Afisa Rasilimali watu
(HR) wa kiwanda cha Bonite Bottlers Ltd, akiwakaribisha watoto na vijana kutoka katika shirika la AGPAHI na kuwapa maelekezo ya utangulizi kabla ya kuingia ndani ya kiwanda hicho.
Picha ya pamoja ya wafanyakazi, wototo, vijana kutoka katika shirika la AGPAHI wakiwa na wahudumu wa afya waliokua wameambatana nao katika ziara ya kutembelea kiwanda cha Bonite Bottlers Ltd.
Peter Zakaria, Msimamizi wa Mradi wa Kilimani
Coffee Culture Tourism Enterprise maarufu kama Kahawa Shambani
akiwakaribisha watoto kutoka katika shirika la AGPAHI kwa kuwapa kila mmoja kikombe cha kahawa.
Deogratias Michael mmoja kati ya wafanyakazi katika Mradi wa Kilimani
Coffee Culture Tourism Enterprise
akiwapa maelekezo namna ambavyo zao la kahawa linavyolimwa kuanzia ngazi ya awali mpaka linapofikia hatua ya kuvunwa na kuandaliwa kwajili ya kutumika kama kinywaji.
Mmoja
kati ya wafanyakazi katika Mradi wa Kilimani
Coffee Culture Tourism Enterprise
akiwaonesha watoto kahawa.
Picha
ya pamoja ya wafanyakazi, wototo, vijana kutoka katika shirika la
AGPAHI wakiwa na wahudumu wa afya walipotembelea Mradi wa Kilimani
Coffee Culture Tourism Enterprise maarufu kama Kahawa Shambani.
Baadhi ya wafanyakazi wa AGPAHI wakipatiwa maelezo ya namna ambavyo Kliniki ya Watoto na Familia (CCFCC) inavyotoa huduma.
Baadhi ya wafanyakazi wa AGPAHI wakipatiwa maelezo ya namna ambavyo Kliniki ya Watoto na Familia (CCFCC) inavyotoa huduma.
Baadhi ya wafanyakazi wa AGPAHI wakiwa katika picha ya pamoja na wahudumu wa afya siku walipotembelea Hospital ya KCMC katika Kliniki ya Watoto na Familia (CCFCC)
Shirika la Ariel Glaser Pediatric
AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) leo
limeendelea na mafunzo ya vijana yanayoendelea Mjini Moshi, Mkoani Kilimanjaro.
Siku ya Alhamisi, 15 Machi 2018,
Watoto na Vijana walipata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali ndani ya mji wa
Moshi ikiwa ni siku maalumu ya mafunzo ya nje ya Darasa. Mji wa Moshi ni mji wa
kitalii unaosifika kwa usafi wa Mazingira, na ndipo ulipo Mlima mrefu kuliko
yote Barani Afrika, Mlima Kilimanjaro na pembezoni mwa mji huu kuna Viwanda
mbalimbali vinavyozalisha bidhaa mbalimbali.
Asubuhi ya Leo watoto waliweza
kufurahia mandhari halisi ya Mji wa Moshi pamoja na kutembelea kiwanda cha
Bonite Bottlers Ltd, kilichopo mjini Moshi kinachotengeneza soda jamii ya
Cocacola. Baada ya kufika kiwandani hapo walipokelewa na Afisa Rasilimali watu
(HR) wa kiwanda hicho na kuweza kuwakaribisha ndani ya kiwanda hicho.
Watoto na Vijana walitembelea sehemu
ya uhifadhi wa maji machafu yanayotoka kiwandani na kusafishwa tena kwa ajili
ya matumizi mengine nje ya matumizi ya uzalishaji kiwandani. Uhifadhi wa maji haya ni jitihada ya utunzaji wa mazingira
wa kiwanda hicho.
Pia baada ya kuona mfumo huo wa maji
walipata fursa ya kutembelea sehemu ya uzalishaji wa maji ya kunywa ya
Kilimanjaro ambayo yanatengenezwa na kiwanda hicho, sambamba waliweza kuona
utengenezwaji wa chupa za maji, vifuniko na upakiaji wa maji katika vifungashio
vyake. Mbali na maji waliweza kuona utengenezwaji wa soda wa kampuni ya Coca Cola na walipata fursa ya kunywa
soda zinazotengenezwa kiwandani hapo.
Safari haikuishia hapo, baada ya
kumaliza ziara katika kiwanda cha soda safari nyingine ilianza ya kutembelea
Kijiji cha Uru Msuni, kata ya Uru Kaskazini katika wilaya ya Moshi Vijijini na
kuweza kujifunza mila na tamaduni za wachaga ambao ndio wakazi wa Mkoa wa
Kilimanjaro. Watoto waliweza kujifunza kilimo cha kahawa hadi kufikia hatua ya
kutumika kama kinywaji.
Ndugu Peter Zakaria, Msimamizi wa
Mradi wa Kilimani Coffee Culture Tourism Enterprise maarufu kama Kahawa
Shambani aliwapokea watoto wa Kambi na kuwaeleza historia fupi ya Kahawa
Shambani. Pia walijifunza historia ya wachaga wanaoishi ndani ya
jamii ya watu wa Uru sambamba na faida ya zao la kahawa na faida ya mradi
huo kwa kijiji.
“Kwa mwaka tunapokea wageni zaidi
ya 1,400 ambao wanatembelea kujifunza, asilimia 60-70 ya malipo yanayolipwa na
wageni hutumika katika miradi ya maendeleo ya kijiji.” Alisema Peter. Mbali
na maelezo hayo watoto na vijana walipata fursa ya kwenda shambani kuona kahawa
na kujifunza namna ambavyo kahawa inalimwa, utunzaji wake, Uvunwaji pamoja na
uandaaji wa kahawa kwa ajili ya matumizi ya kinywaji.
Kupitia safari hiyo watoto na vijana
walifurahi kufahamu kuhusu jamii ya wachaga pamoja na elimu waliyopata juu ya
zao la kahawa. Pia waliweza kuona mlima Kilimanjaro kwa ukaribu zaidi ambapo
watoto na vijana walionekana kuufurahia sana mlima huo mrefu kuliko yote barani
Afrika. Huku shukrani za pekee wakiipa shirika la AGPAHI pamoja na wafadhili
waliowezesha wao kuweza kupata fursa ya kujifunza.
Vilevile, katika juma hilo la kambi ya watoto,
wahudumu wa afya pamoja na wafanyakazi wa AGPAHI walitembelea Kliniki ya Watoto
na Familia (CCFCC) iliyopo katika Hospitali ya KCMC mkoani Kilimanjaro. Lengo kuu ilikua ni kujifunza jinsi kituo cha matunzo na matibabu cha KCMC kinavyotenda kazi. Kliniki hii ilifurahisha wengi kwani ni kubwa na ina vitengo vyote vya muhimu. Inahudumia familia nzima kwa wakati mmoja na huduma za muhimu kama kumuona daktari, kuchukua dawa, kuchukuliwa vipimo vya magonjwa nyemelezi na uzazi wa mpango vyote hupatikana ndani ya jengo moja.
Washiriki walijifunza jinsi kituo cha CCFCC kinavyotoa kipaumbele katika kutoa huduma za kisaikolojia kwa watoto na vijana. Watoto na vijana wana siku maalum ya kukutana ambapo hupata elimu, msaada wa kisaikolojia na kuangaliwa na daktari mwenendo wa afya zao.…mkusanyiko huu hufanyika mara moja kwa mwezi. Safari hii imekua na manufaa makubwa kwa wahudumu wa afya waliotoka vituo mbalimbali vya mikoa ya Tanga, Geita na Mwanza.
No comments:
Post a Comment