MUHIMBILI WAITING ROOM
Hali ya
afya ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka
imeendelea kuwa siri, huku mipango ya haraka ya kumpeleka nchini India
kwa matibabu zaidi ikifanywa na madaktari wenyewe wanaodaiwa kukataa
msaada wa Serikali.
Inaelezwa
hisia za madaktari dhidi ya Serikali kuwa huenda ina mkono katika
kutekwa na kuteswa kwa kiongozi huyo wa mgomo wa madaktari, ndizo
zinazowasukuma kuizuia Serikali kushiriki katika kumpatia tiba Ulimboka
ambaye kufikia leo asubuhi alikuwa anatibiwa na jopo la madaktari katika
Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI).
Kuzuiwa
kwa Serikali kuchangia tiba za Ulimboka kulithibitishwa leo na Msemaji
wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamaja aliyesema kuwa,
Serikali ilikuwa tayari kutoa msaada wa kumsafirisha Dk Ulimboka kwenda
India kwa matibabu zaidi, lakini madaktari wamegomea msaada huo wa
Serikali.
Alisema
wizara hiyo ilipata taarifa kwamba Dk Ulimboka alikuwa anahitajika
kupata matibabu zaidi nchini India au Nairobi, Kenya na hivyo iliamua
kutoa msaada wa usafiri na matibabu kwa daktari huyo, lakini madaktari
wenzake wamegoma Serikali kushiriki katika suala hilo.
Habari
kutoka Muhimbili zilisema zilikuwa zinahitajika Dola za Marekani 40,000
(zaidi ya Sh milioni 60) kumwezesha Dk Ulimboka kusafirishwa nje kwa
matibabu zaidi, na mwito ulitolewa kwa wahisani na wasamaria kujitolea
kusaidia mpango huo.
Na
kufikia leo mchana, habari zilizonaswa zinasema madaktari na baadhi ya
makundi ya watu, wamekuwa wakikamuana kuhakikisha wanapata fedha za
kumsafirisha Dk Ulimboka.
Huku
mgomo ukiendelea na kuwaumiza wagonjwa katika taasisi ya MOI na
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, madaktari wameunda Jopo la Madaktari
sita wakiongozwa na Profesa Joseph Kahamba kumtibu na kumlinda Dk
Ulimboka hospitalini hapo.
Wakati
mipango ya safari ikikamilishwa leo, milango ya MOI iliendelea kuwa
chini ya ulinzi wa madaktari wenyewe, huku wageni wachache wakiruhusiwa
kuingia ndani, huku wageni wengine wakiwemo waandishi wa habari na
wapigapicha wakiagizwa kusubiri maelekezo zaidi.
Hali
ya ulinzi ilionekana pia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH)
huku shughuli zikionekana kusimama, ikiwa pamoja na kutoonekana kwa
pilika za wauguzi na ndugu wa wagonjwa.
Aidha,
kutokana na mazingira yaliyowekwa na madaktari, ilikuwa ni vigumu kwa
watu wa nje kuweza kuingia MOI ambalo Dk Ulimboka anapatiwa matibabu.
Wagonjwa
waliokuwa wamekusanyika nje ya hospitali hiyo wakisubiri huduma
walilaani kuendelea kwa mgomo huo huku wakiziomba pande hizo mbili
zinazovutana kumaliza mgogoro uliopo ili kuwezesha huduma kurejea katika
hali ya kawaida.
Wakati
mgomo ukiendelea kutesa wananchi, Serikali imechukua hatua kadhaa za
kunusuru maisha ya wagonjwa ikiwa pamoja na kuingia makubaliano ya
kushirikiana na hospitali binafsi kadhaa zikiwemo TMJ, Regency, Aga
Khan, Hindu Mandal, CCBRT za jijini Dar es Salaam na ile ya Jeshi
iliyopo Lugalo.
Alisema
hatua hiyo ilifikiwa kutokana na maelekezo yaliyotolewa na Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye alisema Hospitali ya Lugalo ambayo ni ya
Jeshi itatumika kama Hospitali ya Rufaa.
"Serikali
itaelekeza nguvu zake moja kwa moja katika Hospitali za Mwananyamala,
Amana na Temeke ambako hakuna mgomo, ili kuhakikisha kwamba hazilemewi
na mzigo wa wagonjwa,” alisema.
Utafiti umebaini huduma kuendelea bila matatizo katika hospitali hizo za Amana, Temeke na Mwananyamala.
No comments:
Post a Comment