Rais wa Marekani Barack Obama akiwa na mwenyeji wake Rais Jakaya Kikwete mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam jana. |
Ilikuwa kama ngoma ya wakubwa ambayo watoto hawaruhusiwi kucheza wakati Rais wa Marekani taifa lenye nguvu kuliko yote, Barack Obama, pamoja na mke wake, Michelle na watoto wao, walipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jana kwa ziara ya siku mbili huku ulinzi ukiwa umeimarishwa nchi kavu na angani
Ndege ya Rais Obama ambayo hujulikana kama Air Force One, ilitua uwanjani hapo saa 8:35 na ilichukua takribani dakika tano tangu kutua hadi kusimama eneo la kuteremka.
Saa 8: 46 Obama alijitokeza kwenye mlango wa ndege akiwa amemshika mkono bintiye, Maria, kisha na kupungia mkono viongozi waliokwenda kumlaki wakiongozwa na mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete.
Obama alianza ziara ya nchi tatu za Afrika Alhamisi iliyopita nchini Senegal, kisha kwenda Afrika Kusini Ijumaa Juni 28, mwaka huu ambako alikaa hadi jana alipoondoka kuja nchini kumazia ziara yake ambayo ni ya kihistoria tangua aingie madarakani Januari 20, mwaka 2009 kwa kushinda uchaguzi wa mwaka 2008. Hii ni ziara ya pili barani humo.
Kabla na baada ya kuwasili kwake, hali ya jiji la Dar es Salaam ilikuwa tulivu isiyokuwa na msongamano wa magari wala watu wengi kama ilivyo kawaida ya Jumatatu hasa baada ya wananchi kushauriwa kubaki nyumbani kama hawakuwa na mambo ya lazima ya kuwafanya kuwa barabarani.
Hali ya ulinzi ilikuwa ni ya hali ya juu, kabla ya Rais Obama kuwasili, ukaguzi mkali ulifanywa na maofisa usalama wa Marekani kwani mbali askari, mbwa walitumika kunusa kila silaha iliyokuwa inatumiwa na wanajeshi walioshiriki gwaride la heshima kwa Rais Obama, pia magari yote yaliofika JNIA yalikaguliwa na mbwa hao maalumu wa kutambua vitu vya milipuko.
Katika ukaguzi huo, mbwa wa vikosi vya usalama wa Marekani walitumika kuwanusa wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi na Usalama wa Tanzania (JWTZ) ikiwa ni hatua ya tahadhari kubaini kama kuna milipuko.
Wanajeshi waliokaguliwa na mbwa ni wale walioshiriki gwaride maalum lililoandaliwa kwa ajili ya Rais Obama baada ya kuwasili nchini, ambao ni utaratibu wa kawaida unaoandaliwa kwa marais.
Pia kila gari lililoingia uwanjani hapo, likiwamo lililombeba Rais Obama lilikaguliwa na mbwa kwa kufunguliwa ‘boneti’.
Wakati hayo yakijiri, askari wa Marekani, ambao ni maalum kwa udunguaji wa ndege walikuwa juu ya paa la jengo la vyumba vya watu mashuhuri (VIP) baada ya kuwasili uwanjani hapo.
Baada ya ndege ya Rais Obama kutua, helikopta mbili za ulinzi za Marekani zilikuwa zikifanya doria kwenye maeneo yote ya Posta, maeneo ya Ikulu na JNIA.
Baada ya ndege hiyo kutua, magari mawili ya maofisa usalama wa Marekani yalionekana kufuata ndege iliyomchukua Rais Obama kabla hajashuka.
Saa 8:42 Rais Obama aliyevalia suti nyeusi, shati jeupe na tai nyekundu aliteremka ngazi za ndege ambazo kama ilivyo kwa magari yalikuwa kwenye msafara wake likiwamo alilopanda, imetoka Marekani.
Ilipofika saa 8:50, Rais Obama na Rais Kikwete walipanda kwenye jukwaa lililoandaliwa kwenye uwanja huo na kupigiwa nyimbo za taifa za nchi zao na mizinga 21 kwa heshima yao. Wimbo wa taifa la Marekani ulianza kupigwa na baadaye kufuatiwa na wimbo wa taifa la Tanzania.
Saa 8:53, Rais Obama alikagua gwaride la vikosi vya majeshi ya ulinzi na usalama na baada ya kumaliza alirejea katika jukwaa na kupigwa nyimbo za taifa ukianza wa taifa wa Tanzania na kufuatiwa na wa Marekani.
Baadaye saa 9:00 alasiri, gwaride la vikosi hivyo, vilipita kwa mwendo wa kasi mbele ya Rais Obama na Rais Kikwete, ambao walisimama katika jukwaa maalum.
Ilipofika saa 9:02 utambulisho wa viongozi ulifanywa na Rais Kikwete, wa kwanza kutambulishwa kwa Rais Obama akiwa ni Rias wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na kufuatiwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Viongozi wengine waliotambulishwa kwa Rais Obama, ni Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Davis Mwamunyange.
Wengine ni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki. Pia alikuwako Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Didas Masaburi.
Muda mfupi baadaye, Rais Obama alikagua vikundi vya burudani vilivyokuwapo uwanjani hapo kudhihirisha kunogewa na kufurahia ngoma hizo, naye alicheza, hali iliyomfanya mwenyeji wake, Rais Kikwete kumshangilia. Mkewe Michele naye alikuwa akipiga makofi akishangilia utamu wa ngoma hizo.
Saa 9:09 alasiri alitoka uwanjani hapo na kupanda gari lake yeye na familia yake yenye namba 800-002.
Saa 9:12, ndege ya pili iliyobeba ujumbe wa Rais Obama iliwasili katika uwanja huo na dakika mbili baadaye Rais Obama aliondoka uwanjani hapo.
Kabla ya Rais Obama kuondoka, Rais Kikwete alimtangulia kwenda Ikulu kwa ajili ya kumsubiri ili kumkaribisha.
Barabarani kote alikopita Rais Obama, kuanzia JNIA kupitia Nyerere, Gerezani, Sokoine, Kivukoni Front hadi Ikulu, watu walijitokeza na kujipanga pembeni kumlaki. Umati ulikuwa ni mkubwa sana.
Rais Obama aliwasili katika viwanja vya Ikulu saa 9:30 na kupokewa na mwenyeji wake, Rais Kikwete.
Mamia ya watu waliokuwapo kwenye viwanja vya Ikulu kila mmoja alitaka kumshika mkono Rais Obama, huku Rais huyo na mwenyeji wake pamoja na wake zao, Michele na Salma, nao wakiwashika watu hao mikono.
Bendera za taifa la Marekani na Tanzania zilikuwa zikipeperushwa na watu waliojitokeza kulaki ugeni huo ambao umeweka historia kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa kiongozi wa taifa lenye nguvu kuliko yote duniani.
Kadhalika, Obama anaweka rekodi ya kuiweka pambani Kenya nchi ambayo amezaliwa baba yake mzazi, mara ya pili kwa kuipa mgongo kwa kuhitimisha ziara ya pili ya Afrika baada ya ile ya mwaka 2009 aliyotembelea Ghana na kuimwagia sifa kemkem kuwa inaenzi na kujenga demokrasia kwa kuendesha chaguzi huru na haki bila kujikita katika siasa za kikabila.
No comments:
Post a Comment