MATUKIO
ya ubakaji katika mkoa wa Kilimanjaro yameelezewa kuongezeka huku
wahanga wakubwa wakiwa ni watoto jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa
masiha yao.
Takwimu zinaonyesha kuwa jumla ya makosa 46 ya ubakaji yameripotiwa polisi katika kipindi cha Julai hadi septemba mwaka huu ambapo asilimia 90 kati yao ni watoto.
Hayo
yamebainishwa na kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro Bw. Robert Boaz
wakati akizungumza na mtandao huu ofisini kwake kuhusiana na matukio ya
ubakaji katika mkoa huo, ambapo alisema matukio hayo yamekuwa yakijirudia mara kwa mara.
Kamanda
Boaz alisema matukio ya ubakaji yameanza kujitokeza kwa wingi katika
mkoa wa Kilimanjaro hivyo kunahitajika ushirikiano wa hali ya juu kutoka
katika jamii ili kuweza kuyadhibiti na kuyakomesha kabisa.
“Yapo
makosa ambayo yameanza kujitokeza katika mkoa wetu,na makosa ya ubakaji
ni makosa ambayo yamekuwa yakijirudiarudia,sasa jamii inapaswa kuchukua
hatua za makusudi ili kulikemea hili kwani likiachwa liendelee ni
hatari kubwa kwa jamii”alisema Kamanda Boaz.
Kufuatia
hali hiyo Kamanda Boaz alizitaka taasisi za dini kutoa ushirikiano
katika kudhibiti tatizo hilo ili kulikomesha ikiwa ni pamoja na
kulikemea katika nyumba zao za ibada, kutokana na kwamba wanaofanya
vitendo hivyo wapo pia katika nyumba za ibada.
“Tunawaomba
watu wa dini watusaidie katika hili,walikemee kwenye nyumba zao za
ibada lakini pia wanaharakati wa haki za watoto na wanawake nao watuunge
mkono kwani tatizo hili limezidi kuwa kubwa na linawaharibu
watoto”alisema.
Kamanda
Boaz alisema katika kudhibiti tatizo hilo jeshi la polisi limeanzisha
dawati ambalo limekuwa likishughulikia matatizo hayo ikiwa ni pamoja na
ukatili wa kijinsia ili kutoa uhuru kwa watu wa rika zote kufika na
kujieleza.
Alisema
madawati hayo yamekuwa yakifanya kazi kubwa ikiwa ni pamoja na
kuhakikisha haki za watoto zinafatwa ,ambapo pia hushughulikia masuala
ya kijinsia na usuluhishi wa kifamilia.
Na Florah Temba, Moshi
Chanzo: www.kilimanjaro-yetu.blogspot.com
No comments:
Post a Comment