KILIMANJARO JESHI la polisi mkoani Kilimanjaro linamshikia mtu mmoja
aliyefahamika kwa jina la John Macha, kwa tuhuma za kuchoma nyumba ya jirani
yake kwa madai ya kulipiza kisasi baada ya jirani huyo kudaiwa kuhusika katika
mauaji ya ndugu yake Faustine Macha.
Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari mkoani
Kilimanjaro, Kaimu kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Koka Moita, alisema tukio hilo
lilitokea majira ya saa 4:00 subuhi januari 29 mwaka huu katika kijiji cha
kanango wilayani Moshi vijijini.
Alisema afisa mtendaji wa kijiji hicho Kamilius Kessy (56)
alibaini kuwa nyumba hiyo ilikuwa inateketea kwa moto baada ya kuchomwa na mtuhumiwa kwa kile alichokua
anadai analipiza kisasi kutokana na mwenye nyumba huyo kuhusika katika mauaji ya
ndugu yake.
Mwenye nyumba huyo anadaiwa kufanya na kushiriki katika
mauaji ya ndugu yake aitwaye Faustine Macha kwa kumpiga na rungu kichwani na kisha
kumshambulia kwa kipigo sehemu mbalimbali za mwili wake jambo lililo sababisha
kifo chake januari 28 mwaka huu majira ya saa 12 asubuhi.
Kamanda alisema nyumba hiyo iliyokuwa imejengwa kwa matofali
ya udongo na kuezekwa kwa makuti iliteketea na mali zote zilizokuwepo ndani ya
nyumba na kwamba thamani halisi ya mali iliyo teketea bado haijajulikana mpaka
sasa.
Aidha alisema tukio hilo limefanyika wakati mwenye nyumba huyo
akiwa ametoroka kusiko julikana kutokana na tuhuma za mauaji zinazo mkabili na kwamba uchunguzi zaidi wa
tukio hilo unaendelea ili kubaini chanzo halisi cha tukio.
Alisema tukio hilo halijasababisha madhara yoyote kwa
binadamu na kwamba mtuhumiwa huyo anaendelea kushikiliwa na jeshi hilo kwa
mahojiano zaidi.
No comments:
Post a Comment