BARACK Obama ametua Afrika. Mguu wake wa kwanza ameukanyagia Senegal.
Neno lake kuu akiwa Senegal ni DEMOKRASIA. Ameisifu Senegal kwa kuwa
mfano wa kuigwa katika kukuza demokrasia barani Afrika.
Kisha ametua Afrika Kusini. Jana Jumamosi ametembelea Kisiwa cha
Robben, mahali ambapo Nelson Mandela alifungwa kwa miaka 27. Inahusu
DEMOKRASIA. Bila shaka, Obama ataisifu Afrika Kusini kwa kukuza
demokrasia yake na hivyo kuinua uchumi wake. Maana, pasipo na demokrasia
ni nadra kwa uchumi kukua.
Kesho Barack Obama atatua Dar Es Salaam, Tanzania. Huhitaji kuwa
mtabiri, kujua , kuwa Barack Obama atalitamka neno DEMOKRASIA akiwa
Tanzania. Huenda Obama akaitaja Tanzania kuwa mfano wa kuigwa katika
kudumisha Amani na Umoja miongoni mwa watu wake. Lakini, bado Obama
atasisitiza pia umuhimu wa demokrasia na uhuru zaidi wa vyombo vya
habari barani Afrika.
Obama anaipenda Afrika, ni bara alilozaliwa baba yake mzazi, Dr.
Barack Hussein Obama, Sir. Hivyo, kwa Barack Obama, Afrika ni bara la
asili yake, na Kenya ndiko iliko asili yake. Ndiko liliko kaburi la baba
yake.
Lakini, Obama ana simulizi mbaya juu ya bara hil…..
…na hususan inapohusu demokrasia na uhuru wa watu kujieleza. Obama
hahitaji kutoa mifano ya wengine anapozungumzia wahanga wa kukosekana
kwa demokrasia. Obama ana mfano wa baba yake mwenyewe wa kumzaa; Dr.
Barack Hussein Obama.
Baba yake alikufa kwenye ajali ya gari Nairobi, lakini, ni matokeo ya
kuandamwa na mfumo kwenye Serikali ya Mzee Jommo Kenyatta, kwa vile tu,
baba yake Obama alikuwa anafikiri tofauti na watawala. Na mwishowe
alikuwa anatembea na siri ya aliyemwua mwanasiasa Tom Mboya. Aliitwa na
mamlaka na akaambiwa; ” Funga Mdomo!”
Baba yake Obama alikuwa rafiki wa karibu sana wa Tom Mboya aliyeuawa
katika mazingira ya kutatanisha. Lakini, inaaminika, aliuawa kwa vile
alifikiri tofauti na watawala. Kwenye kitabu kiitwacho; ’ The Bridge’
kilichoandikwa na mwandishi David Remnick, mwandishi anaelezea siku
ambayo Jommo Kenyatta alifika Kisumu na kupokewa na kelele za wananchi
wakimwuliza;
” Tom yuko wapi?” ” Tom yuko wapi?”
Jambo hilo lilimwaibisha sana Jommo Kenyatta. Akalaumu chama cha
Jaramong Odinga cha KPU- Kenya People’s Union kwa kuwagawa wananchi.
Naye Rais Jommo Kenyatta akatamka hadharani; ” Odinga ni rafiki yangu,
lakini anawapotosha wananchi, na anaendelea kuwapotosha watu wa eneo
hili. Tutawapondaponda muwe kama unga. Yeyote anayecheza na maendeleo
yetu tutamwangamiza kama nzige. Msije mkasema sijawaonya.”
Baada ya hapo gari la Jommo Kenyatta lililondoka mahali hapo kwa kasi
huku umati ukilirushia mawe. Polisi hawakurusha mabomu, bali,
walilengesha mitutu yao ya bunduki kwenye umati ule . Watu tisa tisa
walikufa hapo hapo na wengine sabini kujeruhiwa.
Siku mbili baadae Jommo Kenyatta akawamata Jaramongi Odinga na
viongozi wengine kadhaa wa KPU. Walishtakiwa kutaka kumpindua Rais Jommo
Kenyatta. Odinga akawekwa jela kwa miaka miwili, na kila msomi mwenye
asili ya Kijaluo alionja joto ya jiwe. ( The Bridge, David Remnick, page
67-68)
Ndio maana ya kusema, kuwa hayo machache tu kwenye simulizi mbaya ya
Obama juu ya Afrika, yanamfanya Barack Obama kuwa wakili mtetezi wa
kweli wa kupigania demokrasia katika Afrika. Obama anaposisitiza umuhimu
wa uwepo wa demokrasia na uhuru wa vyombo vya habari na wanahabari
barani Afrika anamaanisha anachosema na hasemi asichomaanisha.
Na hapa tuyakumbuke maneno ya Obama pale alipotoa hotuba ya kutawazwa kuwa Rais wa Marekani kwa mara ya pili. Obama alisema;
” Taifa la Marekani ni mahali ambapo kila mmoja ana nafasi ya
kutimiza ndoto yake. Ndoto ya kuwa yeyote yule, bila kujali rangi, dini
au jinsia yako. Wakati tukiyaongea haya hapa, kuna wanadamu wenzetu
mahali pengine duniani wako gerezani kwa kosa la kufikiri tofauti. Kwa
kosa la kuonyesha dhamira ya kutimiza ndoto zao.”- Barack Obama.
Naam, kuna mahali fulani hata Barack Obama anajua, kuwa kama
angeliishi Kenya, kwenye nchi ya baba yake, na kuwa na ndoto ya kuwa
Rais wa Kenya. Akaitamka hadharani na kuonyesha kwa matendo, basi,
huenda, sio tu angefungwa gerezani kwa kufikiri tofauti na watawala,
bali, huenda leo angeshakuwa amezikwa kando ya kaburi la baba yake kule
Kerego, Kisumu, Kenya.
Ndio maana, tunaamini, kuwa kauli za Barack Obama kuhusu demokrasia
ni za dhati, na aendelee kuwa wakili wa kweli wa kutetea demokrasia
kwenye bara la asili ya baba yake. Ni kwa vile, bila uwepo wa demokrasia
ikiwamo uhuru wa kujieleza, Afrika itabaki kuwa bara la giza. Tuna
nafasi na kila sababu za kurudisha nuru kwenye bara hili.
Karibu sana Tanzania, Barack Obama. Mungu Ibariki Afrika (77)
No comments:
Post a Comment