Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Sunday, July 22, 2012

Dk. Ulimboka ashindilia serikali...!

Saed Kubenea's picture
Na Saed Kubenea - Imechapwa 18 July 2012
DOKTA Steven Ulimboka bado anashikilia kuwa aliyemteka anafanya kazi ikulu, MwanaHALISI limeelezwa.
Taarifa kutoka ubavuni mwa kitanda chake hospitalini anakotibiwa, nchini Afrika Kusini zinasema, ana uhakika na anachosema na hasa sasa wakati hali yake ikiwa inaendelea kuimarika.
Kauli hii ndiyo inafanya dunia nzima itikisike pale serikali ya Rais Jakaya Kikwete inapochelewesha kuunda tume huru ya kuchunguza tukio la kuteka, kutesa na kujaribu kuua Dk. Ulimboka.
Dk. Ulimboka, ambaye hajahojiwa na polisi wa Tanzania juu ya aliowataja, bado anasisitiza kuwa alipokamatwa alikuwa na akili timamu na kwamba walioshona mpango hadi akatekwa anawafahamu fika, zimeeleza taarifa.
Mtoa taarifa amemnukuu Dk. Ulimboka akisema, “…ndugu yangu, hata sasa nawakumbuka.”
Dk. Ulimboka alitekwa usiku wa 26 Juni katika maeneo ya Leaders Club jijini Dar es Salaam; kusukumizwa kwenye gari, kupigwa, kufungwa mikono na miguu, kunyofolewa kucha na kutolewa meno; na hatimaye kutupwa katika msitu wa Mabwepande.
Daktari huyo, mwenyekiti wa jumuia ya madaktari Tanzania, aliokolewa asubuhi yake na wasamaria wema karibu na msitu huo, Bunju nje kidogo ya Dar es Salaam.
Taarifa hizi zinakuja wiki moja baada ya gazeti hili kuripoti kuwa Naibu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa (TISS), Jack Zoka ni miongoni mwa waliounda mpango wa kutekwa na kuteswa kwa Dk. Ulimboka.
Hata hivyo, tayari Zoka amekana kushiriki njama hizo.
Wakati sakata la Dk. Ulimboka likiwa bado linaining’iniza serikali, mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amekana kauli ya Kamanda wa Kanda Maalum ya Polisi mkoani Dar es Salaam, Suleiman Kova juu ya aliyeitwa mtu anayeshikiliwa na polisi kwa madai ya kumteka Dk. Ulimboka.
Ijumaa iliyopita, Kova aliwaambia wandishi wa habari kuwa polisi wamekamata mtu aitwaye Joshua Malundi kutoka Kenya ambaye amekiri kuteka na kutesa Dk. Ulimboka akiwa katika kanisa la Ufufuo alikokwenda kutubu.
Lakini mchungaji Gwajima alitoa tamko Jumapili iliyopita akisema, “Serikali lazima ieleze vizuri. Huyo anayedaiwa kuja kanisani kwetu kutubu ni mgonjwa wa akili. Nawashauri kabla ya kumfanya chochote wampime akili kwanza,” alieleza mchungaji huyo mbele ya waamini wake.
“Kwanza huyo mtu hajaja kwetu kutubu. Alikuja kuomba kukutana na mchungaji kiongozi,” ameeleza Gwijima na kuongeza, “Lakini tulipomchunguza tukaona ni mgonjwa wa akili. Tukamchukua na kumkabidhi kituo cha polisi Kawe.”
Gwijima amesema kama kutubu, basi mtu huyo angetubu huko kwao Kenya na kuhoji, “…kwani kwao Kenya hakuna Mungu?”
Bali katika hali nuyingine ya kustukiza, Kamanda Kova aliongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Jumatatu na kusema polisi hawako tayari kulumbana na viongozi wa dini.
Amesema suala la mtuhumiwa wake, Mulundi tayari liko mahakamani na “halipaswi kujadiliwa.” Amesema jambo hili halitakiwi kujadiliwa na kwamba anayetaka taarifa zaidi juu ya mtuhumiwa, aende huko mahakamani siku kesi itakapotajwa.
Kamanda Kova anaonekana kuwa tofauti na rais wake ambaye licha ya kujadili suala lililoko mahakamani juu ya madaktari, alienda mbali hadi kuwafukuza kazi huku wakiwa wamefungwa na ombi la serikali yake mahakamani.
Taarifa kutoka Afrika Kusini zinasema hali ya Dk. Ulimboka inaendelea kutengemaa siku hadi siku.
“Kwa kweli, tunashukuru Mungu…afya yake inaendelea vizuri. Mimi mwenyewe nimeongea naye jana (juzi Jumatatu) na amenieleza afya yake inaendelea vema,” ameeleza mmoja wa madaktari jijini Dar es Salaam anayefuatilia kwa karibu matibabu ya daktari huyo.
Amesema, “Madaktari wake wanaendelea na uchunguzi kuhusu figo zake ili waone kama zinaweza kufanya kazi au zinahitaji kuondolewa na kuwekwa nyingine. Lakini kwa jumla, matumaini ya kujumuika na Dk. Ulimboka wiki tatu zijazo ni makubwa mno.”
Fuatana na kumbukumbu za Dk. Ulimboka mara baada ya kuokotwa kwenye msitu wa Mabwepande, ambako aliteswa, kutupwa na kuambiwa hakuna atakayeweza kumwokota. Zimechotwa kwenye mtandao wa intaneti wa U-Tube.
Aliyeandaa utekaji na mateso
Nilishawahi kumwona zamani, kwenye mgogoro (wa madaktari) ule mwingine, lakini mara hii alikuwa makini; akinitafuta akisema kwamba anataka kupata maelezo… ili aweze kutoa ushauri…Huyu bwana anafanya kazi ikulu…namfahamu kutokana na matukio ya kwanza…
Alivyoanza kuteswa
Walikuwa wananipiga usoni moja kwa moja, yaani ngumi zinatua usoni; ndo maana wakafanikiwa kunivunja meno. Na haya mengine yamelegea…unaona haya mengine ya chini yamepotea. Wamenipiga sana, nikafika mahali nikawaambia kwa hivi mlivonipiga, ni bora mkaniua.
Hatua za mateso
Wakanifunga miguu…wakakaza ile kamba; mikono yangu ilikuwa imefungiwa mgongoni. Walikaza kamba mpaka nikaona kama huku mikononi kulikuwa kunavimba. Hata miguu wakafunga sana. Basi wakaendesha gari, wakaendesha wakati huu kwa muda mrefu sana. Sikujua wanaenda wapi.
Kipigo na kiminyo
Wanakupiga na vitu vizito, huku wamebana na koleo… Walikuwa wananibana huku kwa mfano kama kuna vitu nakataa kusema. Kwa hiyo wanasema, yaani wewe kwanini husemi. Nikawaambia mimi…? Mpaka unapokubaliana nao wanakuachia.
Lakini kwa kweli mimi sijawahi kupigwa kama nilivopigwa…wala sijawahi kuona mtu anapigwa kiasi kile. Nilipigwa…mpaka unafika mahali unajaribu kuangalia unaona giza. Huoni kilichoko mbele yako, yaani giza. Wakati huku una fahamu zako, huoni.
Walichokuwa wakitaka
…wakati wote kule kwenye gari walikuwa wakisisitiza kuwa wee jamaa umeshatusumbua vya kutosha. Nikawaambia nimewasumbua nini? (Nikasema) …mimi nilikuwa kwenye mazungumzo; sasa kwenye mazungumzo ndo kusaini makubaliano? (Wakasema) …wewe unatakiwa kusaini makubaliano. Sasa makubaliano gani? Mimi sijawahi kukaa mahali nikakataa kusaini makubaliano yoyote. Na hakuna popote eti mimi nilikaa na watu…halafu ikashindikana kukubaliana.
Hali baada ya kipigo
Nakumbuka ilifika mahali nikawa natoka damu mdomoni, natoka damu kichwani; yaani natoka damu karibu kila mahali…

No comments:

Post a Comment