Na, Venance Mtinya, Mbeya
BAADHI ya Asasi za kiraia zinazojihusisha na huduma ya kulea watoto wanaoishi katika mazingira magumu hapa nchini hujinufaisha wenyewe badala ya walengwa.
Hayo
yalibainishwa na Mkurugenzi wa asasi ya Child Prospective Organization
ya Jijini Mbeya, Zahara Mansour, wakati wa hafla ya chakula cha pamoja
na watoto waishio kwenye mazingira magumu iliyofanyika katika viwanja
vya Airport Pub Jijini hapa juzi.
Mansour
alisema baadhi ya wamiliki wa asasi za kiraia si waaminifu kwa kuwa
wanatumia mgongo wa watoto yatima kujinufaisha wao wenyewe huku
wakisingizia wanawalea bila wao kunufaika na chochote.
Alisema
watoto wa mitaani ni wengi mno kiasi kwamba bila moyo wa huruma na
kujitolea hali itazidi kuwa mbaya kutokana na maambukizi ya Virusi vya
Ukimwi kuongezeka kitu ambacho kinasababisha ongezeko la watoto yatima.
“
Baadhi yetu si waaminifu kabisa kwa sababu wanapata misaada kwa ajili
ya kulelea na kuhudumia watoto wa mitaani lakini watoto wenyewe
kawanufaiki na badala yake utaendelea kuwakuta mitaani wanazurura ovyo
na ukifuatilia utagundua kuna mtu ananufaika kupitia mgongo wao” Alisema
Mkurugenzi huyo.
Aliongeza
kuwa wengine wamekuwa wakitoa takwimu za uongo wakati wa kuomba misaada
hiyo kutoka kwa wahisani lakini ukiwaambia wawakusanye hao watoto
hutofautiana na idadi aliyoombea msaada.
“
Unajua watu wengine si waaminifu utakuta anaandika maombi ya msaada
akidai anawatoto 50 anaowalea lakini ukiangalia kiuhalisia anakuwa na
watoto wasiozidi hata kumi kitu ambacho wengine wanakuwa vivuli tu,
hivyo wito wangu naomba wabadilike wamuogope Mungu maana hawa watoto
hawakupenda kuwa yatima na kuishi mitaani” alifafanua Zahara Mansour.
Hafla
hiyo ilihudhuriwa na watoto wa mitaani zaidi ya 50 kutoka asasi
mbalimbali za Jijini Mbeya huku msaada wa vinywaji ukitolewa na kampuni
ya vinywaji ya Cocacola, chakula kilitolewa na uongozi wa Airport Pub
ambapo kampuni ya saruji Mbeya cement wakitoa fulana na madaftari.
No comments:
Post a Comment