SERIKALI imesitisha rasmi zoezi la uokoaji wa miili ya watu waliozama katika ajali boti ya Mv Skagit Jumatano iliyopita kutokana na ugumu wa kazi hiyo, huku miili zaidi ya 76 ikipotea baharini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Balozi Seif Ali Idd alisema hayo wakati akipokea msaada kutoka Benki ya NMB kwa ajili ya waathirika wa ajali hiyo.
Alisema wataalamu waliokwenda kwenye eneo la ajali kwa ajili ya uokoaji wamethibitisha kutopata mwili hata mmoja kwa muda siku mbili, hivyo Serikali imeamua kusitisha zoezi hilo.
“ Tumeamua siku ya kesho (leo) kusoma hitima kwenye misikiti yote ya Unguja na Pemba, lakini kitaifa hitima hiyo itasomwa katika Msikiti wa Mwembeshauri eneo la Rahaleo mjini Zanzibar,” alisema.
Alisema hitima hiyo itafanyika kwenye misikiti mikuu na kwamba katika mikoa yote hitima hiyo itafanyika saa 7.00 baada ya Sala ya Adhuhuri.
Kabla ya kauli hiyo ya Serikali, Jana ilikuwa siku ya nne kufanyika kwa zoezi la kutafuta maiti katika Bahari ya Hindi lakini waokoaji walirejea majira ya jioni bila ya maiti yoyote.
Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema waliokwenda katika uokozi huo walirejea bila kupata maiti hata moja.
Kati ya watu 290 waliokuwa wamepanda kwenye boti hiyo, ni 146 ndio waliookolewa wakiwa hai huku maiti 68 zikiopolewa baharini ambapo Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Vyombo vya Baharini, Abdalah Hussein Kombo alisema pia zoezi la uokoaji ni gumu.
Awali, mmoja wa wazimiaji ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema : “ Meli inaonekana lakini namna ya kuipindua ili kuziondoa maiti zilizopo tumeshindwa kwa sababu ya ukosefu wa vifaa.”
Chanzo:http://www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment