HATIMAYE
Rais Jakaya Kikwete amewataka madaktari wote wanaoona hawawezi kufanya
kazi serikalini hadi walipwe kiasi cha sh milioni 3.5, waache kazi na
kutafuta sehemu nyingine itakayowalipa vizuri.
Aidha, Kikwete ameweka bayana kuwa serikali haitaweza kulipa kima
hicho cha chini cha mshahara na nyongeza za posho zitakazomfanya daktari
wa ngazi ya chini kulipwa jumla ya sh milioni 7.7 kwa mwezi.
Wakati Rais Kikwete akitoa tamko hilo, Katibu wa Jumuiya ya Madaktari
nchini, Dk. Edwin Chitage, ameweka bayana msimamo wao wa kutorejea
kazini na kuitaka serikali kuwaleta haraka madaktari kutoka nje kujaza
nafasi zao, kama ilivyotangazwa juzi.
Katika hotuba yake kwa taifa jana, Kikwete alisema kuwa haoni sababu
ya madaktari hao kugoma na kugombana na mwajiri ili ashinikize kulipwa
mshahara huo, badala yake amewataka kuondoa usumbufu huo wa kuondolewa
kwa nguvu, kwa wao kuacha kazi kwa amani, na kutafuta sehemu
itakayokubali kulipa kiasi hicho.
Rais Kikwete amedai katika tamko hilo la kwanza tangu kuanza kwa
mgomo huo wa madaktari wiki iliyopita, kwamba hakukuwa na haja ya
madaktari hao kufikia uamuzi wa kugoma, hivyo kuleta madhara makubwa
yakiwamo ya vifo kwa wagonjwa hata baada ya serikali kujitahidi
kutimiza matakwa yao kwa kiwango kikubwa.
Kikwete ambaye alitumia kigezo cha nyongeza ya mshahara katika hotuba
yake kuitetea serikali katika mgogoro huo, alisema itakuwa
kuwadanganya madaktari hao na Watanzania kuwa inao uwezo wa kulipa
kiasi hicho cha mshahara kutoka kima cha chini cha sh 957,700 cha sasa
hadi sh milioni 3.5
“Mwaka 2004/2005, mshahara wa kuanzia wa daktari ulikuwa shilingi
178,700, mwaka 2005/2006 tuliupandisha na kuwa shilingi 403,120.
Tuliendelea kuupandisha mwaka hadi mwaka mpaka kufikia shilingi 957,700
wanazolipwa sasa.
“Kiasi hicho ni mara mbili ya mishahara ya watumishi wa taaluma
nyingine wenye shahada ya kwanza wanaoanza kazi ambao kwa wastani hupata
shilingi 446,100.
“Kwa sasa hatuwezi kuwaahidi kuwa tunao uwezo wa kuwalipa mshahara wa kuanzia wa shilingi 3,500,000 na posho zote zile.
Tukifanya
hivyo malipo ya daktari anayeanza kazi yatakuwa shilingi 7,700,000.
Kwa hakika kiasi hicho hatutakiweza. Si vyema kutoa ahadi hewa kwa watu
tunaowaheshimu na kuwathamini kama walivyo madaktari,” alisema
Kikwete.
Kikwete alisema Mahakama Kuu, Kitengo cha Kazi Machi, 8, 2012, kwa
mujibu wa Sheria ya Mahusiano Kazini, Namba 6 ya mwaka 2004 ilitoa zuio
la mgomo pamoja na kuagiza kuwepo mazungumzo baina ya pande mbili.
Aliongeza kuwa kati ya Aprili, 10, 2012 na 30 Mei, 30, 2012,
vilifanyika vikao sita vya majadiliano kati ya Serikali na Chama cha
Madaktari, kujadili madai 12 ya madaktari, ikiwa ni nyongeza ya mshahara
kutoka kima cha sasa hadi sh 3.5 milioni. Posho ya kuitwa kazini (on
call allowance) asilimia 10 ya mshahara.
Madai mengine ya madaktari yalikuwa kulipwa posho ya kufanya kazi
katika mazingira hatarishi (Risk allowance) asilimia 30 ya mshahara,
madaktari wapatiwe nyumba daraja A au posho ya makazi ya asilimia 30 ya
mshahara, na posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu nayo
asilimia 40 ya mshahara.
Kikwete alisema madai mengine ya madaktari ni posho ya usafiri ya
asilimia 10 ya mshahara au wakopeshwe magari, madaktari wapatiwe Green
Card za Bima ya Afya, kuondolewa kwa watendaji wakuu wa Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii, viongozi wa kisiasa kulazimisha kupewa rufaa nje,
madaktari waliofukuzwa warudishwe kazini, kuboresha huduma za afya na
posho ya uchunguzi wa maiti iongezwe.
Alisema hadi sasa serikali imekubali kutoa Green Card za Bima ya
Afya, kuchukuliwa hatua za kinidhamu dhidi ya watendaji wakuu wa Wizara
ya Afya.
“ Lakini, jambo la kustaajabisha hata Waziri mpya wa Afya alipowataka
waonane kuzungumzia hoja walikataa kumuona. Kwanza walisema hawaoni
sababu kwa vile wameyazungumza na kamati yake kwa miezi mitatu bila ya
mafanikio.
“ Kuhusu viongozi kulazimisha kupewa rufaa ya kutibiwa nje, Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda aliwataka wazingatie maadili ya kazi zao na kukataa
kutoa rufaa kwa mtu asiyestahili, awe kiongozi au asiwe kiongozi. Pili,
walikubaliana kuwa hospitali zilizopo ziboreshwe ili viongozi watibiwe
hapa nchini. Ukweli ni kwamba kufanya hivyo ndiyo sera ya Serikali,”
alisema.
Aliongeza kuwa serikali pia ilikubali madaktari waliofukuzwa, na wale
Interns waliokuwa wamerudishwa wizarani kutoka Muhimbili na kupangiwa
hospitali za Temeke, Ilala, Mwananyamala na Lugalo.
Aidha, alisema pande zote walilokubaliana ni kuhusu kuongeza posho ya uchunguzi wa maiti.
“Hili ni jambo jipya halikuwepo mwazoni. Hata hivyo, serikali
imelikubali na posho hiyo imeongezwa kutoka shilingi 10,000 hadi kufikia
shilingi 100,000 kwa daktari na shilingi 50,000 kwa wasaidizi wake,”
alisema.
Serikali iliwaeleza kuwa watumishi wa kada zote za afya watapatiwa
chanjo dhidi ya maambukizi ya Hepatitis B na fedha zimetengwa katika
bajeti ya 2012/13.
“Serikali imeeleza dhamira ya kurudisha posho ya mazingira hatarishi
kwa watumishi wa umma wanaostahili. Utekelezaji wake utafanyika baada
ya uchambuzi wa kina wa kubainisha mazingira hatarishi ni yepi, viwango
stahiki viwe vipi na nani hasa wahusika.
Madaktari
wamekataa hili la kufanya uchambuzi, wanataka kiwango kiwe kama
wanavyotaka wao, yaani asilimia 30 ya mshahara na kianze mara moja,”
alisema.
Mambo yaliyoshindikana
Hata
hivyo, Kikwete alikiri kuwa kuna mambo mawili hayakufikiwa muafaka
kabisa kati ya pande zetu mbili, nayo ni posho ya kuitwa kazini (on
call allowance).
“ Kwanza sina budi kueleza kuwa serikali imekubali kuongeza posho
hiyo. Tangu Februari, 2012 posho iliongezwa kutoka shilingi 10,000 hadi
shilingi 25,000 kwa daktari bingwa (specialist), shilingi 20,000 kwa
dakari mwenye usajili wa kudumu (Registrars) na shilingi 15,000 kwa
madaktari waliohitimu ambao wapo katika kipindi cha mafunzo kazini
(Interns). Viwango hivyo vya posho vinatumika hivi sasa.
“Madaktari kwa upande wao hawakukubali uamuzi huo wa serikali na
kusisitiza walipwe asilimia 10 ya mshahara. Ugumu wa kukubali pendekezo
la madakari ni kuwa sharti la malipo haya ni mtu kuitwa kazini.
Ukitaka
ilipwe kiwango cha mshahara ina maana kuwa hata kama daktari
hakupangwa kuitwa au alipangwa na hakutokea aendelee kulipwa. Hili
haliwezi kuwa sahihi kufanya.
Linaweza
kuwafanya baadhi ya madaktari kutokutimiza wajibu wao kwa vile wana
hakika mwisho wa mwezi malipo yako pale pale,” alisema.
Alidai jambo la pili ambalo muafaka haukufikiwa baina ya serikali na
madaktari ni kuhusu mshahara wa kuanzia kazi wa daktari, ambao wanataka
uwe shilingi 3,500,000 wakati serikali imesema kiasi hicho hawakiwezi,
badala yake ipo tayari kuongeza mshahara kwa kati ya asilimia 15 mpaka
20 kama ambavyo itafanya kwa watumishi wote wa umma katika mwaka huu
wa fedha.
“Kwa kiwango cha sasa cha mshahara wao, daktari ataanzia kati ya
shilingi 1,100,000 na 1,200,000 kutegemea kiwango kipi hatimaye
kitaamuliwa. Madaktari wamekataa katakata na wameng’ang’ania shilingi
3,500,000,” alisema.
No comments:
Post a Comment