Mkuu wa Jeshi la
Polisi wa Jimbo la Bavaria na Rais wa Chuo cha Polisi Bavaria cha Nchini
Ujerumani Bw. Wolfgang Sommer akiongea na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini
IGP Said Mwema wakati wakiwa katika kikao cha pamoja
na maafisa wa Polisi Makao Makuu.Bw.Sommer yupo katika ziara ya kutembelea na
kujionea mafanikio ya Jeshi la Polisi Tanzania (Picha na Frank Geofray-Jeshi la
Polisi)
Mkuu wa Jeshi la Polisi wa Jimbo la Bavaria na Rais wa
Chuo cha Polisi Bavaria cha Nchini Ujerumani Bw. Wolfgang Sommer
akimkabidhi zawadi Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Said Mwema
wakati wa ziara ya kutembelea na kujionea mafanikio ya Jeshi la Polisi
Tanzania (Picha na Frank Geofray-Jeshi la Polisi)
Mkuu wa Jeshi la Polisi wa Jimbo la Bavaria na Rais wa Chuo cha
Polisi Bavaria cha Nchini Ujerumani Bw. Wolfgang Sommer akiangalia jinsi
ya uendeshaji wa mafunzo katika Gym ya Polisi iliyopo katika Chuo cha Taaluma
ya Polisi Dar es Salaam (DPA) wakati wa ziara ya kutembelea na kujionea
mafanikio ya Jeshi la Polisi Tanzania (Picha na Frank Geofray-Jeshi la Polisi)
…………………………………………………………..
Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi
Jeshi la Polisi nchini limefaidika kwa kiasi kikubwa na
ushirikiano uliopo kati yake na chuo cha Bavaria cha Ujerumani
katika Nyanja za mafunzo, vifaa na polisi jamii jambo ambalo limewezesha maboresho
ya jeshi hilo kuendelea vyema na kutoa huduma inayostahili kwa wananchi.
Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Mkuu wa Jeshi la Polisi wa
Jimbo la Bavaria na Rais wa Chuo cha Bavaria cha Nchini Ujerumani Wolfgang
Sommer alipotembelea Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na baadhi ya vikosi
vya Jeshi hilo kujionea mafanikio ya Polisi jamii pamoja na changamoto
wanazokabiliana nazo katika utendaji wao wa kuimarisha usalama wa raia na mali
zao hapa nchini.
Akizungumza katika ziara hiyo Kamishna wa Operesheni na Mafunzo
wa Jeshi la Polisi Paul Chagonja alisema ushirikiano baina ya chuo hicho na
polisi umesaidia kwa kiasi kikubwa katika kupata mafunzo ya jinsi ya kuimarisha
mkakati wa polisi jamii pamoja na jinsi ya kuboresha mitaala katika vyuo vyetu
vya polisi.
“Ujerumani ni moja ya nchi zilizoendelea sana duniani hivyo na
sisi kupitia maboresho yetu tuna mambo mengi ya kujifunza ili kuendana na usasa
unaohitajika katika kuwahudumia wananchi wa Tanzania katika nyanja ya
usalama”Alisema Kamishna Chagonja.
Kwa upande wake Mkuu wa Polisi jimbo la Bavaria na Rais wa Chuo
cha Bavaria cha Ujerumani Wolfgang Sommer alisema majeshi ya Polisi hivi sasa
duniani yanakabiliwa na changamoto nyingi kutokana na kuibuka kwa wahalifu
wenye kutumia mbinu zilizoendelea hivyo Polisi wana wajibu wa kujifunza kwa
kasi mbinu hizo.
Bw.Sommer alisema Polisi kote duniani wapo katika maboresho
hivyo kwa siku zijazo majeshi hayo yataimarika katika kupambana na uhalifu na
lengo la ziara yake ni kujifunza mbinu zinazotumiwa na polisi wa Tanzania
katuika kukabiliana na uhalifu.
Katika ziara hiyo alitembelea Kikosi cha matengenezo ya magari
ya Polisi ambacho kwa kiasi kikubwa kilifadhiliwa na Serikali ya Ujerumani
mwaka 1994, Kikosi cha Mbwa na farasi, Chuo cha Taaluma ya Polisi (DPA), Kikosi
cha Polisi Anga pamoja na vikundi vya ulinzi shirikishi vilivyopo katika Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment