KILIMANJARO Hospitali ya rufaa ya KCMC iliyopo mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, imetunukiwa tuzo ya kimataifa ya utendaji bora wa kutibu wagonjwa kwa kutumia teknolojia ya upasuaji wa kutumia njia ya matundu badala ya kufanya upasuaji wa kawaida, utaalamu ambao madaktari wa hosptali hiyo wameupata katika chuo cha utafiti na upasuaji cha hospitali hiyo.
Daktari bingwa wa kitengo cha upasuaji cha hosptali hiyo Dkt. Kondo Chilonga, alisema wameipata tuzo hiyo, baada ya taasisi zaidi ya 200 duniani kushindanishwa nchini Uingereza, kwa kuonesha kazi mbalimbali za utoaji wa huduma za afya ambapo KCMC ilitumia mfumo wa kipekee wa upasuaji kwa njia ya matundu na kutoa matokeo bora, kama yanayofanyika katika nchi zilizoendelea.
Alisema mafanikio hayo ni sehemu ya utekelezaji wa matokeo makubwa sasa, katika kuleta afya njema kwa wananchi na kwamba, toka wameanza kutoa huduma kupitia mfumo huo, wamefanikiwa kutoa matibabu kwa wagonjwa zaidi ya 600, kutoka katika maeneo mbalimbali hapa Tanzania.
Aidha Dkt. Chilonga alifafanua kuwa mfumo wa upasuaji kwa kutumia matundu unafaida nyingi ikiwemo mgonjwa kukaa hosptalini kwa siku moja ukilinganisha na siku saba anazokaa mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji kwa njia ya kawaida.
Akipokea tuzo hiyo Askofu mkuu wa kanisa la KKKT, Dkt. Alex Malasusa, pamoja na kuwapongeza watendaji wa kituo cha upasuaji cha KCMC kwa juhudi walizofanya, amewaasa kutobweteka na mafanikio hayo, na badala yake waongeze bidii ili kuondoa adha kwa wagonjwa hapa nchini.
Profesor Raimos Ulomi, ambaye ni kaimu mkurugenzi mkuu wa hosptali ya rufaa ya KCMC, alisema kutokana na ongezeko kubwa la wagonjwa hospitalini hapo, wameweka utaratibu wa kuwapatia mafunzo baadhi ya madaktari wa hosptali hapa nchini, ili waweze kuwahudumia wagonjwa katika hospitali zao badala ya kuwapelekwa katika hospital ya KCMC.
No comments:
Post a Comment