Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Tuesday, July 3, 2012

POLISI MBEYA WAKAMATA MALI ZA WIZI, WANANCHI WATAKIWA KUJITOKEZA KWENDA KUZITAMBUA MALI ZAO...!

Kamanda wa polisi mkoani Mbeya Athuman Diwani 
akiongea na waandishi wa habari
 Pikipiki tatu zilizoibwa  namba T 584 BPU aina ya Star,
T 301 BRU aina ya SanLG na T 489 BQU aina ya Sanya.
Kamanda Diwani akionyesha bunduki walizokamata




WANANCHI wote waliowahi kuibiwa vitu mbalimbali mkoani Mbeya wametakiwa kufika  katika kituo kikuu cha Polisi kutambua mali zao walizowahi kuibiwa.

Wito huo umetolewa na Kamanda mpya wa Polisi mkoani Mbeya wakati akizungumza na waandishi wa habari na kuwaonesha vitu vilivyokamatwa na jeshi hilo zikiwemo bunduki.


Kamanda huyo alisema kuwa wakati wa Opareshini hiyo ambayo ni endelevu, mbali na vitu kadhaa kuvikamata pia wamewakamata na watu 88 wakihusishwa na matukio mbalimbali ya uharifu ikiwemo wizi wa mafuta aina ya diseli kwaajili ya kuendeshea mitambo katika ujenzi wa barabara kati ya Tunduma-Sumbawanga.


Alisema katika matukio ya wizi wa diseli jumla ya lita 4,440 zenye thamani ya zaidi ya sh laki tisa zilikamatwa na tayari mahakama imeamuru mafuta hayo yarejeshwe yalikoibwa ili yakaendeleze shughuli za ujenzi wa barabara huku watuhumiwa nane wa wizi huo wakiwa tayari wamefikishwa mahakamani.

Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Lusekelo Paza, Anyemike Swile, Weiti Mwakatumbula, Michael Mwampamba, Mahona John, Erasto Mwaipaja,Seleman Nasoro na Hassan mrisho.

Jeshi hilo pia limekamata pikipiki tatu zilizoibwa akizitaja kuwa ni yenye namba T 584 BPU aina ya Star,T 301 BRU aina ya SanLG na T 489 BQU aina ya Sanya.

Mali nyingine ni bunduki mbili zilizotengenezwa kienyeji zinazotumia risasi za Shotgun, risasi nane, Televisheni mbili, kompyuta ndogo(Laptop) mbili, Printa moja, redio tatu, mbili aina ya Sub ufa na moja ya kawaida pamoja na simu nane za aina mbalimbali.

Hata hivyo alisema matokeo hayo mazuri yanatokana na ushirikiano mzuri ulioneshwa kati ya raia wema na askari wa jeshi hilo akisema wananchi walijitahidi kwa kiasi kikubwa kutoa taarifa juu ya uwepo wa vitendo vya uharifu.


Amewaomba wananchi kuendeleza ushirikiano huo mzuri akisema utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza uharifu na kuufanya mkoa wa Mbeya kuwa na amani na utulivu na kwamba watoe taarifa kwa askari wanaowaamini zaidi akiwemo yeye mwenyewe.

No comments:

Post a Comment