Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi.
Bei mpya yaongezeka kwa Sh.232, dizeli Sh.261, mafuta ya taa sh.369, Ni matokeo ya kuzidi kudorora kwa shilingi.
Kuendelea
kuporomoka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani kumeendelea
kuongeza makali ya maisha baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za
Nishati na Maji (EWURA) kulazimika kuongeza bei elekezi ya petroli,
dizeli na mafuta ya taa kuanzia leo licha ya bidhaa hiyo kushuka bei
katika soko la dunia.
Taarifa
iliyotolewa na EWURA jijini Dar es Salaam jana ilitaja bei mpya elekezi
ya rejareja itakayotumika kuanzia leo Julai 1, 2015 kuwa ni petroli
iliyoongezeka kwa Sh. 232 kwa lita sawa na asilimia 11.82, dizeli
imeongezeka kwa Sh. 261 kwa lita (asilimia 14.65) na mafuta ya taa
yameongezeka kwa Sh. 369 wka lita, sawa na asilimia 22.75.
Taarifa hiyo
iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura,
Felix Ngamlagosi, ilieleza kuwa miongoni mwa sababu zilizoongeza bei ya
mafuta ni kuendelea kudhoofu kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya
Marekani na pia mabadiliko ya tozo za serikali katika mafuta kuanzia
Julai Mosi mwaka huu (leo).
Kadhalika,
taarifa hiyo ya Ngamlagosi ilieleza kuwa bei za jumla kwa mafuta hayo
zimeongezeka pia, petroli ikipanda kwa Sh. 232.35 kwa lita sawa na
asilimia 12.49, dizeli Sh. 261.15 kwa lita sawa na asilimia 15.57 na
mafuta ya taa Sh. 369.41 kwa lita, sawa na asilimia 24.32.
“Kulinganisha
na thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani kwa machapisho ya bei
za mwezi Juni na Julai 2015, shilingi imepungua thamani kwa shilingi
175.11 kwa dola ya Marekani sawa na asilimia 8.65,” ilieleza sehemu ya
taarifa hiyo iliyosainiwa na Ngamlagosi.
BEI HALISI
Taarifa ya
EWURA ilieleza kuwa kufuatia mabadiliko hayo, bei elekezi ya rejareja ya
petroli kwa mkoa wa Dar es Salaam ni Sh. 2,198, dizeli Sh. 2,043 na
mafuta ya taa Sh. 1,993.
Kadhalika,
taarifa hiyo ilitaja bei elekezi katika kila mkoa, ukiwamo wa Arusha
ambao bei elekezi kwa lita moja ya petroli kuanzia leo ni Sh. 2,282,
dizeli Sh. 2,127 na mafuta ya taa Sh. 2,077, huku bei elekezi ikionekana
kuwa juu zaidi katika maeneo kama Bukoba ambako petroli itauzwa Sh.
2,413, dizeli Sh. 2,258 na mafuta ya taa Sh. 2,208; na Uvinza mkoani
Kigoma bei ya petrol ni Sh. 2,441, dizeli Sh. 2,286 na mafuta ya taa Sh,
2,236.
Taarifa hiyo
ilibainisha vilevile kuwa vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha
bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana wazi na kuonyesha
bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa
na kituo husika.
SOKO LA DUNIA
Wakati bei
ya petroli ikipanda nchini, hali iko tofauti katika soko la dunia ambako
bei ya mafuta ghafi imeendelea kushuka kila uchao.
Taarifa
zinaonyesha kuwa Mei 1, 2015, bei ya pipa moja la mafuta ghafi ya
petroli lilikuwa likiuzwa kwa dola za Marekani 64.13. Hata hivyo, bei
hiyo imeendelea kuporomoka kila uchao na hadi kufikia Juni 22, pipa moja
la mafuta ghafi ya petroli katikia soko la dunia lilikuwa likiuzwa kwa
dola za Marekani 60.54, sawa na punguzo la dola za Marekani 3.95, sawa
na asilimia 5.93.
Kupungua
huko kwa bei ya petroli katika soko la dunia hakuonyeshi kuleta nafuu
kubwa nchini kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya kuendelea
kuporomoka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola. Takwimu za Benki Kuu
ya Tanzania (BoT) zinaonyesha kuwa kufikia Mei 29, 2015, dola moja ya
Marekani ilikuwa ikibadilishwa kwa Sh. 2,007.08 huku wastani kwa mwezi
wote ikiwa ni dola moja ya Marekani kwa Sh. 1,955.72. Kufikia jana (Juni
30, 2015), kwa wastani dola moja ya Marekani ilikuwa ikibAdilishwa kwa
Sh. 2,030.40, ikiwa ni kuporomoka kwa shilingi kwa wastani wa asilimia
7.2 kulinganisha na Mei, 2015.
Source: Nipashe
No comments:
Post a Comment