Rais, Dk Jakaya Kikwete, amekiri kuwa bado taifa linakabiliwa na uhaba mkubwa
wa madaktari, licha ya kuwepo kwa jitihada za dhati zinazofanywa na Serikali yake
ya kumaliza tatizo hilo.
Rais Kikwete alibainisha hayo
wakati wa ziara yake Mkoani Mkoani Kilimanjaro, ambapo alizindua jengo la
upasuaji katika Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi, pamoja na jengo la kitega uchumi
lililojengwa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Katika hafla hiyo ambayo pia
ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Naibu Waziri wa Afya, Steven
Kebwe, pamoja na viongozi wa kisiasa, Rais Kikwete alisema kuwa uhaba uliopo
nchini wataalamu wa afya ni mkubwa
ukilinganisha na nchi zilizoendelea.
Alisema kuwa kwa sasa daktari
moja nchini anahudumia wagonjwa 30,000 hadi 50,000, huku muuguzi mmoja
akihudumia hadi wagonjwa 23,000.
Hata hivyo alisema kuwa idadi
hiyo ya madaktari na wauguzi ni tofauti kwa nchi za ulaya ambapo nchi nyingi
ambazo amekuwa akitembelea daktari mmoja na muuguzi huudumia wagonjwa 300 hadi
500.
Kutokana na changamoto hiyo
Rais Kikwete alisema kuwa Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali ikiwemo
kuwasomesha madaktari, pamoja na kuongeza vyuo vya wataalamu wa afya.
Alisema jitihada za Serikali
zimeanza kuzaa matunda kwa baadhi ya vyuo ikiwemo chuo kikuu cha
Dodoma, Muhimbili, ambapo mwaka jana chuo kikuu cha UDOM kilianza wataalamu wa
uuguzi ambapo mwaka huu wanatarajia kupata wataalamu wa udaktari.
Kwa upande wa chuo cha
Muhimbili Rais alisema wamepanua wigo wa kupokea wanafunzi wa taaluma ya afya
kutoka wanafunzi 250 hadi kufika 300 huku Serikali ikiendelea kufungua vyuo
vipya vya kufundisha wataalamu wa afya.
Akisoma risala kwa Rais Kikwete, kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi Dk. Endrew Quaker, alisema kuwa
hospitali hiyo imekaa kwa zaidi ya miaka mitano bila kuwa na huduma ya upasuaji
kwa wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.
Alisema kukamilika kwa jengo
hilo kutapunguza adha kwa akina mama wajawazito, wazee, watoto pamoja na
wagonjwa wengine kwenda kwenye hospitali binafsi ambazo wanapata huduma hiyo
kwa garama kubwa.
No comments:
Post a Comment