Wakati
mjadala wa Katiba mpya ukiwa umewagawa viongozi wa dini, siasa na
serikali, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, (BLW) jana
walikutana na Tume ya mabadiliko ya Katiba kutoa maoni yao.
Akizungumza na Wajumbe wa Baraza hilo juzi Naibu Spika, Ali Abdalla
Ali, alisema kwamba wajumbe na viongozi watapata fursa ya kutoa maoni
kuhusu mabadiliko ya Katiba ya Tanzania juu ya mambo mbali mbali ikiwemo
mfumo wa muungano wenyewe.
“Napenda kuwataarifu wajumbe kuwa siku ya Jumapili Tume ya mabadiliko
ya Katiba itakuja kusikiliza maoni ya wajumbe kuhusu mabadiliko ya
Katiba ya muungano,” alisema Naibu Spika muda mfupi kabla ua kuahirisha
Baraza hilo.
Alisema mkutano wa kukusanya maoni utaanza kufanyika majira ya saa 3:00 asubuhi na kuwataka wajumbe kufika kwa muda muafaka.
Alisema Baraza la Wawakilishi linaangalia uwezekano wa mjadala huo
kuonyeshwa moja kwa moja na vyombo vya habari kwa manufaa ya wananchi
wake.
Hata hivyo kazi ya kukusanya maoni katiba mpya inafanyika wakati
viongozi wa serikali ya Umoja wa kitaifa Zanzibar (SUK), wakiwa
wamegawanyika kuhusu mfumo unaofaa wa Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar.
Wakati Makamu wa kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad akitetea
mfumo wa Muungano wa mkataba, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali
Iddi na waasisi wa Mapinduzi na Muungano wameuponda mfumo huo na kutetea
muundo wa Muungano wa serikali mbili nchini.
Balozi Seif alisema muongozo wa CCM umeweka wazi umuhimu wa kuwa na
mfumo wa muungano wa serikali mbili kwa sababu umefanikiwa kudumisha
amani na Umoja wa kitaifa kwa wananchi wa Tanzania tangu kuasisiwa
Muungano huo mwaka 1964.
Mwaasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar Hamid Ameir, alisema wanaotetea
mfumo wa muungano wa Mkataba wana ajenda ya siri ya kutaka kuzorotesha
muungano na hatimaye kufikia malengo ya kuvunja muungano wa Tanganyika
na Zanzibar.
Upande wake Maalim Seif, amekuwa akipigia chapuo mfumo wa muungano
wa mkataba wa serikali tatu ambao amesema utasadia Zanzibar kuwa na
mamlaka yake kamili katika muungano wa Tanzania.
Maalim Seif Sharif Hamad, aliwaambia wananchi katika mkutano wake wa
hadhara kisiwani Pemba mwishoni mwa wiki kuwa Zanzibar imefika wakati
kuwa na mamlaka kamili na Tanganyika yenye mamlaka kamili na baadaye
nchi mbili ziwe na muungano wa mkataba.
Akishangiliwa na wafuasi wake, Maalim Seif alisema chini ya mfumo
muungano wa mkataba Zanzibar iwe na waziri wake mambo ya nje, benki kuu,
mahakama ya rufaa, jeshi la polisi, na kiti chake Umoja wa Mataifa,
(UN).
Hata hivyo, wananchi katika kisiwa cha Unguja na Pemba wanaendelea
kutoa maoni kuhusu mabadiliko ya Katiba huku suala la mfumo wa serikali
mbili likionekana kuchukuwa nafasi kubwa katika mjadala huo.
No comments:
Post a Comment