ULINZI WAIMARISHWA KATIKA NYUMBA ZA IBADA MKOANI KILIMANJARO
KUTOKANA
na tishio la vitendo vya kigaidi katika maeneo ya nyumba za ibada,
Jeshi la Polisi Mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, limeanza mkakati wa
kuweka ulinzi katika nyumba za ibada wakitumia dhana ya Polisi Jamii.
Akizungumzia
mkakati huo kwa waumini wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Kristu Mfalme
lililoko Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Moshi,
(OCD), Deusdedit Kasindo, alisema lengo ni kujihami na matukio hayo
kabla hayajatokea.
"Wenzetu katika nchi jirani, magaidi wamevamia
Kanisa, kuua watu na wengine kujeruhiwa...nasi tumeona ni bora tukaanza
kuchukua hatua kupitia dhana ya Polisi Jamii hivyo tunaomba ushirikiano
wetu," alisema.
Aliongeza kuwa, kwa kuanzia jeshi hilo limetoa wito
katika madhehebu mbalimbali wilayani humo kuanzisha vikundi vya ulinzi
na usalama pamoja na kuviimarisha vilivyopo viweze kushirikiana na
polisi kukabiliana na hali hiyo.
"Kumekuwa na vikundi
vinavyojihusisha na wizi wa baiskeli, pikipiki na baadhi ya vitu ndani
ya magari kwenye nyumba za ibada, lakini kwa hili la uvamizi ambao
umeanza kushamiri hatuna budi kujiimarisha zaidi," alisema.
OCD
Kasindo alisisitiza kuwa, tayari jeshi hilo limezunguka katika Makanisa
na Misikiti mbalimbali mjini humo ili kutoa wito huo ambapo jeshi lipo
tayari kutoa mafunzo yanayohusiana na ulinzi kama vikundi hivyo
vitaundwa.
Alisema wameamua kusisitiza matumizi ya Polisi Jamii
kutokana na jeshi hilo kuwa na askari wachache ukilinganisha na idadi ya
wananchi wanaohitaji huduma za polisi maeneo mbalimbali.
"Matokeo
ya sensa yaliyotoka hivi karibuni, askari mmoja ana jukumu la kulinda
raia kati ya 1,300 na 1,500, hivyo ni muhimu raia wenyewe wakaanza
kujichunga kwa asilimia 90 na asilimia 10 iliyobaki, usalama wao
utasimamiwa na polisi," alisema. Kwa upande wake, Paroko wa Parokia hiyo, Padri Crispin Jumanne, alilipongeza jeshi hilo kwa uamuzi huo uliokuja wakati mwafaka.
"Mkakati
huu utasaidia kuwaondoa hofu waumini ambao baadhi yao walianza kuogopa
na kushindwa kuhudhuria ibada...kwa niabaya Baba Askofu Isaack Amani,
tunaahidi kutoa ushirikiano ambao tutauanza mara moja," alisema.
Alitoa
wito kwa waumini wa kanisa hilo, kuliunga mkono jeshi hilo kwa kuwapa
ushirikiano wao ili waweze kufanikisha azma ya kuhakikisha waumini
wanafanya ibada kwa amani bila hofu.
Source: Majira
No comments:
Post a Comment