Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Tuesday, August 21, 2012

Dk Slaa ambana Pinda atoe maelezo juu ya fedha na Mali zilizochangwa na Watanzania wakati wa Maafa Mbalimbali...!Viongozi wa Chadema wakishiriki chakula cha mchana kilichoandaliwa na wananchi wa mkoa wa Morogoro baada ya kusitisha mikutano ya Operesheni Sangara juzi na kuungana nao katika kusheherekea sikukuu ya Idd el Fitr.Picha na Mpigapicha wetu

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa amemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutoa maelezo juu ya fedha na mali zilizochangwa na Watanzania wakati wa maafa mbalimbali yaliyotokea hivi karibuni nchini, yakiwamo ya Kilosa, Gongo la Mboto, Dar es Salaam, vinginevyo ajiuzulu.

Aidha, amemtaka Waziri Mkuu kumwagiza Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovic Utouh kukagua hesabu hizo na kutoa taarifa hadharani na endapo atashindwa kuchukua hatua hizo ndani ya siku 30 Chadema kitachukua hatua nyingine.

Kauli hiyo ya Dk Slaa ilitolewa wakati wa tathmini ya chama hicho katika operesheni yake ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) iliyofanyika katika majimbo saba ya Mkoa wa Morogoro.

Akizungumza na waandishi wa habari jana wakati wa kutoa tathmini hiyo, Dk Slaa alisema endapo Waziri Mkuu atashindwa kuwajibu au akitoa maelezo yasiyoridhisha, ajiuzulu vinginevyo watamshtaki kwa umma wa Watanzania.
Alisema hali waliyonayo waathirika wa mafuriko ya Kilosa yaliyotokea miaka mitatu iliyopita ya kulala sakafuni na familia kuchangia chumba kimoja ni ya kusikitisha.

Alisema waathirika hao wamekuwa wakiendelea kuishi katika kambi hizo kwa shida huku utu wao ukidhalilishwa kutokana na kuishi baba, mama na watoto katika chumba kimoja na kutumia vyoo visivyokuwa na staha.

Alisema Watanzania wengi walijitokeza kutoa misaada mingi kwa watu walioathiriwa na maafa ya Gongo la Mboto, Mbagala na wale waliokumbwa na mafuriko na kuhamishiwa eneo la Mabwepande, Dar es Salaam.

Alisema katika majanga hayo, Ofisi ya Waziri Mkuu haikutoa hesabu za fedha zilizochangwa wala namna zilivyotumika.

Alisema haiingii akilini Serikali kuwapatia waathirika wa Kilosa kila mmoja mabati sita, mfuko mmoja wa saruji, misumari kilo moja na ubao mmoja kwa ajili ya kujengea nyumba huku wakiwa hawajakabidhiwa viwanja vya kujengea.

“Kutokana na hali hiyo, Chadema tunamtaka Waziri Mkuu kueleza fedha, mali na vitu vilivyochangwa na Watanzania vimekwenda wapi na kwa nini watu hawa wanapata shida huku Waziri Mkuu na viongozi wengine wakiangalia,” alisema Dk Slaa.

Katibu mkuu huyo alisisitiza kuwa Chadema kitawaagiza wabunge wake kupeleka hoja bungeni ya kuitaka Serikali kutoa taarifa za fedha na mali zilizochangwa ili kuwasaidia waathirika.

Mbio za Mwenge

Kuhusu Mbio za Mwenge ambazo zimekuwa zikiendeshwa kila mwaka nchini, Dk Slaa alisema malengo yake yamepoteza misingi halisi iliyowekwa na hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Alisema anachoona ni kwamba hivi sasa zinaeneza Virusi Vya Ukimwi (VVU) pamoja na kuwanyanyasa wananchi kwa kuwabebesha mizigo ya michango, badala ya malengo yaliyokusudiwa.

Alisema katika kipindi cha Mwalimu, mwenge ulikimbizwa nchini ukiwa na maana ya kueneza upendo pasipokuwa na upendo, amani pasipokuwa na amani, kueneza mwanga palipo na giza tofauti na ilivyo sasa.

“Hakuna sheria inayolazimisha mtu kutoa mchango wa mwenge. Mchango wa mwenge ni sawa na mchango wa harusi au send-off kwa hivyo Serikali iache kuwanyanyasa wananchi kwa michango hiyo isiyo ya kisheria,” alisema.

Alisema ikiwa chama chake kitafanikiwa kushika dola mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, mwenge huo utapelekwa makumbusho ili watu waweze kufika na kupewa historia yake.

Tathmini ya operesheni

Akizungumzia tathmini ya siku 12 ya operesheni hiyo mkoani Morogoro, Mkuu wa M4C, Benson Kigaila alisema Chadema kimepata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuingiza wanachama zaidi ya 31,537 kutoka katika vijiji 471 vya majimbo hayo saba.

Kigaila alisema tangu kuanza kwa operesheni hiyo mkoani Morogoro Agosti 8, mwaka huu chama hicho kimefungua zaidi ya matawi 100 akisema hiyo itasaidia kuwa takwimu sahihi za wapiga kura wake.

Alisema katika operesheni ya M4C, jumla ya kadi 7,605 za vyama vingine zimekabidhiwa kwa Chadema huku chama hicho kikifanikiwa kuuza kadi zake na kupata kiasi cha Sh15.8 milioni na wananchi wakikichangia kiasi cha Sh17.9 milioni.

Sensa ya Watu na Makazi

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Zanzibar, Said Issa Mohamed alisema Chadema kinaunga mkono Sensa ya Watu na Makazi na kuwataka wanachama wake kujitokeza kuhesabiwa.

Mohamed amewataka wanaChadema na wananchi kwa ujumla kuondoa itikadi zao za kidini, kisiasa na ukabila katika suala hilo akisema ni muhimu kwa ajili ya Serikali kuandaa mipango yake ya maendeleo.

Wakati huo huo: Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anatarajia kwenda Marekani wiki hii kwa ziara ya kukiimarisha.

Mbowe alisema mjini hapa juzi kuwa lengo la ziara hiyo ni kwenda kuhamasisha na kufungua matawi ya chama hicho kwa kushirikiana na Watanzania wanaoishi huko.
 

No comments:

Post a Comment