Naibu
Waziri wa Uchukuzi, Charles Tizeba amemkabidhi mikononi mwa Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mthamini wa makazi ya wahanga
wa ujenzi wa bandari mpya ya Mwambani ya jijini Tanga kwa kuisababishia
serikali hasara ya sh. milioni 800.
Tizeba alitoa amri hiyo mbele ya ofisa wa Taasisi hiyo aliyeambatana
na msafara wake wa kukagua eneo lililoandaliwa kwa ajili ya ujenzi wa
bandari ya kisasa.
Hali ya hewa ilianza kubadilika pale mthamini wa makazi, Gregory
Mwapule kueleza kuwa kuna nyongeza ya sh. milioni 800 za fidia kwa
wakazi hao tofauti na sh. bilioni 1.7 zilizolipwa awali na serikali.
Katika hali ya kubabaika mthamini huyo alimueleza Naibu Waziri kuwa
majengo ambayo hayakufanyiwa uthamini awali hayakufahamika wamiliki wake
na mengine yalijengwa baada ya zoezi hilo kukamilika na kwamba
alilazimika kufanya marudio ya uthamini kwa mara nyingine.
Baada ya taarifa hiyo, Naibu Waziri alipata hofu na kutaka maelezo
kamili kuhusiana na ongezeko hilo na kudai kuwa haimuingii akilini
kwamba mthamini huyo aliacha majengo ambayo wamiliki wake
hawakutambulika kwa bahati mbaya ama kwa mujibu wa muongozo wa kazi
yake.
Akipingana na taarifa hiyo, Tizeba alitaka kuonyeshwa majengo hayo
mapya hata hivyo hayakuwepo na badala yake yalionekana maboma ya zamani
tofauti na maelezo ya mthamini huyo.
“Hili si boma jipya ni la zamani iweje liwe ni ongezeko…unajua mimi
sitaki mambo ya ubabaishaji, nieleze hizi milioni 800 umezipata
wapi...kwani hili jengo halikufanyiwa uthamini awali!? Alihoji Tizeba
alipoonyeshwa moja ya boma linalodaiwa kuwa ni ongezeko la uthamini wa
awali.
“Wewe bwana acha wizi…huu ni ufisadi, sitaki kuamini kuwa wewe hujui
wajibu wako, lakini hainiingii akilini madai yako ya kutothaminisha
jengo eti mmiliki hajulikani!…hivi wewe unathaminisha mali au
watu?…kwanini usingethaminisha majengo yote na baadae kutambua
wamiliki?” alihoji Tizeba.
Kutokana na mkanganyiko huo, Tizeba aliitaka taasisi ya Takukuru
kuondoka naye kwa ajili ya kumchunguza yeye pamoja na mtandao wake
aliyoshirikiana nao katika kutenda hujuma hizo za kuitia serikali hasara
ya sh. milioni 800.
“Takukuru hebu ondokeni na huyu mtu,…fanyeni uchunguzi kwa kuibia
serikali, na taarifa yake naitaka kabla ya kuanza Bunge, sawa!? alisema
Tizeba huku akimkabidhi Mwapule mikononi mwa Takukuru.
Aidha Mwapule alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo alidai kuwa yeye
ni safi na wala hana hofu na hilo kwa kuwa kilichofanyika ni kwa mujibu
wa taratibu za utekelezaji wa majukumu yake.
“Aaa!, unajua mimi sibabaiki, kama ni kusimamishwa ama kuchunguzwa si
mageni kwangu yalishanifika kwa Waziri Magufuri” alisema huku
akionyesha kukerwa na kauli ya Naibu Waziri.
No comments:
Post a Comment