Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Wednesday, October 22, 2014

Afya za wafanyabiashara wa soko la Uchira hatarini kwa kujisaidia katika mifuko ya rambo

KILIMANJARO wafanyabiashara  wa soko la  Uchira, katika  wilaya ya Moshi vijijini, mkoani Kilimanjaro,  wapo hatarini  kupatwa na magonjwa ya mlipuko kutokana na kukosa huduma ya vyoo na maji, hivyo kulazimika kujisaidia kwenye mifuko ya rambo na kutupa kinyesi hicho hovyo.

Hali hiyo imejitokeza kutokana na wafanyabiashara  hao kukaa kwa muda mrefu katika soko hilo bila ya kuwa na huduma ya vyoo na maji katika sehemu hiyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwanaharakati wa mtandao huu wa "Kilimanjaro Official Blog", baadhi ya wananchi wa kijiji hicho, walisema hali hiyo ya ukosefu wa vyoo inasikitisha kutokana na wafanyabiashara hao kwenda kujisaaidia kwenye vibanda vinavyo zunguka soko hilo na kutupa hovyo uchafu huo.

Walisema kwa takribani miaka 10 soko hilo halijawahi kuwa na vyoo wala maji, licha ya wakala ambaye amepewa tenda ya kukusanya ushuru akiendelea kuwatoza fedha hizo huku huduma za kijamii zikikosekana sokoni hapo.

Jenipha Marandu, alisema soko hilo linakabiliwa na harufu mbayo kutokana na watu kujisaidia kwenye mifuko ya  rambo na pindi wanapokwenda hospitali wamekuwa wakigundulika na ugonjwa wa maambukizi katika mfumo wa kutolea mkojo (U.T.I)

Jeremiah Joseph, mkazi wa Uchira alisema kutokana na ukosefu wa vyoo katika eneo hilo wafanyabiashara hao wamekuwa wakijisaidia kwenye  vibanda vilivyopo karibu na soko hilo na kuweka kinyesi hicho kwenye mifuko ya rambo na kuitupa katika shimo ambalo lilichimbwa na kuachwa wazi bila kukamilishwa.

Njarita Japutia, mkazi wa kijiji cha Uchira alisema tangu soko hilo liwepo halijawahi kuwa na choo, pia hakuna dalili ya kupata vyoo wala maji katika soko hilo, wala hawajawahi  kusomewa  taarifa ya mapato na matumizi ya michango yao kwa kipindi cha miaka mitano.

Alifafanua kuwa soko hilo linamzabuni ambaye amekuwa akiwatoza ushuru wafanyabiashara hao licha ya kuwa huduma za kijamii zinazotakiwa kuwepo katika soko hilo hazipo, licha ya wafanyabiashara hao kuendelea kuchangishwa  fedha na uongozi  huo wa kijiji.      

Akizungumzia Changamoto hizo mtendaji wa kata ya Kirua vunjo Kusini, Jovita Mosha alisema kero za ukosefu wa choo katika soko hilo zipo, licha ya kukataa kuwa hakuna wafanyabiashara ambao wanajisaidia na kutupa kinyesi hicho katika eneo hilo.

No comments:

Post a Comment