Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Tuesday, November 12, 2013

WAFANYABIASHARA WA SOKO LA MWIKA WAPO KATIKA HATARI YA KUAMBUKIZWA MAGONJWA YA MLIPUKO

MOSHI wafanyabiashara katika soko la Mwika lililopo wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro wapo hatarini kuambukizwa magonjwa ya mlipuko kufuatia kurundikana kwa uchafu wenye kinyesi cha binadamu katika dampo la soko hilo huku likiwa lipo jirani na kituo cha mafuta.

Sambamba na hilo, miundombinu ya maji ya mvua katika soko hilo haijasafishwa huku kukiwa na uchafu mwingi jambo ambalo mvua inaponyesha inasababisha miundombinu hiyo kuziba na kupelekea maji kukosa muelekeo.

Wakizungumza na chanzo chetu baada ya kufika sokoni hapo na kujionea hali halisi, wafanyabiashara bw. Amani Mrema na Bi. Mary Shayo wamelalamikia kiasi cha ushuru kinachotozwa sokoni hapo na huduma za usafi kutokuwa za kuridisha huku wakitupia lawama kulipia kiasi cha tsh.200 kwa ajili ya choo ili hali wanalipia tsh.1000 kwa ajili ya ushuru.

Wamefafanua kuwa,endapo hutolipa kiasi hicho cha Tsh.500-1000 kwa ajili ya ushuru unanyang’anywa mzigo ulionao na huruhusiwi kuuza hata kama ndiyo kwanza umefungua na haujauza na kuongeza kuwa, wao siyo kwamba hawataki kulipia ushuru, bali wanachotaka wao ni hali ya usafi iimarishwo sokoni hapo kutokana na ukweli kwamba ushuru unaokusanywa sokoni hapo ni zaidi ya Tsh. milioni mbili kwa siku ya soko moja.

Hata hivyo msimamizi wa soko hilo alipotafutwa ili kuzungumzia juu ya kero hiyo,amesema kuwa yeye siyo msemaji huku akikimbia kwa madai kuwa suala la dampo kutokuzolewa uchafu lipo chini ya halmashauri na kwamba yeye kazi yake ni kukusanya ushuru.

Kwa upande wake diwani wa kata hiyo Charles Kawiche ameuambia mtandao huu kuwa kuwa,mara baada ya kupita sokoni hapo na kuzungumza na wafanyabiashara hao, walimweleza kuwa msimamizi wa soko hilo amekuwa akitoa lugha zisizoridhisha huku akionyesha kutokujali afya za wafanyabiashara hao.

Juhudi za kumpata mkurugenzi wa halmashauri hiyo pamoja na Mwenyekiti wa halmashuri hiyo ziligonga mwamba kutokana na kile kilichodaiwa kuwa wapo nje ya ofisi kikazi.

No comments:

Post a Comment