KILIMANJARO wananchi wa kijiji cha Mshiri wilayani Moshi mkoani
Kilimanjaro wameandamana na kuchukua uamuzi wa kufunga kwa makufukuli chuo cha
ufundi Mshiri wakipinga chuo hicho kubinafsishwa kwa mwekezaji.
Wananchi hao walifikia hatua hiyo baada ya kupata taarifa za
kuaminika kwamba uongozi wa chuo hicho unataka kuuza chuo na kukabidhi kwa
mwekezaji bila ya kuwashirikisha
wananchi.
Wakizungumza katika mkutano mkuu wa kijiji hicho uliofanyika juzi
nje ya ofisi ya kijiji, baadhi ya wananchi hao Winford Mosha na Given Estomihi,
walisema wanashangazwa na kitendo cha uongozi wa chuo hicho kutaka kubinafsisha
chuo, huku uongozi huo ukifahamu fika
kwamba kilijengwa kwa nguvu za wananchi.
Walisema chuo hicho kilijengwa mwaka 1996 kwa michago ya
wananchi, ambapo kila mwananchi alichanga shilingi 1000, huku wakishirikiana na
mfadhili mmoja aliyejulikana kwa jina la Caty Allen na kwamba hawapo tayari
kuona chuo hicho kikibinafsishwa kwa mwekezaji yeyote.
Walisema mapatano ya awali wakati wa makabidhino ya chuo
hicho kwa mfadhili huyo, yalikuwa ni kukiendesha na iwapo itashindikana kukufanya
hivyo akirudishe kwa serikali ya kijiji na sio kukibinafsisha au kukiuza kama wanavyotaka kufanya.
Aidha walisema ni vema chuo hicho kikarudishwa kwenye mikono
ya uongozi wa serikali ya kijiji, na kukiendesha wenyewe bila kuwepo kwa
misaada ya mfadhili huyo, kutokana na kwamba hana nia njema na wananchi wa eneo
hilo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Mshiri Wilson Mosha
alisema maazimio waliofikia katika mkutano huo ni kuendelea kufunga chuo hicho
mpaka pale muafaka utakapopatikana, na kwamba jambo hilo kwa sasa liko chini ya
mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Moshi.
Aidha alisema ni vema serikali ikaiingilia kati suala hilo,
kwani ni wazi linawakatisha tamaa wananchi kuendelea kuchangia miradi ya
maendeleo katika maeneo wanayoishi, kutokana na kwamba miradi hiyo imekuwa
ikitumika ndivyo sivyo na kuwanufaisha watu wachache badala ya wajamii.
No comments:
Post a Comment