Taarifa hiyo inabidi iwasilishwe katika kikao hicho kabla ya kupita siku saba tangu siku ile kilipoanza kikao hicho.
Sheria ilivyo sasa inaelekeza kuwa baada ya ripoti hiyo kuwa silishwa bungeni itajadiliwa katika kamati tatu zinazosimamia Hesabu za Serikali kwa ajili ya kuifanyia uchambuzi, kisha kuwasilisha taarifa zake bungeni katika muda zitakazopangiwa.
Kamati hizo za Bunge ni zile za Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Hesabu za Serikali Kuu (PAC) ambazo hufanya uchambuzi kisha kusoma taarifa zake ndani ya Bunge kwa hatua zaidi.
Hata hivyo, marekebisho yaliyowasilishwa Bungeni jana na Jaji Werema yanapendekeza kubadili utaratibu mzima wa kushughulikia taarifa hiyo, kwani yanaongeza vipengele, “vinavyoliwajibisha Bunge kwa Serikali” badala ya kinyume chake.
Serikali imeongeza vipengele vya ziada ambavyo vinazitaka kamati za Bunge zinapofanya uchambuzi wa ripoti ya CAG, kupeleka maazimio yake kwa Serikali ili “yatafutiwe majawabu” badala ya utaratibu wa sasa wa kupeleka hesabu zake bungeni.
Kimsingi Kamati za Bunge hufanya kazi kwa niaba ya Bunge, hivyo taarifa zake husomwa Bungeni na siyo kwingineko kama ambavyo marekebisho ya sheria yanataka kuelekeza.
Jaji Werema alisema: “Marekebisho haya yamefanywa ili kumwezesha Waziri wa Fedha kuwasilisha taarifa ya majibu ya Serikali ya hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali”.
Ikiwa Bunge litapitisha marekebisho hayo ni dhahiri kwamba Bunge halitakuwa tena na uwezo wa kuwawajibisha watendaji wa Serikali ambao watabainika kuhusika na upotevu wa fedha au kufuja fedha za umma, hivyo kupunguza uzito wa mjadala na uwezo wa wabunge kuhoji.
Kadhalika taarifa za LAAC, POAC na PAC kuhusu taarifa ya CAG na mapendekezo ya kamati hizo, yatajadiliwa sambamba na majibu ya Serikali. Hivyo hakutakuwa na nafasi ya Bunge kutekeleza wajibu wake wa kuisimamia Serikali kama inavyoainishwa katika Katiba.
Hatua hiyo ni sawa na kulifunga Bunge mikono kutokutekeleza wajibu wake kuhusu ripoti ya CAG, kwani kwa mujibu wa sheria halitaweza kujadili chochote hadi Serikali kupitia kwa Mlipaji Mkuu (Paymaster General) atakapokuwa ametoa majibu ya utetezi kuhusu kasoro katika ripoti hiyo.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa inalenga kuzuia kile ambacho kimekuwa kikitokea miaka ya karibuni ambapo Bunge huzingatia mapendekezo ya kamati za usimamizi wa hesabu za Serikali kwa kutoa maazimio ambayo mara nyingi yamekuwa mwiba kwa Serikali ikiwamo kusababisha uwajibikaji wa watendaji wake wakiwamo mawaziri.
Mwaka jana Rais Jakaya Kikwete alilazimika kufanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri na kuwaondoa mawaziri sita na manaibu waziri wawili, yakiwa ni matokeo ya mjadala kuhusu yaliyojiri katika taarifa ya CAG ambayo ilibainisha kuwapo kwa madudu mengi katika hesabu za fedha katika maeneo wanayoyasimamia.
Sheria nyingine ambazo Serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, inapendekeza zifanyiwe marekebisho ni udhibiti wa fedha haramu, kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu, mahakama na mahakimu, ardhi, mafao ya wastaafu ya watumishi wa umma, kusimamia umiliki wa ardhi katika vijiji vilivyokwishaanzishwa na sheria ya mabaraza ya kata.
Lissu
Akiwa akitoa maoni ya Kambi Upinzani bungeni kuhusu Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Sheri namba 3 wa 2012 (The Written Laws - Miscellaneous Amendments Bill), Mnadhimu Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisema kwamba Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman alikiuka sheria za nchi kwa kuwaajiri mahakamu ambao nafasi zao hazipo kwa mujibu wa Katiba.
Mbali na kumtuhumu Jaji Chande, pia Lissu alimtuhumu Spika wa Bunge, Anne Makinda pamoja na uongozi wa Bunge kwamba wamekuwa wakikiburuza chombo hicho kwa kuruhusu baadhi ya mambo kujadiliwa bila kufuata kanuni.
Akichambua mapendekezo ya marekebisho ya sheria za mahakama za mahakimu, Lissu ambaye pia ni waziri kivuli wa katiba na sheria, alisema marekebisho hayo yanalenga kubariki uvunjwaji wa sheria uliokwishafanywa na Jaji Mkuu.
Katika mapendekezo hayo Serikali kwa jumla inataka mahakimu wa wilaya na mahakimu wakazi wapewe mamlaka ya kusikiliza kesi katika mahakama za mwanzo ikiwa ni hatua ya kuboresha mfumo wa utoaji haki nchini. “Lengo halisi la marekebisho haya ni kujaribu kuhalalisha ‘expost facto’ ukiukaji mkubwa wa sheria hiyo uliofanywa na uongozi wa juu kabisa wa Mahakama ya Tanzania mwezi Septemba ya mwaka jana,”alisema Lissu na kuongeza:
“Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na vyombo mbali mbali vya habari, 15 Septemba, 2012 Jaji Mkuu wa Tanzania, Mheshimiwa Mohamed Chande Othman aliwaapisha ‘Mahakimu Wakazi wa Mahakama za Mwanzo’ wapatao 372 katika sherehe iliyofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama, Lushoto”.
Alisema taarifa ambazo kambi yake inazo, mahakimu hao wamekwishatawanywa katika se hemu mbalimbali nchini, lakini wameshindwa kuanza kazi baada ya kupewa ajira kwa sababu Sheria ya Mahakama za Mahakimu haitambui cheo cha Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo.
“Hata hivyo, watumishi hawa wameendelea kulipwa mishahara na stahili nyingine za ajira hiyo pamoja na kwamba hawafanyi kazi yoyote ya uhakimu waliyoajiriwa kuifanya,”alisema na kuhoji:
“Kwa nini Serikali imeruhusu kada ya watumishi wasiotambuliwa na sheria za nchi kuajiriwa na Mahakama ya Tanzania na kulipwa mishahara kwa fedha za umma wakati utumishi wao hautambuliwi na sheria yoyote?”.
Chanzo - Mwananchi
No comments:
Post a Comment