Leo nimeamua kusawazisha dhana
potofu hususan kuhusu muziki wa vijana ambao wapigaji wake ni vijana, mashabiki
wake ni vijana na hata wengi wa wadau wake ni vijana pia.
Na wengi huchukulia kimakosa
kuwa bongo-fleva ni muziki wa kizazi kipya, inaweza kuwa
sawa kwa sasa, lakini pia inaweza kuwa si sawa kwa kuwa bongo-fleva si kizazi kipya
cha kwanza hapa
nchini.
Hali ya muziki huo kuitwa wa kizazi kipya
inaweza kuwa
imesababishwa na ule mshawasha wa kutaka kujitambua, kutokana na sababu
mbalimbali tutakazozianika kwenye mada yetu ya leo.
Kwanza tuelewane
kuwa kama siku
zinavyokwenda na kusababisha miaka ipite, hata muziki nao huathiriwa na wakati
kutokana na mahitaji husika ya jamii kwa wakati husika.
Na hiyo husababisha kaliba jipya
la kizazi
cha umri fulani, ambacho huja na ubunifu wake na kutaka kujitambua katika mabadiliko
ya wakati unaowahusu zaidi wao wenyewe kwa kizazi chao.
Kutokubalika huchochea kizazi
kijitambue mdau wangu, kwa msingi wa niliyoyaeleza hapo
juu nikufahamishe kuwa, kwa hapa nchini kizazi kipya cha kwanza kimuziki
kilianza mnamo
kabla ya miaka ya mwishoni mwa 1950 kutokana na sababu zilizokuwepo wakati huo.
Hiyo ilitokana na wanamuziki wa
kwanza kabisa
wa muziki wa dansi, kuacha kunakili nyimbo za Kizungu kutoka kwenye santuri na kutumbuiza kwenye
social clubs.
Badala yake wakagubikwa na homa ya
Kilatino (Latino Fever), iliyolikumba eneo kubwa la Afrika kuanzia Afrika Magharibi,
Kati na Mashariki,
kwa kuwa mipigo ya Kilatino ilishabihiana vyema kabisa na mipigo ya Kiafrika.
Hilo halikutokea kwa bahati
mbaya, kwa kuwa nchi za Ulatino (Marekani Kusini) zina vizazi vingi
vya watu ambao ni matokeo ya uzao mchanganyiko wa Waafrika na watu wa
Ughaibuni.
Na haishangazi ule muziki wao
kuwa na chembe chembe za Kiafrika, kama ulivyo
muziki wa Wamarekani weusi au Marasta
wa Carribean au wapigani wa mitindo kama cumbya, charanga, patcheco, merengue
nakadhalika, walioko kwenye visiwa vya Cuba, West Indies, Guyana, Dominica, Jamaica na
Haiti.
Tukirudi hapa nchini, wakoloni
hawakupenda kabisa muziki wa kizazi kipya wa wakati huo hivyo waliushutumu
sana. Lakini hawakuweza kuuzuia maana watu waliupenda zaidi
muziki huo, kuliko ule muziki wao wa kikasumba (wa kikoloni).
Kwa maana
hiyo ukihesabu kutoka hapo, kuna urithi wa wanamuziki wengi tangu wakati huo na
wote hao ni kizazi kipya kwa maana ya
awamu mpya kimuziki.
Vuka toka hapo hadi nyakati za kina
Salum Abdallah, Juma Kilaza, kisha tuama katika nyakati za kina
Mbaraka Mwinshehe hadi zama za kina Marijani Rajabu, halafu kizazi cha
kina Hemedi Maneti, Hamza Kalala, Juma Ubao na hadi kufikia kizazi cha
kina Shabani Dede, Hassan Bitchuka na kizazi cha sasa cha mtiririko huo huo sawia.
Kuna wanamuziki wengi na hatuwezi
kuwataja wote, lakini tofauti ya vizazi hivyo na hiki cha sasa ni aina ya muziki
na kurithishana ujuzi kama nitakavyoeleza kwenye
sehemu ya kipengele kinachofuata.
Ukiangalia vizazi
vilivyopita, ni kwamba vilirithishana ujuzi kutokana na kupiga muziki
unaorandana au wa aina moja.
Kwa hiyo ushirikiano wa vizazi
hurithisha ujuzi muhimu baina ya kizazi kinachopokea kutoka kilichopita, kisha
huendeleza ujuzi
husika. Ubunifu huongezeka na kila ubunifu mpya wa wanamuziki wapya ni kizazi
kipya, lakini kwa bongo-fleva kuna tofatuti na vizazi
vingine tulivyovitaja.
Kwanza ni
mtindo uliokumbatia silika za utamaduni uliokuja nyakati za baadaye,
baada ya kufunguliwa milango kwa mabadiliko ya sera za kisiasa
hapa nchini.
Ni Utamaduni wa
kigeni ambao walioanzisha bongo-fleva waliuchanganya na mambo ya
nyumbani, ili kupata kilichoitwa muziki wa nyumbani wenye ladha ya kimataifa.
Tumeshawahi kueleza jambo
hili tulipochambua reggae, bongo-fleva na hip-hop kwenye safu hii.
Kwamba hii inayoitwa bongo-fleva
kimsingi iliundwa na wanamuziki wa reggae na rap wa hapa nchini, ambao waliamua
kuungana baada ya kutengwa na wahafidhina waliowaona kama tishio
kwa mirindimo yao ya dansi.
Na hata jina la mtindo huo
lilitokana na kujitetea kwa wana-reggae na wana-rap hao dhidi ya shutuma walizoelekezewa,
kwa kudai kwamba wanachokipiga wao ni fleva za Kibongo kimataifa.
Baadaye maneno
hayo yakabadilishana nafasi, neno ‘Bongo’ likawa mwanzo na ‘fleva’ mwisho na kuzalisha
jina la bongo-fleva.
Lakini hadi wakati huo maneno
hayo yanabadilishana nafasi, wanamuziki wa reggae na rap wakawa wameshajitenga
na mkusanyiko huo wa uasisi.
Hiyo ilitokana na muziki huo
kuingiliwa na vijana walioonekana kutokuwa na silika za ukweli
halisi wa muziki huo, hapo ndipo silika za ubitozi na mapenzi
zikatawala mno ndani ya muziki huo.
Hiyo ikarejesha upya zile shutuma kuwa
ni muziki wa kizazi kipya kutoka kwa wale wahafidhina wa kwanza, ambao
kuna wakati waliukubali baada ya kuona waasisi wa mwanzo wakipiga muziki hai.
Lakini shida kubwa inayosababisha
kusiwe na muendelezo wala kurithishana baina ya wanamuziki wa bongo-fleva, ni
kutokubali kwao kuchota ujuzi kwa wakongwe wa muziki hata kama hawapigi
mitindo kama
yao.
Lakini ajabu moja wakishaamua
kuvuka madaraja
ya mafanikio
na kuanzisha bendi, huelemea kwenye mirindimo hiyo hiyo ya wakongwe ambao
huwakacha mwanzoni.
Naomba niishie hapa
By Chalii wa Moshi
No comments:
Post a Comment