KILIMANJARO wafanyabiashara wa
soko la Uchira, katika wilaya ya Moshi vijijini, mkoani
Kilimanjaro, wapo hatarini kupatwa na magonjwa ya mlipuko kutokana na
kukosa huduma ya vyoo na maji, hivyo kulazimika kujisaidia kwenye mifuko ya rambo
na kutupa kinyesi hicho hovyo.
Hali hiyo imejitokeza kutokana na wafanyabiashara hao kukaa kwa muda mrefu katika soko hilo bila
ya kuwa na huduma ya vyoo na maji katika sehemu hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwanaharakati wa mtandao huu wa "Kilimanjaro Official Blog", baadhi ya wananchi
wa kijiji hicho, walisema hali hiyo ya ukosefu wa vyoo inasikitisha kutokana
na wafanyabiashara hao kwenda kujisaaidia kwenye vibanda vinavyo zunguka soko
hilo na kutupa hovyo uchafu huo.
Walisema kwa takribani miaka 10 soko hilo halijawahi kuwa
na vyoo wala maji, licha ya wakala ambaye amepewa tenda ya kukusanya ushuru
akiendelea kuwatoza fedha hizo huku huduma za kijamii zikikosekana sokoni hapo.
Jenipha Marandu, alisema soko hilo linakabiliwa na harufu
mbayo kutokana na watu kujisaidia kwenye mifuko ya rambo na pindi wanapokwenda hospitali
wamekuwa wakigundulika na ugonjwa wa maambukizi katika mfumo wa kutolea mkojo (U.T.I)
Jeremiah Joseph, mkazi wa Uchira alisema kutokana na ukosefu
wa vyoo katika eneo hilo wafanyabiashara hao wamekuwa wakijisaidia kwenye vibanda vilivyopo karibu na soko hilo na
kuweka kinyesi hicho kwenye mifuko ya rambo na kuitupa katika shimo ambalo
lilichimbwa na kuachwa wazi bila kukamilishwa.
Njarita Japutia, mkazi wa kijiji cha Uchira alisema tangu
soko hilo liwepo halijawahi kuwa na choo, pia hakuna dalili ya kupata vyoo wala
maji katika soko hilo, wala hawajawahi kusomewa taarifa ya mapato na matumizi ya michango yao
kwa kipindi cha miaka mitano.
Alifafanua kuwa soko hilo linamzabuni ambaye amekuwa
akiwatoza ushuru wafanyabiashara hao licha ya kuwa huduma za kijamii zinazotakiwa
kuwepo katika soko hilo hazipo, licha ya wafanyabiashara hao kuendelea
kuchangishwa fedha na uongozi huo wa kijiji.
Akizungumzia Changamoto hizo mtendaji wa kata ya Kirua vunjo
Kusini, Jovita Mosha alisema kero za ukosefu wa choo katika soko hilo zipo,
licha ya kukataa kuwa hakuna wafanyabiashara ambao wanajisaidia na kutupa
kinyesi hicho katika eneo hilo.
No comments:
Post a Comment