Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Sunday, March 8, 2015

Watoto zaidi ya 17 wenye umri wa miaka 2 hadi 16 wakutwa wamehifadhiwa katika nyumba moja kinyume na taratibu

KILIMANJARO watoto zaidi ya  17 wenye umri wa miaka miwili hadi kumi na sita (2-16) katika Kata ya Pasua Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro walikuwa wamehifadhiwa katika moja ya nyumba katika kata ya Pasua kinyume na taratibu.

Akizungumza na wananchi waliokuwepo eneo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi Novatus Makunga, alisema kuwa walipata taarifa kuwa eneo la pasua kuna mtu mwenye kituo amehifadhi watoto kinyume na taratibu na ndiyo kamati  ya ulinzi na usalama ilifika eneo la tukio na kukuta watoto  hao katika nyumba hiyo.

Alisema kuwa taarifa ya kuwepo kwa watoto hao waliipata wiki moja iliyopita lakini machi  7  mwaka huu,  ndiyo jeshi la polisi liliizingira nyumba hiyo kuanzia majira ya saa 12:05 jioni  kutokana na kukosa sehemu ya kuwahifadhi watoto hao.

Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwakusanya watoto sehemu moja bila kibali ni kinyume cha sheria za nchi, na kwamba mmiliki wa nyumba hiyo alipaswa kuomba kibali lakini pia mafunzo anayoyatoa kwa watoto hao hata kama ni masuala ya dini ni lazima yafuate taratibu za nchi.

“Sheria zipo unapokusanya watoto mahala pamoja kunatakiwa kuweje kuanzia mazingira hadi eneo lenyewe, na kama una taasisi unaendesha mafunzo je kituo kimesajiliwa na ndiyo maana tumeagiza watoto warudishwe kwa wazazi wao,” alisema Makunga.

Nyumba hiyo yenye idadi ya vyumba vinne pekee na choo kimoja, imewafanya viongozi mbalimbali   walipofika eneo hilo kupata wasiwasi kutokana na idadi kubwa ya watu wanaoishi kwenye nyumba hiyo.

Kwa upande wake mmiliki wa nyumba hiyo  Abdulnasir Abdurhman, alisema kuwa wamewakusanya watoto hao ili kuwafundisha masomo ya dini ya kiislam na kuwakuza katika imani hiyo wakiwa wadogo.

Alisema kuwa watoto hao wameletwa hapo na wazazi wao kwa ajili ya kupata elimu ya dini  na wazazi wao wanajua na wanachangia vitu mbalimbali ikiwemo vyakula ili kuhakikisha watoto wao wanapata elimu ya dini ya kiislam.

“Watoto wote tunaoishi nao hapa wana wazazi wao, ambapo wamekubaliana na sisi waendelee kupata elimu hiyo hapa chini ya uangalizi wetu na wazazi wao wamekubaliana kuwalea,” alisema Abdurhman.

Jeshi la Polisi  lililazimika kutumia askari wa kutuliza ghasia wakiwa na mabomu ya machozi kudhibiti umati wa mamia ya wananchi waliofurika katika moja ya nyumba ambayo ilikuwa imewahifadhi.
 
Jeshi la polisi linawashikilia baadhi ya wazazi na mmiliki wa nyumba hiyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Na
Queen Isack,
Kilimanjaro Official Blog.

No comments:

Post a Comment