Serikali
inatarajia kuwanyang’anya wawekezaji waliopewa vibali vya kujenga
hoteli za kimataifa kwenye hifadhi, kutokana na kushindwa kuendeleza
maeneo hayo.
Hayo yalisemwa jana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyarandu, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, kuhusiana
na kongamano la kwanza la Afrika, kuhusu usimamizi wa utalii endelevu
katika hifadhi za taifa, litakaloanza Oktoba 15 na kushrikisha washiriki
412 toka nchi 40 za Afrika.
Alisema kuwa maeneo hayo walipewa kwa lengo la kuyaendeleza na
kupunguza uhaba wa maeneo ya kufikia watalii, lakini wameyahodhi na
kushindwa kuendeleza, jambo linalokera na kulazimisha serikali kuchukua
hatua zingine.
“Tutayachukua maeneo haya na yatakuwa chini ya hifadhi husika, kisha
tutawapatia wawekezaji wengine kuwekeza katika maeneo haya, na tutatoa
kipaumbele kwa wazawa,” alisema Nyarandu.
Alisema kuwa Tanzania inahitaji hoteli za kutosha, sababu inakabiliwa
na uhaba mkubwa wa vitanda vya kulaza wageni na kutoa mfano wa Mkoa wa
Arusha ambako kuna vitanda 2,800, Dar es Salaam 3,700, Mwanza 914 na
Kilimanjaro 414, wakati mji wa Nairobi nchni Kenya una vitanda 15,000 na
Mombasa na Malindi 28,000, idadi ambayo inavimeza vitanda vya hapa
nchini.
Alisema ili kukidhi mahitaji yaliopo kwa sasa ambayo ni makubwa sana,
kutokana na kupokea idadi kubwa ya watalii na hasa wakati wa Msimu wa
Utalii, kunahitajilka jitihada za haraka kukidhi hilo.
Aidha, serikali inatarajia kufungua Uwanja wa Ndege wa Arusha Mjini, ili uweze kutumika kwa kuruka na kutua ndege za kutoka
Nairobi moja kwa moja bila kupitia KIA.
Nairobi moja kwa moja bila kupitia KIA.
“Tukifungua Uwanja huu tutaweza kuongeza utalii kwa zaidi ya asilimia
kumi, tena kwa haraka sana, hivyo tupo mbioni kuanza hili kwa ajili ya
kupunguza pia muda mrefu wa kukaa watalii uwanja wa KIA kusubiri usafiri
wa Nairobi,”alisema.
Kuhusu usalama wa watalii kutokana na mauaji ya watalii yaliyotokea
siku za karibuni, alisema serikali wameongeza ulinzi wa kutosha maeneo
ya hifadhi na kudhibiti wanaoingia bila sababu.
No comments:
Post a Comment