Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Friday, May 31, 2013

Machafuko bungeni

Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Kimataifa  jana ilisababisha mtafaruku mkubwa bungeni na siku nzima Bunge likakwama kufanya shughuli zake. Awali  Naibu Spika, Job Ndugai, aliahirisha Bunge asubuhi hadi jioni, lakini hata liliporejea jioni, aliliahirisha tena ili kutuliza hali ya hewa. Vile vile, Msemaji wa Kambi hiyo, Ezekiah Wenje alinusuruka kupigwa ka wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF), baada ya kuokolewa na askari wa Bunge na kupelekwa kusikojulikana kutokana na hotuba aliyokuwa ameitoa bungeni.. 
Vurugu zilianza wakati Wenje alipokuwa akisoma maoni ya kambi ya upinzani kuhusu Wizara hiyo na kukihusisha Chama cha Wananchi (CUF), na vyama vinavyoshabikia vitendo vya ushoga na usagaji duniani.


Wenje alikuwa anawasilisha hotuba ya kambi ya upinzani baada ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, kusoma hotuba yake ya bajeti kwa mwaka 2013/14.
 Hali ya hewa bungeni ilibadilika alipofika ukurasa wa saba wa hotuba yake aliposema itikadi za CUF ni za mrengo wa kiliberali ambazo miongoni mwa misingi yake ni pamoja na kupigania haki za ndoa za jinsia moja, usagaji na ushoga na kwamba hilo ndilo tangazo la chama hicho kwenye mtandao wao wa umoja wa maliberali duniani.
Mbunge wa Mtambile (CUF),  Masoud Abdalah Salum, alisimama na kuomba mwongozo kuhusu kauli hiyo ya Wenje kukihusisha chama chao na ushoga na usagaji, lakini hata kabla ya Spika hajatoa mwongozo wabunge wote wa CUF walisimama huku wakimporomoshea matusi Wenje.
Naibu Spika alisimama na kuwaomba wabunge hao wa CUF wampe nafasi Wenje afafanue kauli yake na aliposimama alikataa kufuta kauli yake akijitetea kwamba wanaomshutumu hawajaelewa alichokuwa akikisema.
“Mheshiniwa hapa tunazungumzia uhusiano wa vyama vya hapa nchini na vile vya nje kuhusu itikadi wanazofuata, CCM wanafuata mlengo wa kushoto, Chadema sisi tuko kati na CUF wanafuata mlengo wa waliberali, tunachosema hapa ni mrengo wa itikadi,” alisema Wenje na kusababisha wabunge kulipuka kwa kelele wakisema hotuba hiyo haitasomwa huku wakiwa wamesimama.
Utetezi huo wa Wenje ulionekana kama umeongeza mafuta kwenye moto huku wabunge wote wa CUF wakisimama na kutoa matusi mazito kwa Wenje wakiungwa mkono na baadhi ya wabunge wa CCM, ambao walisikika kwenye vipaza sauti wakisema apigwe apigweeee hana adabu.
Kauli ya Wenje ilizua zogo kubwa kiasi cha kutoweka kwa usikivu hali iliyomlazimu Naibu Spika kusimama na kuahirisha shughuli za Bunge hadi jioni huku akiiagiza Kamati ya Maadili ya Bunge ikutane kujadili hali hiyo.
Baada ya kuahirishwa kwa shughuli za Bunge, wabunge wa CUF walionekana wakitoka nje kwa kasi huku wengine wakichana chana hotuba hiyo ya kambi ya upinzani wakiwahi nje kwa ajili ya kumzonga Wenje.
Walipofika nje hawakufanikiwa kumwona Wenje ambaye aliondolewa maeneo hayo na askari wa Bunge kwa sababu za kiusalama na ndipo hasira zao zikamwangukia Mbunge wa Musoma Mjini (Chadema), Vincent Nyerere, waliyemkuta nje ya ukumbi ingawa wakati wa mzozo wote hakuwapo bungeni.
Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Selemani Bundala ‘Bwege’, aliwaongoza wenzake kumporomoshea matusi Nyerere ambaye alionekana kuduwaa kwani hakuwa anajua yaliyotokea bungeni.
“Sisi tutawapiga kweli chezeeni CCM, sisi msituchezee tutawatandika msidhani CUF ni CCM mnaowachezea kila siku, acheni mambo ya kijinga tutawakomesha muache kutuchezea,” alisikika Bungala huku wabunge wengine wa chama hicho wakiwa wamemzingira Vincent.
Mbunge huyo wa CUF alipokaribia kumtwanga ngumi Vincent Nyerere, Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde, alifanya kazi kubwa kumlinda Nyerere kujinasua katikati ya kundi la wabunge wa CUF walioonekana wakizungumza kwa jazba huku wakimnyooshea kidole.
Wabunge wengi walionekana nje ya ukumbi wa Bunge wakiwa katika makundi makundi wakijadili mtafaruku huo uliosababishwa na hotuba ya kambi ya upinzani.
Mbunge wa Mjimkongwe (CUF), Ibrahim Sanya, alionekana akifoka kwa sauti ya juu akidai kuwa wabunge wa Chadema tangu Bunge lianze wamekuwa wakitoa hotuba za kuwadhalilisha wabunge wa chama chake.
“Leo (jana) jioni wakirudia ujinga huu tunapiga mtu humo humo ndani ya ukumbi wa Bunge, hatuwezi kukubali dhihaka ya namna hii, Bunge liongeze askari wa kutosha maana hapatakalika mle ndani tukidhalilishwa tena,” alisikika Sanya akifoka.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CUF), Ali Keisy, alisikika akiwafokea wabunge hao wa CUF kwamba wameshindwa kumshughulikia Wenje ndani ya Bunge, hivyo hawana sababu ya kupiga kelele wakiwa nje ya ukumbi.
Alisema matusi yaliyotolewa dhidi ya CUF yangekuwa yameelekezwa upande wa CCM machafuko makubwa yangetokea ndani ya ukumbi huo kwa kuwa wasingekubali Wenje atoke bila kufuta kauli yake.
“Mmeshindwa kumshughulikia bungeni mnakuja nje kupiga kelele tu, mngemtandika akalazwa Muhimbili au Aga Khan ningewaelewa, lakini mmeishia kuangalia tu, angeitukana CCM ningemla nyama mimi, kwa kweli wabunge wa CUF mmenidhalilisha sana kwa uzembe mliouonyesha,” alisema Mbunge huyo wa CCM na kuongeza:
“Naomba msiendelee kutupigia kelele hapa nje, kama mmeshindwa kummaliza mle mle bungeni msitupigie kelele….mnasema mtamshughulikoa jioni huo ni uongo, ni sawa na kumfumania mtu halafu unamlea badala ya kummaliza hapo hapo, ingekuwa chama changu kimetukanwa asingetoka akiwa anacheka,” alisema Keisy kwa sauti kubwa akiwaeleza wabunge wa CUF waliokusanyika nje ya ukumbi wa Bunge.
Akizungumzia tukio hilo, Nyerere alisema amesikitishwa na tukio hilo kwani hakuwa sehemu ya mzozo huo.
Alisema alivamiwa na wabunge wa CUF ambao walianza kumporomoshea matusi na kejeli za kina aina wakiongozwa na ‘Bwege’.
“Mimi nimemheshimu Bungala kwa utu uzima wake, sikuwa najua lolote, nimeshangaa kuona navamiwa na kundi la wabunge kila mmoja akitoa tusi lake dhidi yangu na Chadema, wamenifedhehesha sana,” alisema.
Katika hali ya kushangaza, Naibu Spika, Job Ndugai, aliwalaumu waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Bunge kwamba ndio wanasabasisha vurugu bungeni.
Ndugai alisema waandishi wa habari wamekuwa wakipendelea vyama vya upinzani na kuwakandamiza wale wa CCM.
“Haya ni matokeo ya kazi zenu waandishi wa habari, mnawabeba sana wapinzani, fanyeni kazi zenu kwa usawa maana wapinzani hata wangefanya uovu gani nyinyi huwa hamuoni ila wakifanya wabunge wa CCM mnayakuza,” alisema Ndugai.
WENJE AGOMA KUOMBA RADHI
Wakati huo huo kikao cha Bunge kilichokuwa kiendelee jana joni kilivunjika tena baada yaa kutokea kutoelewana baina ya wabunge wa CUF na Wenje.
Kikao hicho kilipoanza jioni Ndugai, alimwita, Mbunge wa Manyoni Mashariki (CCM), John Chiligati, ambaye aliongoza kikao cha Kamati  ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kusuluhisha mzozo huo atoe taarifa.
Chiligati aliposimama alilitaarifu Bunge kuwa kwenye kikao cha kamati hiyo, waliwashirikisha Mbunge wa Mtambile  Salim na Wenje kwa ajili ya mashauriano na kuwa  walikubaliana Wenje afute maneno yake na aombe radhi.
Alisema katika kikao hicho, Wenje alikubali ushauri wao wa kufuta maneno yake na kuomba radhi bungeni na akwamba hakuwa na nia mbaya.
“Lakini mheshimiwa Spika katika hali ya kushangaza Wenje hajafuta maneno yake isipokuwa ameyaweka kwa lugha ya Kingereza tu, hivyo kamati imekushauri mheshimiwa Naibu Spika umwamuru ayafute,” alisema Chiligati.
Ndugaia, alisimama na kumpa Wenje dakika tano kujieleza kuhusu tuhuma zilizokuwa zimeelekezwa kwake.
Katika maelezo yake, Wenje alisema hataomba radhi kwa kuwa yote aliyosema ni ya kweli na CUF ilisaini makubaliano ya kuwa mwanachama wa vyama vyenye mrengo wa kiliberari.
“Mkutano uliofanyika Oxford 1997 CUF wakiwa wanachama ulitoka na maazimio kwamba ushoga na usagaji ni mambo yanayokubalika kwamba ni halali kwa  vyama vya mfumo wa mrengo huo, sasa mnataka nifute maneno ambayo ni kweli? niombe radhi kwa kosa lipi, mimi siwezi kuomba radhi kwa kosa ambalo halipo,” alisema.
Salim ambaye aliomba mwongozo asubuhi, alipopewa nafasi ya kuzungumza alisema lazima Wenje afute maneno yake na kuomba radhi la sivyo hotuba ya kambi rasmi ya upinzani haitasomwa bungeni.
Katika hatua ya mwisho, Ndugai alimwomba Wenje kuendelea na hotuba yake kwa kuanza kuomba radhi na ayaondoe maneno katika kifungu cha tatu na badala yake asome kuanzia cha nne.
Wenje aliposimama alianza kusoma hotuba yake kuanzia ukurasa wa nne na kuyaacha maneno yaliyokuwa yamewaudhi CUF asubuhi, lakini wabunge wa chama hicho hawakuridhika na kusimama huku wakizomea.
Wabunge wote wa CUF walisimama na kumtaka Wenje aombe radhi hali iliyomlazimu Ndugai kusimama na kusitisha shughuli za Bunge.
“Waheshimiwa kwa hali ilivyo siwezi kuendesha shughuli za Bunge kwa hiyo nasitisha shughuli za Bunge hadi kesho saa tatu asubuhi,” alisema Ndugai.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment