KILIMANJARO halmashauri ya wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, inakusudia kuanza ujenzi wa
choo kwenye soko la mboga na matunda, inalotumiwa na wafanyabiashara
pamoja na wanunuzi katika eneo la Uchira wilayani hapa.
Ujenzi
wa choo hicho unatarajiwa kuanza mwezi Februari mwaka huu, baada ya
halmashauri hiyo kufanya makadirio ya ujenzi na gharama halisi za
kutekeleza mradi huo, ambao ni muhimu kwa wafanyabiashara wa eneo hilo.
Akizungumza
na mwanaharakati wa mtandao huu wa Kilimanjaro Oficial Blog ofisini kwake, mkurugenzi wa halmashauri hiyo
Fulgence Mponji, alisema kuwa kukwama kwa ujenzi wa choo hicho
kulitokana na makadirio ya mhandisi wa halmashauri kuzidi gharama
zilizowekwa kwenye bajeti ya utekelezaji.
Hata
hivyo amefafanua kuwa makadirio ya ujenzi yaliyotolewa na mhandisi wa
halmashauri hiyo yalionesha ujenzi huo utagharimu kiasi cha shilingi
milioni sita, juu ya fedha zilizotengwa kiasi cha shilingi milioni tano.
Awali
watumiaji wa soko hilo la Uchira, walilalamikia ukosefu wa choo, hivyo
kuwaweka kwenye hatari ya kupatwa na maambukizi ya magonjwa ya mlipuko.
Wafanyabiashara
hao walisema soko hilo ambalo pia linakabiliwa na changamoto ya
upatikanaji wa huduma ya maji, imewalazimu wafanyabiashara kujisaidia kwenye mifuko ya rambo na kuitupa hovyo.
Changamoto
hizo zilizodumu kwa zaidi ya miaka kumi sasa imeendelea kuwa kero kwa
watumiaji wa soko hilo, ambao wamelalamikia kukosa huduma hiyo kwa muda
mrefu licha ya kuwepo wakala aliyepewa zabuni ya kukusanya ushuru bila
kupata huduma hizo muhimu za kijamii.
No comments:
Post a Comment