Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Sunday, March 8, 2015

EMANUEL OKWI AWALIZA YANGA PAMOJA NA MASHABIKI WAKE

Kikosi cha Simba
Mashabiki Simba
Mshambuliaji wa Simba, Elias Maguri akijaribu kuwahi mpira huku beki wa Yanga akiwa chini
Kikosi cha Yanga
Benchi la Yanga baada ya mchezo kumalizika
Makocha wakipongezana baada ya mchezo kumalizika
Add captioMashabiki wa Yanga
Kampeni ya Imetosha nayo ilihamia Taifa kwa ajili ya kuwahamasisha mashabiki kuhusiana na kuacha vitendo vya unyanyapaa na vifo vya watu wenye ulemavu wa ngozi

BAO la dakika ya 51 lililofungwa na mshambuliaji Emmanuel Okwi, lilitosha kuipa pointi tatu timu ya  Simba iliyokuwa ikipambana na Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania bara uliochezwa uwanja wa taifa Dar es Salaam.

Ushindi huo unakuwa wa pili mfululizo kwa Simba ambayo wiki iliyopita iliweza kuifunga Tanzania Prisons mabao 5-0 na sasa imefufua matumaini ya kuwania ubingwa baada ya kufikisha pointi 26 katika nafasi ya tatu huku Yanga wakiendelea kubaki kileleni na pointi zao 31.

Katika mchezo huo Simba ilionyesha daliliza ushindi tangu mwanzoni baada ya kutawala mchezo huo hasa eneo la kiungo kwa dakika 20 huku Yanga wakionekana kucheza kwa kujihami na kutumia mashambulizi ya kustukiza ambayo hata hivyo hayakuwa na madhara kwa wapinzani wao.

Mshambuliaji anayechipukia kwa kasi wa Simba alikuwa wa kwanza kulifikia lango la Yanga katika dakika ya pili na kuachia shuti kali ambalo halikuweza kulenga lango na kutoka nje.

Simon Msuva angeweza kuifungia timu yake ya Yanga bao la kuongoza dakika ya saba baada ya kupata nafasi nzuri akiwa ndani ya 18 lakini chakushangazabaada ya kumtengenezea Amissi Tambwe afunge alipiga shuti dhaifu lililodakwa na kipa wa Simba Ivo Mapunda.

Kadri muda ulivyokuwa ikienda Yanga ilionekana kuimarika na kurudi mchezoni na kuanza kuutawala mchezo na kutengeneza nafasi nyingi ikiwemo ile ya dakika 25 aliyoipata Danny Mrwanda lakini alipatwa na kigugumizi cha muguu na kushindwa kufunga.

Dakika tano baadaye kocha wa Yanga Hans van der Pluijm aliamua kumtoa nje Mrwanda na nafasi yake kuchukuliwa na Hussein Javu , hiyo ilitokana na mchezaji huyo kuonyeshwa kadi ya njano baada ya kumuonyesha ubabe beki wa Simba Kessy Ramadhani ambaye awali alimchezea rafu.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika timu hizo zilikuwa bado hazija fungana na Yanga ndiyo waliopata nafasi tano za kufunga mabao kupitia kwa washambuliaji wake Mrisho Ngassa, Simon Msuva, Tambwe na Mrwanda.

Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kuanza kuliandama lango la Yanga  ambapo Ibrahim Ajibu, alipata nafasi nzuri  dakika ya 47 akiwa nje ya eneo la hatari na kupiga shuti kali lilitoka nje na kuwa goli kiki.
Yanga ilijibu shambulizi hilo katika dakika ya  49 Javu aliyewapangua mabeki wa Simba na kupiga shuti kali lililopanguliwa na kipa Mapunda na kuwa kona ambayo iliokolewa vyema na mabeki wa Simba .

Mchezo huo uliendelea kuwa wa ushindani zaidi kwa timu zote mbili kutafuta nafasi ya mabao lakini makosa yaliyofanywa na mabeki wa Yanga kwa kushindwa kujipanga vyema yaliinufaisha Simba katika dakika ya 51 baada ya Okwi kufunga bao hilo pekee akipokea pasi ya Ibrahim Ajibu na kumtungua kipa wa Yanga Ally Mustapha ‘Bartherz’ aliyekuwa ametoka langoni mwake.

Baada ya kuingia kwa bao hilo Yanga walionekana kubadilika na kucheza kwa kasi wakitafuta bao la kusawazisha lakini katika dakika ya 74 walijikuta wakicheza pungufu baada ya kiungo Mnyarwanda Haruna Niyonzima kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi Martin Saanya kwa kosa la kupiga mpira wakati filimbi imeshapigwa.

Hiyo ilikuwa ni kadi ya pili ya njano awali Niyonzima alionyeshwa kadi ya njano  dakika ya 42 kipindi cha kwanza kwa kumchezea rafu Ramadhani Singano.

Simba nayo baada ya kupata bao hilo ilionekana kucheza kwa kupoteza muda huku ikifanya mashambulizi ya kustukiza na dakika ya 80 Okwi tena alipiga shuti kali lilitoka pembeni kidogo ya lango la Yanga.

Kutokana na presha ya mchezo huo kwa nyakati tofauti wachezaji wa timu zote mbili walionekana kuchezeana kibabe ambapo dakika ya 78 beki wa Simba Juuko Murshid na Amissi Tambwe walionyeshwa kadi za njano kwa  kuonyeshana undava.

Baada ya kuona mambo magumu kocha wa Yanga aliamua kumtoa Ngassa na kumuingiza Kpah Sherman hwakati kwa uande wa Simba kocha Goran Kopunovic aliwatoa Ibrahim Ajibu ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Elias Maguli na dakika ya 87 ilimtua Abdi Banda ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Simon Sserunkuma.

Simba: Ivo Mapunda, Kessy Ramadhani, Mohamed Hussein,Hassani Isihaka, Juuko Murshid, Abdi Banda/Simon Sserunkuma, Ramadhan Singano, Jonas Mkude, Ibrahim Ajibu/Elias Maguli, Said Ndemla, Emmanuel Okwi.

Yanga Ally Mustapha, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub, Kelvin Yondan, Said Juma, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Mrisho Ngassa/Kpah Sherman,Danny Mrwanda/Hussein Javu.

Na Rahel Pallangyo wa Lenzi ya michezo.

No comments:

Post a Comment