Monday, 25 June 2012 08:31 |
ELIZABETH MICHAEL LULU
James Magai
MAHAKAMA
Kuu Kanda ya Dar Es Salaam leo inatarajiwa kusikiliza utata wa umri wa
msanii wa fani ya filamu nchini Elizabeth Michael maarufu kama Lulu,
anayekabiliwa na kesi ya mauaji. Hatua hiyo inalenga kubaini umri halali wa mshtakiwa huyo, baada ya kuwepo kwa mvutano baina ya mawakili wanaomtetea wakidai kuwa bado ni mtoto, na upande wa mashtaka (Jamhuri) unaodai kuwa ni mtu mzima. Lulu anakabiliwa na kesi ya mauaji katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akituhumiwa kumuua msanii mwenzake, Steven Kanumba aliyefariki dunia nyumbnani kwake Sinza, April 7, 2012. Hata hivyo umri wake umezua utata baada ya mawakili wanaomtetea kuomba kesi yake isikilizwe katika Mahakama ya Watoto (Juvenile Court) wakidai kuwa bado ni mtoto kwa kuwa ana umri wa miaka 17 na si 18 kama hati ya mashtaka inavyoonyesha. Lakini Mahakama ya Kisutu iliyakataa maombi hayo ikisema kuwa haina nguvu ya kisheria kuyashughulikia kulingana na mazingira ya kesi hiyo na hivyo kushauri maombi hayo yawasilishwe Mahakama Kuu. Mei 15 mawakili hao waliwasilisha maombi hayo Mahakama Kuu kwanza wakiiomba Mahakama hiyo itamke kuwa Mahakama ya Kisutu ilikosea kuyakataa maombi hayo wakidai kuwa wanaamini mahakama hiyo ilikuwa na uwezo wa kuyashughulikia. Pia waliiomba Mahakama Kuu kama itaridhika kuwa Mahakama ya Kisutu haikuwa na uwezo basi Mahakama Kuu yenyewe ifanye uchunguzi wa umri halali wa mshtakiwa huyo na iagize mwenendo wa kesi hiyo katika Mahakama ya Kisutu usimame hadi suala umri litakapoamriwa. Mahakama Kuu katika uamuzi wake Juni 11, 2012 kwanza ilisema kuwa Mahakama ya Kisutu ilikosea kuyakataa maombi hayo kwa kuwa inayo mamlaka ya kisheria kuyashughulikia. Hata hivyo katika uamuzi huo Jaji Dk. Fauz Twaib alisema kuwa maombi hayo yaliwasilishwa kwake bila kufuata vifungu sahihi vya kisheria, lakini akakubali kuyashughulikia kulingana na unyeti na uzito wa mashtaka katika kesi hiyo . Hivyo aliziagiza pande zote katika kesi hiyo (waombaji yaani Lulu kupitia kwa mawakili wake) na wajibu maombi (Jamhuri)kuwasilisha mahakamani hapo ushahidi na vielelezo watakavyovitumia katika hoja zao na kupanga kuyakiliza maombi hayo leo. Jopo la Mawakili wanaomtetea Lulu linaundwa na Mawakili Kennedy Fungamtama(kiongozi wa jopo), Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Peter Kibatala na Fulgence Massawe kutoka Kituo cha Msaada wa Kisheria na Haki za Binadamu (LHRC). Kwa upande wa Jamhuri unawakilishwa na Mawakili wa Serikali, Elizabeth Kaganda na Shadrack Kimaro. Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo kunatarajiwa kuibuka kwa mvutano mkali wa kisheria baina ya pande husika kutokana na kila upande kuwasilisha mahakamani vielelezo vinavyoonesha mshtakiwa huyo kuwa na umri tofauti. Wakati vielelezo vya upande wa muombaji vikionyesha kuwa mshtakiwa huyo ana umri wa miaka 17, vielelezo ya upande wa mashtaka navyo vinaonesha kuwa mshtakiwa huyo ana umri wa zaidi ya miaka 18 yaani miaka 21. Vielelezo vya upande wa maombi ni pamoja na viapo vya wazazi wa mshtakiwa huyo mama yake Lucresia Augustin Kalugila, mkazi wa Dar es Salaam na baba mzazi Michael Kimemeta, mkazi wa Moshi, cheti cha kuzaliwa na cha ubatizo vya mshtakiwa. Vielelezo vilivyowasilishwa na upande wa mjibu maombi ni pamoja na Mkanda wa video aina ya CD, yenye mahojiano kati ya mshtakiwa huyo na mtangazaji wa kituo kimoja cha runinga nchini. Vingine ni maelezo ya mshtakiwa huyo aliyoyatoa polisi wakati alipohojiwa kuhusiana na tuhuma zinazomkabili, maombi ya hati ya kusafiria (Passport) na maombi ya leseni ya udereva, pamoja na hati ya kiapo kinzani (counter affidavit) kilichoapwa na Wakili Kimaro. Viapo vyote wazazi wa mshtakiwa, cheti cha kuzaliwa na cha ubatizo vya mshtakiwa vinaeleza kuwa mshtakiwa huyo alizaliwa April 16, 1995 katika kituo cha Afya Muhimbili na kupewa cheti cha kuzaliwa namba B.0318479 cha Julai 23, 2004. Pia viapo hivyo vinaeleza kuwa baada ya kuzaliwa mshtakiwa mama yake alimpa jina la Diana Michael Kimemeta, lakini alimpeleka mtoto huyo Moshi mkoani Kilimanjaro kwa ndugu zake, walimpa jina la Elizabeth, jina la bibi yake Elizabeth Shikana. Viapo hivyo vinaendelea kueleza kuwa baada ya majadiliano wote, yeye mama, baba na ndugu wengine walikubaliana kuwa wamuite Diana Elizabeth Michael Kimemeta . “ Elizabeth Michael Kimemeta alibatizwa katika Kanisa la Katoliki Chang’ombe Septemba 28, 1997 na alichukua majina ya ubatizo Diana Elizabeth Michael Kimemeta;” inasomeka sehemu nyingine ya kiapo hicho cha mama wa mshtakiwa. |
Banner
FOLLOW US FACEBOOK
propertyfinder.co.tz
Monday, June 25, 2012
Uchunguzi umri wa Lulu kuanza leo ..!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment