NAIBU Waziri mmoja wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete (jina
tunalihifadhi) usiku wa kuamkia jana amezushiwa tuhuma za kufumaniwa na
mke wa askari mkoani Singida katika Hoteli ya Aqua.
Kwa mujibu wa habari kutoka eneo la tukio, mwanamke huyo aliyejulikana
kwa jina la Neema, alikuwa na naibu waziri huyo ambaye pia aliwahi kuwa
kiongozi wa Bunge.
Naibu waziri huyo inadaiwa alikuwa safarini kwenye mikoa ya kaskazini kushiriki msiba wa wakwe zake.
Taarifa zilizolifikia Tanzania Daima Jumapili, zimedai tukio hilo
lilitokea saa 10 alfajiri ambapo mwenye mke aliyejulikana kwa jina moja
la Zephania na wenzake walikwenda kuizingira nyumba hiyo.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, Naibu waziri huyo alipokuwa
akitoka hotelini hapo mgoni wake huyo aliamua kumjeruhi mkononi kwa
sime.
Walibainisha kuwa baada ya ‘kigogo’ huyo kujeruhiwa alipelekwa polisi
kwa lengo la kutoa maelezo pamoja na kupatiwa fomu ya matibabu, ambayo
hata hivyo haijawekwa wazi aliyapata katika hospitali gani.
Tanzania Daima Jumapili lilidokezwa kuwa kulikuwa na jitihada kutoka kwa
watu mbalimbali kuzuia habari hiyo isiandikwe kwenye vyombo vya habari
kwa hoja kuwa inakichafua chama tawala na serikali yake.
Baadhi ya ‘vigogo’ walipiga simu katika chumba cha habari kueleza kuwa
habari hiyo si ya kweli, hivyo wakataka kama imefika isitumiwe.
Tanzania Daima Jumapili, liliwasiliana na viongozi wa Jeshi la Polisi
mkoani Singida ambao walikana waziri huyo kufumaniwa licha ya kukiri
kuwapo kwa tukio hilo.
Viongozi hao walisema waziri huyo hahusiki na fumanizi hilo, bali
anayehusika ni mfanyakazi wa ofisi moja ya serikali iliyopo mkoani
Dodoma, ambaye alitajwa kwa jina moja la Boniface.
Hata hivyo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Linus Sunzumwa,
alitofautiana na viongozi wenzake kwa kukana kuwapo kwa tukio hilo
ambalo alisema amelisoma kwenye mitandao.
Gazeti hili lilipomhoji kama kuna tukio linalofanana na hilo, kamanda
huyo alijibu kwa ukali: “Wewe si umeniuliza tukio la naibu waziri
kufumaniwa? Sasa nimeshakujibu si kweli, hilo jingine la nini?,” alihoji
na kukata simu.
Tanzania Daima Jumapili liliwasiliana na Waziri wa Mambo ya Ndani,
Emmanuel Nchimbi, ambaye alikiri kutokea kwa tukio hilo lakini
halijamhusisha naibu waziri huyo.
Nchimbi alisema mtu aliyekutwa na mkasa huo pamoja na mwanamke
aliyefumaniwa walichukuliwa maelezo yao huku yule aliyejeruhiwa
akipelekwa hospitali kwa matibabu.
“Kimsingi sisi hatujui ni kwanini watu wanatengeneza uongo na kumhusisha
waziri, nakuhakikishia naibu waziri ni mzima na anaendelea na shughuli
zake,” alisema.
Tanzania Daima Jumapili, lilidokezwa kuwa upo uwezekano wa mwanamume
aliyefumaniwa alijitambulisha kuwa yeye ni naibu waziri huyo ili apate
huduma tofauti na watu wengine kwenye maeneo aliyokuwapo.
Tanzania Daima Jumapili pia liliwasiliana na naibu waziri anayetuhumiwa
kufumaniwa ambapo alisema taarifa hizo amezipata kwenye mitandao ya
kijamii pamoja na ujumbe mfupi wa simu za viganjani (sms).
Alibainisha kuwa juzi jioni aliaga bungeni mkoani Dodoma kuwa anakwenda
kwenye msiba unaowahusu wakwe zake lakini alipofika mkoani Singida
majira ya saa tatu usiku aliamua kulala katika Hoteli ya Aqua.
Alisema akiwa hotelini hapo alikutana na wabunge wa chama kimoja cha
upinzani ambao alizungumza nao na kuwapiga ‘ofa’ ya vinywaji na baadaye
aliamua kwenda kulala.
Naibu waziri huyo alidokeza kuwa aliondoka mkoani Singida saa 12 asubuhi
bila kupata tatizo lolote, lakini alishangazwa na simu alizokuwa
akipigiwa kuhusishwa na fumanizi hilo.
Ndugu yangu mimi ni mzima, nimezisikia kwenye simu na kusoma kwenye
mitandao ya kijamii taarifa hizo, hazina ukweli wowote, hivi sasa nipo
msibani,” alisema.
Aliongeza kuwa taarifa hizo zimelenga kumchafulia jina kwenye medani ya kisiasa lakini alijinasibu kuwa hazitafanikiwa.
Habari za mbunge huyo kufumaniwa jana zilizagaa katika mitandao ya
kijamii pamoja na watu kutuma ujumbe mfupi wa maneno kupitia simu za
viganjani (sms) wakilitaja jina la naibu waziri huyo
chanzo:daima
No comments:
Post a Comment