Wakati Jeshi la Polisi nchini 
limesema limepata taarifa za mwonekano wa mtu aliyetupa bomu katika 
mkutano wa kampeni wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) 
Arusha,Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe amesema wabunge wake leo hawataingia bungeni.
 
source:/freebongo (38)
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mbowe alisema wabunge hao 
watawasili Arusha kwa ajili ya kuungana na wananchi pamoja na wanachama 
kwenye msiba huo.
Alisisitiza kwamba kuanzia leo mahema yatawekwa viwanja vya Soweto 
kwa ajili ya kuomboleza msiba huo na  mara polisi wakimaliza uchunguzi 
wao na kutoa majibu juu ya vifo hivyo, marehemu hao watasafirishwa.
Wakati Mbowe anatoa kauli hiyo Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk 
Emmanuel Nchimbi akizungumza jana mjini Arusha na waandishi wa habari, 
alisema taarifa za awali zinaonesha mlipuko huo ni bomu la kutupwa kwa 
mkono (grumeti)  na hivi sasa timu ya wataalamu  ikiongozwa na Kamishna 
wa Operesheni Maalumu wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja inaendelea na 
uchunguzi wa tukio hilo.
Naye  Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini,  Inspekta Jenerali wa Polisi 
(IGP), Said Mwema  katika taarifa yake kwa vyombo vya habari ameahidi 
kupambana na kuhakikisha wahusika wanapatikana.
Alitoa taarifa hiyo jana kwa waandishi wa habari Dar es Salaam na 
kusema hadi jana, watu waliothibitika kufa katika tukio hilo ni wawili 
na 68 ni majeruhi.
Waliokufa ni Katibu wa Baraza la Wanawake (Bawacha) wa Chadema, 
Kata ya Sokoni 1, Judith Moshi (25) na mtoto aliyejulikana kwa jina moja
 la Justin.
“Mpaka hivi sasa  watu waliokufa ni wawili  na wengine 68 
wamejeruhiwa na mlipuko huo, lakini naahidi kuwa tutapambana na 
kuhakikisha tunawapata wahusika,” alisema Mwema.
Sanjari na kupatikana taarifa juu ya mtu aliyetupa bomu, Mwema 
alisema  timu ya jeshi hilo imetumwa kutoka makao makuu kwenda Arusha 
kuongeza nguvu katika upelelezi.
Hata hivyo, hakufafanua zaidi juu ya mtuhumiwa huyo kutokana na 
kile alichosema taarifa husika  zinafanyiwa uchunguzi  kabla ya  
kuwakamata watu sahihi waliohusika na tukio hilo.
Kwa mujibu wa IGP Mwema, timu ya polisi kutoka Makao Makuu 
inayoongozwa na makamishna wawili, imeondoka  kwenda mkoani Arusha 
kuongeza nguvu katika operesheni na upelelezi.
Timu hiyo inaongozwa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Paul 
Chagonja na Isaya Mngulu kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, 
wakishirikiana na vyombo vingine vya ulinzi.
Alisema polisi inafanya operesheni kali nchini kote kuhakikisha 
inawatia mbaroni watu wote waliowezesha, waliofadhili na waliotenda 
uhalifu huo.
“Kikubwa wananchi waendelee kuwa watulivu na waendelee kutoa ushirikiano kwa wakati wote uchunguzi ukiendelea,” alisema.
IGP ametaka mtu yeyote atakayekuwa na taarifa za wahalifu hao, atoe taarifa kupitia namba yake ya simu ambayo ni 0754 785557 au kwenye kituo chochote cha polisi ili wakamatwe.
‘Kwa nini  iwe Arusha’ hii ni kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, 
Mulongo aliyoitoa baada ya kutembelea majeruhi katika Hospitali za Mount
 Meru, St Elizabeth pamoja na Hospitali ya Arusha Lutheran Medical 
Centre jijini.
“Nawapa pole sana ndugu zangu wa Chadema, na wana Arusha kwa ujumla
 pamoja na watanzania. Lakini najiuliza kwa nini Arusha …tukio hili 
limenihuzunisha sana na nawaomba tusiingize masuala ya kisiasa, tuache 
polisi wachunguze tukio hili kwani timu ya wataalamu kutoka Jeshi la 
Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) pamoja na wataalamu wengine 
wanachunguza tukio hili na wahusika watachukuliwa hatua.’’
Mulongo ambaye tukio hilo la juzi limekuja ikiwa ni  mwezi mmoja 
tangu kutokea kwa mlipuko katika Kanisa Katoliki la Joseph Mfanyakazi la
 Olasiti, alisema jana anayefanya ulipuaji wa mabomu na kumwaga damu za 
watu mbalimbali na wengine kufa, ipo siku Mungu atamhukumu.
Kati ya majeruhi  59  waliolazwa kwenye hospitali hizo, wawili 
wamehamishiwa Hospitali ya KCMC kutoka Hospitali ya  AICC kwa matibabu. 
Wagonjwa wengi wamelazwa hospitali ya Selian ambao ni 40. Hata hivyo, 
wanane waliruhusiwa baada ya matibabu.
Mkuu wa Mkoa alisema  anajisikia mnyonge kutokana na matukio hayo 
mawili tofauti; mlipuko wa kanisani na la juzi wakati Chadema ilipokuwa 
ikihitimisha kampeni zake za udiwani kwenye kata nne za Themi, Kaloleni,
 Elerai na Kimandolu ambao hata hivyo uliahirishwa kutokana na tukio 
hilo.
Mulongo alitaka wananchi  wasihusishe na masuala ya kisiasa badala 
yake wawaachie polisi kuchunguza tukio hilo. Kwa mujibu wa Mulongo, watu
 kadhaa wamekamatwa.
Katika kipindi kisichozidi miezi miwili, mji wa Arusha umeshuhudia 
majeruhi wasiopungua 130, na vifo vya watu watano vilivyotokana na 
kurushwa mabomu na watu wasiojulikana katika mikusanyiko kanisani na 
kwenye mkutano huo wa siasa wa Chadema.
Katika tukio la mwezi uliopita katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu 
Joseph Mfanyakazi,  watu watatu walifariki na wengine wapatao 59 
kujeruhiwa.
Mmoja wa watuhumiwa ambaye ni dereva wa pikipiki maarufu kama 
bodaboda, Victor Ambrose  alifikishwa mahakamani akidaiwa kuhusika 
katika shambulio hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari, daktari wa hospitali ya Selian,
 Paul Kisanga alisema walipokea wagonjwa 48  kabla ya wanane kuruhusiwa.
Alisema miongoni mwa wagonjwa hao, wamo watoto watano wanne wakiwa 
wa kiume na mmoja wa kike. Mtoto Fahad Jamal (7)  amelazwa kwenye wadi 
ya wagonjwa mahututi chini ya uangalizi wa madaktari.
Hospitali ya St Elizabeth wapo wagonjwa wanane na Mount Meru 
imepokea wagonjwa tisa. Mganga Mkuu wa Mkoa wa hospitali ya Mount Meru, 
Frida Mokiti alisema wamepokea miili ya marehemu wawili ambao ni Judith 
Moshi (25) ambaye ni Katibu wa Baraza la Wanawake (Bawacha)  kata ya 
Sokoni 1, Jijini Arusha pamoja na mtoto aliyejulikana kwa jina moja la 
Justin (13).
Kwa mujibu wa majeruhi wa tukio hilo,  Abraham Samuel waliona kitu 
kikiwa kwenye mfuko wa rambo kikirushwa juu na baada ya muda mfupi 
walisikia vilio na wengine kuzimia.
Kitu hicho kilirushwa kabla ya  Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho 
Taifa, Freeman Mbowe kuhitimisha kampeni za uchaguzi za udiwani wa kata 
nne za Jimbo la Arusha Mjini.
Mlipuko huo unadaiwa kuwa ulitokea jirani na gari la matangazo la 
Chadema, aina ya Mitsubishi Fuso lililokuwa karibu na jukwaa alilokuwa 
akitumia Mbowe.
Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe amedai tukio hilo si la bahati mbaya bali lilipangwa na kundi la watu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema wabunge wa chama 
hicho leo hawataingia bungeni bali watawasili jijini Arusha kwa ajili ya
 kuungana na wananchi pamoja na wanachama wa kwenye msiba huo.
Kwa mujibu wa Mbowe, marehemu Judith atapelekwa mkoani Kilimanjaro 
na Justin atapelekwa mkoani Tabora kwa ajili ya maziko mara baada ya 
polisi kukamilisha uchunguzi juu ya tukio hilo.
Alisisitiza kwamba kuanzia leo mahema yatawekwa viwanja vya Soweto 
kwa ajili ya kuomboleza msiba huo na  mara polisi wakimaliza uchunguzi 
wao na kutoa majibu juu ya vifo hivyo marehemu hao watasafirishwa.
‘’Nimetembelea majeruhi jana hospitalini lakini kwa Hospitali ya
 Selian, Arusha Lutheran Medical Centre majeruhi ni wengi lakini 
walioumia sana ni watoto kuna mtoto mmoja amekatika mkono na mguu ambaye
 ni Sharifa Jumanne na Amiri Ally ana vyuma vitatu mwilini mwake,’’alisema Mbowe.
Ingawa polisi imesema inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kabla 
ya kutoa taarifa kamili, Mbowe aliwaambia waandishi wa habari kwamba 
zipo taarifa kwamba shambulio hilo liliambatana na risasi za moto.
Chama cha Wananchi (CUF) kupitia kwa Mwenyekiti wake, Profesa 
Ibrahim Lipumba, kimelaani tukio hilo na kutaka Serikali ichukue hatua 
za haraka na kukamata waliohusika na matukio hayo iwe fundisho.
“Hatuna sababu na tusijenge utamaduni wa nchi yetu kugeuka eneo 
ambalo palipo na mkusanyiko mabomu yanalipuka, Tanzania ni nchi ya 
amani, kwa matukio haya CUF tunalaani kwa nguvu zote na kutoa pole kwa 
familia zilizoathirika,” alisema Lipumba.
Lipumba alisema kitendo kilichofanyika katika mkutano huo wa 
Chadema ni unyama wa kutisha wenye makusudi ya kundi fulani kutekeleza 
azma yao dhidi ya chama, watu, kundi na viongozi.
Alisisitiza kuwa utamaduni huo wa kufanya unyama katika mkusanyiko 
wa watu  unapaswa kudhibitiwa mapema ili kuepusha madhara mengine ndani 
ya jamii kwa kusababisha vifo, ulemavu wa kudumu na familia tegemezi.
“Tumefikia hatua mbaya sana ya kufanya siasa za mabomu huu ni 
utamaduni unaopaswa kukemewa na kupingwa, matukio haya yanajirudia 
kutokana na Serikali  yenyewe kuyakaribisha kwa kushindwa kuwachukulia 
hatua kali wahusika, tunaomba dola ifanye ifanyalo katika uchunguzi wake
 na kuwakamata na kuwafikisha wahusika kwenye vyombo vya sheria,” alisisitiza.
 

 
 
No comments:
Post a Comment