Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Saturday, November 9, 2013

KCMC YAIBUKA KINARA WA KULIPA KODI MKOANI KILIMANJARO

HOSPITALI ya Rufaa ya mkoa wa Kilimanjaro (KCMC), imetangazwa kuwa mlipa kodi bora kwa mwaka 2013 mkoani Kilimanjaro katika kitengo cha walipa kodi wakubwa wa mkoa huo.


Mkurugenzi wa Hospitali ya rufaa ya KCMC, Prof. Moshi Ntabaye, akipokea cheti kutoka kwa mkuu wa wilaya ya Moshi, Dkt. Ibrahim Msengi baada ya Hospitali yake kutangazwa kuwa kinara wa ulipaji Kodi mkoani Kilimanjaro.
KCMC imekuwaya kwanza kati ya Makampuni na Taasisi mbalimbali mkoani hapa yaliyoshindanishwa katika kitengo cha walipa kodi wakubwa kutokana na juhudi zake katika kuhakikisha inalipa kodi kutokana na huduma wanazotoa kwa jamii.

Mkurugenzi wa Hospitali ya rufaa ya KCMC, Prof. Moshi Ntabaye, akiwa ameshika cheti alichokabidhiwa na mkuu wa wilaya ya Moshi, Dkt. Ibrahim Msengi (hayupo pichani) baada ya Hospitali yake kutangazwa kuwa kinara wa ulipaji Kodi mkoani Kilimanjaro.
Hii ni mara ya pili kwa Hospitali hiyo kuibuka wa Kwanza kwani mwaka 2011 KCMC ilifanikiwa kupata tuzo ya mlipa kodi bora tuzo zinazotolewa kila mwaka na wakala waKodi na makato nchini (TRA).

Akikabidhi cheti cha ubora kwa Mkurugenzi wa Hospitali hiyo katika maadhimisho ya siku ya mlipa kodi yaliyofanyika kimkoa jana katika viwanja vya Uhuru Hostel, ya mjini Moshi, Meneja wa TRA mkoani Hapa, Patience Minga  alisema kwa kuibuka mshindi wa kwanza kama mlipa kodi mkubwa bora, Hospitali ya KCMC imedhihirisha kwamba inawajali wateja wake.

Minga alisema kuwa kila mwaka wamekuwa wakishindanisha makampuni na Taasisi mbalimbali katika tuzo hizo kwa lengo la kuingeza ufanisi katika swala zima la ulipaji kodi ikiwa ni pamoja na kuleta hamasa ya umuhimu wa kulipa kodi.
Mkurugenzi wa Hospitali ya rufaa ya KCMC, Prof. Moshi Ntabaye (katikati), Afisa uhusiano wa Hospitali ya KCMC, Gabriel Chisseu (kushoto, aliyeshika cheti) na mmoja wa ujumbe wa Hospitali hiyo, wakiwa katika picha ya pamoja muda mfupi baada ya kutangazwa kuwa  kinara wa ulipaji Kodi mkoani Kilimanjaro.
 “Kila mwaka, TRA tumekuwa tukishindanisha makampuni mbalimbali kwa lengo la kuongeza hamasa katika swala la kulipa kodi ambapo pia huwa tunatoa elimu kwa wananchi wote,” alisema Minga

Meneja huyo alisema kuwa kila mwaka wamekuwa wakikusanya zaidi ya shilingi bilioni 10 mkoani Kilimanjaro kutokana na kodi huku akibainisha kuwa malengo yao kwa huu ni kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 74.

Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Prof. Moshi Ntabaye alisema uongozi wa Hospitali hiyo imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na serikali katika kuhakikisha inarudisha fadhila kwa jamii ya Tanzania ambayo imeendelea kuiamini kwa takribani miaka 42 tangu ilipozinduliwa mwaka 1971, katika huduma wanazotoa kwa kulipa kodi.

Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya rufaa ya KCMC Prof. Moshi Ntabaye akizungumza na wanahabari baada ya kupata Hati na Tuzo ya ushindi kwa ulipaji bora wa kodi kwa Mkoa wa Kilimanjaro kwa mwaka 2013.
Ntabaye alisema ushindi huo unatokana na ukweli kwamba Hospitali ya KCMC imekuwa ikitoa huduma bora ambayo inawawezesha kulipa kodi kwa wakati kila mwaka ambapo alisema huwa wanalipa zaidi ya shilingi milioni mia moja kila mwaka.

Kwa upande wake Mgeni Rasmi katika Maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi Dkt. Ibrahimu Msengi, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, aliwataka Wafanyabiashara na Wananchi kuendelea kulipa kodi kila mara kwani nchi haiwezi kuendeeshwa bila kodi.

“Nchi yoyote ile haiwezi kuendeshwa bila Kodi, inatupasa kulipa kodi kila mara bila shuruti, hatuwezi kuendelea kwa kutegemea misaada hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha tunalipa kodi ili uchumi wetu ukue,” alisema Msengi.

Washindi wengine ni, Mfanyabishara Patrick Boisafi, shule ya secondari ya St. Magreth, shule ya sekondari ya Kiraeni, Mamlaka ya Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KADECO), shule ya sekondari ya international Moshi pamoja na mengine mengi.

No comments:

Post a Comment