Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Tuesday, July 3, 2012

MADAKTARI, SERIKALI KAENI MEZANI; MGOGORO UISHE...!


Waziri Mkuu Mizengo Pinda (kulia) akisalimiana na Dk. Steven Ulimboka 
alipofanya mazungumzo na madaktari.
KWANZA kabisa nimshukuru Mungu kwa wema wake wa kutufanya tuzidi kuwa hai leo hii huku tukitafakari jinsi ya kuendeleza nchi yetu, hakika anapaswa kutukuzwa milelele amina.
Baada ya kusema hayo niweke wazi kuwa leo naujadili mgogoro unaoendelea hivi sasa kati ya serikali na madaktari.
Kuna mambo mengi ambayo yamejitokeza katika mgogoro huu na baya kuliko yote ni unyama wa kupitiliza aliofanyiwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Steven Ulimboka wiki iliyopita na watu wasiojulikana kwa madai kuwa lengo ni kumnyamazisha na kusitisha harakati za madaktari nchini kudai haki zao pamoja na kuboreshwa kwa mazingira ya kazi katika hospitali zetu hapa nchini.
Kitu ambacho mimi siamini hata kwa asilimia moja ni kwamba mgogoro huo unaweza kumalizwa kwa vitendo vya ubabe na vitisho, ikiwa pamoja na kudhani kwamba suluhisho la mgogoro huo ni kwenda mahakamani.
Lakini pia akili yangu haiamini kabisa kuwa mgogoro huo utatoa mshindi iwe isiwe, kwa maana ya kumpata mshindi katika mazingira hayo ya uhasama na chuki kati ya serikali na madaktari pasipo kuwapo maridhiano kati ya pande zote mbili hizo kupitia meza ya mazungumzo.
Lakini licha ya wasiwasi huo wa juu niliouainisha, siamini pia kwamba serikali inaweza kuwa mchezaji na wakati huo ikawa mwamuzi wa mgogoro huo kutokana na ukweli kwamba nayo, kama walivyo madaktari ni sehemu ya tatizo linalotikisa nchi hivi sasa na kusababisha mateso makubwa kwa raia wasio na hatia.
Kutokana na mgogoro huo kuwapo kwa muda mrefu, hivi sasa serikali na madaktari wamejikuta katika mazingira ya uhasama, chuki, utengano na kutoaminiana kiasi cha kutoweza kufanya mawasiliano ya moja kwa moja pasipo kuwapo kiungo kati yao cha kuwaleta pamoja na kujadili hatima ya tatizo hili zito.
Lakini pamoja na ukimya ninaouona sasa, siamini hata kidogo kwamba serikali imeshindwa kumaliza tatizo na kuamua kutumia mabavu ya dola kuwafukuza kazi madaktari wote au viongozi wao wanaoratibu mgomo wao nchi nzima. Naamini kwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha balaa nchi nzima kwa sababu sidhani kama serikali ina madaktari wa kutosheleza mahitaji ya wananchi kwa kuwafukuza waliogoma wote na kwamba kuwachukua madaktari wastaafu au wale walio katika majeshi yetu itakuwa ni kukuza tatizo.
Nasema hivyo nikiamini kuwa kunaweza kuwafanya wauguzi na madaktari wanaofanya kazi kwa vitendo (interns) katika hospitali zetu kukasirika na kuamua kujiunga na mgomo huo, hivyo kuchochea tatizo badala ya kutatua.
Mgogoro huu siyo mpya maana umeanza mwishoni mwa mwaka jana na nimewahi kuishauri serikali kukaa meza moja na madaktari, naamini walifanya hivyo sasa nawaomba wakae tena na serikali ambayo nayo naiasa kuwa ijiepushe kufanya maamuzi ya ovyo, bali ifungue milango yote ya mawasiliano kati yake na upande wa pili.
Niliwahi kushauri huko nyuma kuwa kutokana na migomo hii na uhasama wa kutisha, watafutwe wasuluhishi waadilifu wanaokubalika pande zote mbili ambao busara, weledi na uwezo wao utazijengea pande hizo mbili mazingira ya kuaminiana ili kila upande uweze kuzungumza na mwingine kwa uhuru bila hofu.
Hivi ndivyo inavyofanyika katika nchi mbalimbali duniani na ndizo kanuni na taratibu za usuluhishi. Ukweli ni kwamba serikali nyingi katika dunia hii zimeacha utamaduni wa kujihusisha na usuluhishi wa migogoro ambayo serikali hizo zinahusika kwa namna moja ama nyingine kama njia ya kupata suluhisho la kudumu la migogoro fulani.
Kwa kusema ukweli bila kumung’unya maneno, haiwezekani serikali ambayo inatuhumiwa na madaktari ikubalike kama msuluhishi wa mgogoro ambao pia unaihusu. Ndiyo maana tunasema kukua na kushindwa kutatuliwa kwa mgogoro huo kumesababishwa na serikali yenyewe ambayo imekuwa kama mchezaji na mwamuzi wa mchezo kwa wakati mmoja.
Serikali sasa itakuwa imegundua na kujua kwamba baadhi ya watu wamelihusisha tukio la mgogoro wa madaktari na lie la wiki iliyopita la Dk. Ulimboka kufanyiwa unyama kwa kupigwa, kuteswa na kutupwa msituni ni kielelezo tosha. Bila shaka tukio hilo linafanya utatuzi wa mgogoro huo kuwa mgumu zaidi na ndiyo maana nasema kuwa, kama serikali inayo dhamira ya kweli ya kumaliza mgogoro huo, lazima ishirikiane na madaktari hao kupata watu waadilifu na wasiokuwa na masilahi binafsi katika mgogoro huo ili waweze kuwasuluhisha.
Wakati suala hilo likifanyiwa kazi, naamini kwamba serikali itahakikisha wahusika wote waliomfanyia unyama Dk.Ulimboka wanatiwa mbaroni na kushtakiwa. Ajabu kubwa ni kwamba Rais Jakaya Kikwete aliutangazia umma kuwa mgomo wa kwanza ungekuwa ni historia lakini utekelezaji bila shaka umekuwa sifuri, nani alaumiwe?
Naishauri serikali iunde tume huru kuchunguza suala hilo badala ya kuliachia Jeshi la Polisi Tanzania ambalo tayari limetuhumiwa na watu wengi, kufanya hivyo kutalipa heshima jeshi la polisi hasa kama ikibainika kuwa halihusiki na tukio lile la kutisha.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

No comments:

Post a Comment