Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, amesema Tanzania imejipanga kikamilifu kushiriki na kushinda katika wimbi jipya la uwekezaji wa nishati duniani, wakati ambapo usalama wa nishati umekuwa ajenda kuu kutokana na changamoto za minyororo ya ugavi zinazosababishwa na masuala ya kijiografia na kisiasa.
Akizungumza leo, Novemba 2, 2026, katika Mkutano wa Kimataifa wa Nishati (ADIPEC 2026) unaofanyika Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Dkt. Homera ameeleza kuwa Tanzania imeweka wazi mikakati ya kuvutia mitaji ya ndani na ya kimataifa, ikionyesha fursa kubwa ilizonazo na hatua mahsusi zinazochukuliwa kuimarisha mazingira ya uwekezaji.
Dkt. Homera amebainisha kuwa Tanzania inazo rasilimali za nishati zinazoweza kuibua uwekezaji mkubwa, ikiwemo Gesi Asilia ambapo takribani futi za ujazo trilioni 57.54 (TCF), zenye uwezo wa kuendeleza miundombinu ya usindikaji (LNG) na Mini - LNG na uzalishaji wa umeme kama umeme wa Maji wa Mradi wa Julius Nyerere (MW 2,115), Mradi wa umeme wa jua wa Kishapu (MW 150), miradi ya upepo mkoani Singida, na nishati ya jotoardhi mikoa ya Mbeya na Songwe.
Aidha, nafasi ya kijiografia ya Tanzania inaiwezesha kuwa kitovu cha biashara ya nishati kikanda kupitia Eastern Africa Power Pool na Southern Africa Power Pool, jambo linaloongeza mvuto wake kwa wawekezaji.
Kwa upande mwingine Dkt Homera ameeleza kwamba Ili kushinda ushindani wa kimataifa wa mitaji,upo umuhimu wa sera thabiti na endelevu kupunguza hofu na gharama kwa wawekezaji, ufanisi wa kisheria na udhibiti kupunguza urasimu, kuweka ushuru unaotabirika, na kurahisisha taratibu za biashara, miradi inayoweza kufadhilika ili kuandaa miradi yenye tafiti za kina, mikataba thabiti ya ununuzi wa umeme, na uwazi wa kifedha kwa mashirika yanayonunua nishati na vyanzo mbalimbali vya fedha ikiwemo kutumia Serikali, benki za biashara, wawekezaji wa kimataifa, na taasisi za kimataifa za kifedha.
Akihitimisha wasilisho lake, Dkt. Homera ameeleza kuwa Tanzania chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imejipambanua kupitia Mkataba wa Kitaifa wa Nishati (National Energy Compact) wenye lengo la kuhamasisha uwekezaji binafsi wa takribani dola za Marekani bilioni 4.039, vipaumbele vikuu vikijumuisha manunuzi ya nishati jadidifu yenye ushindani, uwekezaji katika miundombinu ya usafirishaji wa umeme na ushirikiano thabiti kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP).
Kwa hatua hizi, Tanzania inaonyesha dhamira ya dhati ya kubadilisha rasilimali na mipango kuwa miradi halisi yenye mvuto wa kimataifa, na hivyo kujihakikishia nafasi ya kipekee katika soko la nishati duniani ameeleza Dkt. Homera.

No comments:
Post a Comment