi wa sehemu za Mkoa wa
Njombe kulazimika kupanda mitini ili kupata mawasiliano ya simu za mkononi.
Rais Kikwete ameyasema hayo leo, Ijumaa,
Oktoba 18, 2013, wakati alipohutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji cha
Wanginyi, Kata ya Lupembe, Wilaya ya Njombe katika Mkoa Mpya wa Njombe kwenye
siku yake ya kwanza katika ziara yake ya siku saba kukagua na kuzindua miradi ya
maendeleo katika Mkoa huo.
Akizungumza na wakazi wa Kijiji hicho na
vijiji vya jirani, Rais Kikwete amezungumzia dhana nzima ya Maisha Bora kwa
Watanzania akisisitiza kuwa maendeleo na Maisha Bora kwa Kila Mtanzania hayawezi
kupatikana kwa watu kushinda wanacheza mchezo wa pool mchana kucha.
“Ndugu zangu, nimepata kusema huko nyuma
na nataka kurudia tena kuwa Maisha Bora kwa Kila Mtanzania yanawezekana kwa
watu kujituma na kuchapa kazi na siyo kwa watu kushinda kwenye meza za pool
wakipiga kale kampira huku wakiilaumu Serikali na kuulizana ‘Maisha Bora yako
wapi’?”
Ameongeza Rais Kikwete: “Inawezekana kweli Maisha Bora
yakaja kwa mtu anayeshinda anagonga mpira wa pool kwenye meza? Ni kwa kufanya
kazi kwa bidii na shughuli nyingine za kutuingizia kipato ndipo maisha yetu
yatakapokuwa bora.”
Kuhusu hali ya mawasiliano ya simu Mkoani
Njombe, Rais Kikwete, baada ya kuwa ameambiwa kuwa katika baadhi ya sehemu za
Mkoa huo, watu wanalazimika kupanda juu ya miti ili kupata mawasiliano, alisema
kuwa Serikali yake itakomesha haraka kero hiyo.
“Ni ajabu na aibu kabisa kwamba watu
wanalazimika kupanda mitini ili kupata mawasiliano….Hii ni hatari … kwa sababu
mtu anaweza kuanguka na kuvunja viungo…mtu anaweza kuvunja kiuno,”
alisema Rais Kikwete huko watu wakiangua kicheko.
“Tutahakikisha kuwa watu hawavunjiki
viungo kwa sababu ya kupiga ama kupokea simu za ndugu zao,” Rais
Kikwete amewahakikishia wana-Njombe.
Katika kufafanua azma hiyo ya Serikali
kumaliza kero hiyo, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa
Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa Serikali italimaliza tatizo la mawasiliano
katika Mkoa wa Njombe kwa awamu mbili.
Alisema kuwa katika awamu ya kwanza, kiasi cha
Sh.milioni 260 zimetengwa kwa ajili ya kuboresha mawasiliano katika vijiji 25 vya
Jimbo la Uchaguzi la Njombe Kaskazini na kuwa kazi hiyo itakuwa imekamilika
ifikapo Machi, mwakani, 2014. “Tunataka watu waache kupanda kwenye miti
kwa kutafuta mawasiliano ya simu tu.”
Amesema kuwa katika awamu ya pili, kiasi cha
Sh.bilioni 1.552 zitatumika kutoka Mfuko wa Mawasiliano Vijijini kwa ajili ya
kuboresha mawasiliano ya simu katika Mkoa mzima wa Njombe.
Amesema kuwa kazi ya kuboresha mawasiliano
katika awamu hiyo ya pili, itakamilika ifikapo Agosti, mwakani, 2014.
Kuhusu matumizi ya simu zenyewe, Mheshimiwa
Mbarawa amewataka Watanzania kuzitumia simu hizo za mkononi vizuri kwa mawasiliano
ya maana na yasiyokuwa ya ovyo ikiwa ni pamoja na kutukana watu. “Tuzitumie
simu zetu vizuri kwa mawasiliano mazuri na ya maana na siyo kutumia simu kujenga
na kusambaza fitina na majungu ama kushiriki matusi dhidi ya watu wengine.”
Baadaye jioni, Rais Kikwete alikuwa
anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika sherehe za Uzinduzi Rasmi wa Mkoa wa Njombe
kwenye Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
18
Oktoba, 2013
No comments:
Post a Comment