|
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissau
Waandishi Wetu, Dar na Dodoma MABADIKO
ya Sheria ya Hifadhi za Mifuko ya Jamii ya mwaka 2012, iliyopitishwa
Aprili mwaka huu, imeendelea kuzua mtafaruku sehemu mbalimbali nchini,
huku wabunge wakishinikiza kuwa, sheria hiyo inapaswa kurejeshwa bungeni
ili ijadiliwe upya.
Jana, wabunge waliunga na wafanyakazi
kupinga kipengele cha sheria hiyo kinachomtaka mfanyakazi kupata mafao
yake baada ya kufikisha umri wa kustaafu kwa hiari ambao ni miaka 55, au
miaka 60 kwa mujibu wa sheria.
Hoja ya kutaka suala hilo
lijadiliwe upya ilitolewa na Mbunge wa Kisarawe (CCM), Selemani Jafo
ambaye aliungwa mkono na Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu
Lissu na Mwenyekiti wa Bunge ambaye pia ni Mbunge wa Peramiho (CCM),
Jenista Mhagama.
Hoja ya Jafo ilitokana na kuwapo kwa taarifa
kuwa, zaidi ya wafanyakazi 600 katika migodi minane nchini wameacha
kazi huku wengine zaidi ya 4,000 wakiwa tayari wamewasilisha barua za
kuacha kazi kutokana na sheria hiyo.
Hata hivyo, Mbunge wa
Mwibara (CCM), Kangi Lugola alitofautiana na wenzake pale aliposema kuwa
sheria inayolalamikiwa ilishapitishwa na Bunge, hivyo angependa kujua
uhalali wa kujadiliwa tena bungeni.
Jijini Dar es Salaam, mjadala
mzito uliendelea huku baadhi ya wanasheria waliozungumza na gazeti hili
wakisema: “Marekebisho hayo ni kandimizi na yanalenga kuwanyima haki
wanachama ambao wanaweza kupata matatizo mbalimbali wakiwa kazini”.
Kwa
upande wake Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya
Jamii (SSRA), jana ilitoa taarifa iliyoweka bayana kuwa, fao la kujitoa
kazini limefutwa na kwamba jambo lolote linalohusu mafao ya aina hiyo
linapaswa kusubiri kutolewa kwa miongozo husika.
Bungeni Dodoma Jafo
alitoa hoja akitaka Bunge liahirishe mjadala wa hotuba ya Wizara ya
Viwanda na Biashara jana ili kujadili kwa dharura sheria hiyo aliyosema
kuwa imeanza kuzua mtafaruku na sintofahamu miongoni mwa jamii.
"Mheshimiwa
Mwenyekiti, Wafanyakazi wa sekta mbalimbali wamepinga marekebisho ya
sheria hiyo kwa maelezo kwamba ni kandamizi na yanalenga kuwanyima haki
ya fedha zao wanazokatwa kwa mujibu wa sheria. Naomba mwongozo wako,
Bunge tujadili suala hilo kwa dharura," alisema.
Jafo alitoa hoja hiyo akitumia Kanuni ya 47 (1)(2) na (3) ambayo huruhusu jambo la dharura kujadiliwa.
Hoja
ya Jafo iliungwa mkono na Mhagama ambaye alisema kuwa hilo ni jambo
kujadiliwa lakini kwa wakati huo lilikuwa limekosa kitu kimoja ambacho
ni mdai halisi ya wafanyakazi ambayo yanalalamikiwa.
“Hoja yako
imeungwa mkono na ni kitu muhimu kujadiliwa, lakini imekosa kitu kimoja.
Naomba unisaidie, ni mambo gani hasa ambayo wafanyakazi wanayohitaji
yajadiliwe,” alisema Mhagama na kuongeza:
“Tunatakiwa tuwasaidie
wafanyakazi nchini, kwani hali imekuwa tete kwa wafanyakazi kuhusu suala
hili na ili tuwatete ipasavyo ni vizuri tukajua madai halisi kuhusu
jambo hilo.”
Alipomaliza kutoa mwongozo huo, Mbunge wa Kigoma
Kaskazini, Zitto Kabwe alisimama na kukieleza kiti cha Spika kuwa jambo
hilo ambalo Jafo amelizungumzia ni zito na hadi sasa kauli ya Serikali
haijatoka hadi hivi sasa.
“Kwa busara yako mwenyekiti, naomba uitishe kamati ya uongozi ili tuweze kujadili jambo hili,” alisema Zitto.
Lissu
kwa upande wake alisema kuwa, jambo aliloeleza Jafo ndicho kiini cha
kelele zilizopo mtaani hivi sasa, hivyo anaiunga mkono.
Baada ya
Lissu kumaliza, alisimama Mhagama na kueleza kuwa tayari alishatoa
mwongozo kuhusu jambo hilo kwamba, ni muhimu Jafo akafanya mawasiliano
na wafanyakazi ili kujua wanachohitaji kifanyike.
“Nilichokisema
hapa nampa muda Jafo afanye ‘consultation’ na wafanyakazi hao ili
atengeneze hizo hoja zake vizuri na kulileta suala hilo bungeni,”
alisema Mhagama na kuongeza:
“Ifikapo 7:15 mchana (jana) Kamati ya Uongozi itakaa ila Jafo awasiliane na wafanyakazi ili tuweze kujua matatizo yao...”
Lakini
Lugora alitoa mawazo tofauti akisema: “Wanalalamikia kitu ambacho ni
sheria iliyopitishwa hapa bungeni. Nataka kujua uhalali wa kujadiliwa
suala ambalo tulilipitisha hapa bungeni”.
Mhagama alisimama na
kumweleza Lugola kuwa Bunge linatakiwa kujadili maslahi ya wananchi na
kwamba, sheria zilizopitishwa na Bunge siyo msahafu ambao hauwezi
kubadilishwa.Baadaye jioni, Mhagama alisema Jafo ameelekezwa kwamba
akaandae hoja yake kisha aiwasilishe kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda
ili iwasilishwe bungeni kwa taratibu za kawaida.
Wanasheria Mwanasheria
wa Kituo cha Sheria na Kaki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia alisema
wanapinga marekebisho ya Sheria hiyo kwa kuwa yanawanyima haki
wanachama wa mifuko hiyo kupata stahili zao wanapozihitaji.
“Mimi
kama mwanasheria naona kuwa, marekebisho haya yanalenga kuwakandamiza
wanachama wa mifuko hiyo, kwani kila mtu ana mahitaji yake na majukumu
yake sasa sio vema kumpangia mtu lini anapaswa kuchukua stahili yake,”
alisema Sungusia na kuongeza:
“Tunafahamu kuwa, Serikali inadaiwa
fedha nyingi na mifuko hii kutokanana mikopo mbalimbali; kwa mfano
ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Machinga Complex pamoja na jengo la
Bunge. Sasa wameamua kufanya marekebisho haya ili kufidia fedha
zilizotumika na kusababisha ukandamizaji kwa wanachama.”
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk Sengondo Mvungi alisema marekebisho
ya sheria hiyo ni kandamizi wa wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii
na kwamba wanachama wanapaswa kuamka kupinga sharia hiyo.
Alisema wananchi wanachama wanapaswa kupinga sharia hiyo kwani haijawashirikisha na ina lengo la kuwakandamiza. Dk,
Mvungi alifafanua kuwa, sharia hiyo imepitwa na wakati kwani
wafanyakazi hawakushirikishwa na kwamba sharia hizo zilitungwa wakati wa
chama kimoja.
Kauli ya SSRA Taarifa kwa vyombo vya habari
iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Uhamasishaji Dar es Salaam
jana imesema kuwa, maombi yote ya kujitoa katika mifuko ya hifadhi
yamesimamishwa hadi baada ya miezi sita.
Taarifa hiyo ilisema
usitishaji huo wa kujitoa hautayahusu maombi ya wale ambao wamejitoa
kabla ya Julai 20 mwaka huu 2012 na uamuzi huo imebainisha taarifa hiyo
kuwa imefuatia mkanganyiko uliojitokeza hivi karibuni na kuleta mgongano
baina ya wadau.
Taarifa hiyo imekanusha madai kuwa sitisho la
fao la kujitoa linatokana na shinikizo la Serikali, au madai mengine
kuwa, mifuko imefilisika.“Mamlaka inawaomba wanachama na wadau wote kuwa
na utulivyu wakati wa mchakato ukiendelea kwa lengo la kulinda na
kutetea maslahi ya wanachama” sehemu ya taarifa hiyo imesema.
Taarifa
hiyo imebainisha na kufafanua kuwa marekebisho hayo ambayo yamezua
migongano na wadau yamepitia hatua zote za kisheria na ushirikishwaji wa
wadau muhimu katika sekta hiyo, ambao ni pamoja na vyama vya
wafanyakazi, chama cha waajiri pamoja na serikali.
“Mchakato
umefanyika kwa kuzingatia tofauti ya ajira, mazingira ya kazi na hivi
sasa mamlaka inaendelea kuandaa miongozo na kanuni za mafao kwa lengo la
kuboresha maslahi ya wanachama na majadiliano yatahuisha wadau wote
muhimu” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Imeandaliwa na Joseph Zablon, Aidan Mhando na Pamela Chilongola, Dar na Boniface Meena, Dodoma.
|
|
|
No comments:
Post a Comment