Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Friday, November 14, 2014

Serikali imeliagiza shirika la NSSF kuwachukulia hatua za kisheria waajiri walioshindwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati

KILIMANJARO serikali imeliagiza shirika la hifadhi ya jamii (NSSF), kuanza mara moja kuwachukulia hatua za kisheria waajiri walioshindwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao katika shirika hilo kwa wakati.

Agizo hilo limetolewa na mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama, katika hotuba yake wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa jengo jipya la NSSF, unaoendelea mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Gama amesema kuwa baadhi ya waajiri wanaochelewesha au kutochangia michango ya watumishi wao kwenye mfuko huo, wamekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo ya mfuko pamoja na wanachama wake.
Mkuu huyo wa mkoa wa Kilimanjaro ameutaka  uongozi wa shirika hilo, kutumia sheria zinazoongoza mfuko huo, kuwadhibiti waajiri wote wanaoshindwa kuwasilisha michango yao kama walivyoelekezwa kwa mujibu wa sheria ya mifuko ya hifadhi za jamii hapa nchini.
Aidha ameongeza kusema kuwa mkoa wa Kilimanjaro ni moja ya maeneo yanayokabiliwa na uhaba mkubwa wa nyumba kwa ajili ya makazi ya wananchi, wafanyakazi, wadau wa mfuko na wanafunzi wanaojiunga na vyuo vya elimu ya juu mkoani hapa.
Awali akisoma hotuba Kaimu mkurugenzi mkuu wa shirika la hifadhi ya jamii (NSSF), Chiku Matessa, amesema tathmini za shirika hilo zinaonesha baadhi ya waajiri mkoani Kilimanjaro, wamekuwa wacheleweshaji wakubwa wa michango ya wafanyakazi wao kwa mujibu wa sheria.
Matessa amefafanua kuwa  jambo hilo limekuwa linawaweka wafanyakazi hao katika hali mbaya ya maisha baada ya kustaafu, hivyo akasisitiza waajiri hao kubadilika ili kufikia malengo ya shirika kuwa na maendeleo yanayofanana na hali bora ya maisha ya wanachama wake.
Shirika la NSSF, linakamilisha ujenzi wa jengo hilo, ambalo litakuwa na maeneo ya biashara, kumbi za mikutano, kumbi za starehe, maofisi na hoteli za kitalii, ambapo ujenzi wake ulianza Februari mwaka 2013, na unatarajiwa kukamilika Desemba 2014.

No comments:

Post a Comment