Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Tuesday, August 21, 2012

BOTI YA MV SALWAT YAZAMA WAKATI IKITOKEA PANGANI-TANGA KWENDA ZANZIBAR...!


WATU 10 wakiwemo raia wa kigeni wameokolewa na wengine wawili hawajulikani walipo baada ya Boti ya Mv Salwat waliyokuwa wanasafiria kutoka Tanga kwenda Pemba kuzama katika eneo la Pangani juzi jioni.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini, Abdallah Hussein Kombo amethibitisha kuzama kwa boti hiyo baada ya  kupigwa na wimbi kali na kusababisha kupinduka.


Kombo alisema kuwa watu 12 walikuwepo katika boti hiyo wakiwamo wanawake wawili, na miongoni mwa abiria hao 10 wamepatikana wakiwa hai,  wawili bado hawajapatikana lakini mamlaka zinazohusika zinaendelea kuwatafuta.

“Ndio tayari watu 10 wamepatikana lakini hao wawili bado wanatafutwa, wakipatikana tutatoa taarifa kamili lakini hivi sasa bado juhudi za kuwatafuta zinaendelea,” alisema Kombo.

Mkurugenzi huyo alisema juhudi za kuwatafuta na kuwaokoa watu hao zimefanyika ikiwa pamoja na kupeleka mapema boti za uokozi katika eneo la tukio.


Alisema manahodha walimudu kuwapatia abiria makoti ya kuokolea na hivyo kusaidia kuonekana kirahisi wakiogolea.


“Life Jacket zimesaidia maana waokoaji wameweza kuwaona na kuwafuata na kisha kuwaingiza katika maboti kwa sababu wameonekana wakiogolea,” alisema mkurugenzi huyo.


Baadhi ya waliokolewa ni Nahodha wa Boti hiyo, Ahmada Haji Gora ambaye hali yake ni mbaya lakini wengine wote wamepatikana wakiwa hali zao ni nzuri wakiwemo hao raia wa kigeni ambao hawajajulikana ni raia wa nchi gani.


Wakizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kufika katika eneo la Bandari ya Mkokotoni, Zanzibar mmoja wa waokoaji, Omar Salum alisema alipokea simu kutoka kwa kaka yake ambaye ni nahodha wa chombo hicho kwamba boti yao imezimika na tayari maji yamejaa ndani, hivyo kuomba msaada.


“Nahodha ni kaka yangu lakini niliwasiliana naye jioni (juzi) akisema chombo kimezimika na maji yameshajaa, huku hofu ikiwa imewajaa na wanahitaji msaada lakini bahati mbaya kila nikijaribu tena kumpigia sikuwa napata simu yake na hapo ndio nikaingiwa na wasiwasi tukaanza kutafuta chombo lakini ni mbali kule,” alisema muokoaji huyo.


Baadhi ya viongozi wa Serikali, maofisa wa Jeshi la Polisi na vikosi vya ulinzi na Kamati ya Maafa walifika eneo la Mkokotoni wakisubiri kuwapokea majeruhi hao huku umati mkubwa wa watu ukiwa umekusanyika kushuhudia boti zilizokuwa zikishusha majeruhi nao, tayari kupelekwa katika Hospitali ya Kivunge iliyopo Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Mwezi uliopita boti nyingine ya Mv Skagit ilizama katika Bahari ya Hindi na kusababisha vifo na majeraha kwa mamia ya watu. 
 

No comments:

Post a Comment