Monalisa Liyumba.
Ndugu wa Monalisa waliofika kituo cha polisi Uwanja wa Ndege
wa Julius Nyerere kumwekea dhamana.
Amatus Liyumba.
Na Makongoro Oging’BINTI mwingine anayetajwa kuwa ni wa Amatus Liyumba aliyejitaja kuwa anaitwa Monalisa Liyumba amenaswa na polisi wa Kituo cha Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Kitengo cha Kuzuia Madawa ya Kulevya, Uwazi imeambiwa.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, binti huyo alikamatwa mara baada ya kuwasili uwanjani hapo kwa ndege ya Qatar iliyotua saa 2:05 asubuhi Juni 27, mwaka huu.
Kabla ya ndege hiyo kutua, habari zinasema, polisi wa kuzuia madawa ya kulevya walikuwa wametanda kila kona ya uwanja huo kumsubiri binti huyo na alipotua akatiwa mbaroni.
“Mama wa binti huyo aliyejulikana kwa jina la Nina alionekana akiwa amechanganyikiwa huku akibishana na polisi na kuwaomba wamwachie binti huyo,” kilisema chanzo hicho.
Habari zinasema juhudi hizo ziliishia ukutani baada ya polisi kumpiga pingu binti huyo na kwenda kumtupa mahabusu na hadi saa 12 jioni binti huyo alikua bado ameshikiliwa na polisi.
Mwandishi wetu alifanikiwa kuzungumza na mmoja wa wana familia ambaye hakutaka kujitambulisha jina lake ambaye alisema kuwa, Monalisa aliachiwa kwa dhamana aliyowekewa na mtu mmoja aliyetajwa kwa jina moja tu la Frank.
Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Kuzuia Madawa ya Kulevya, Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Polisi, Alfred Nzowa alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lakini akasema alikuwa nje ya nchi, hivyo upelelezi wa tukio hilo unaendelea.
Mapema mwaka huu, mtoto wa Liyumba aitwaye Morine alikamatwa nje kidogo ya Mkoa wa Lindi na kuhusishwa na madawa ya kulevya, familia yake imekuwa ikimtembelea mara kwa mara mahabusu anakoshikiliwa.
No comments:
Post a Comment