Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Monday, August 27, 2012

Hukumu ya Mchungaji Christopher Mtikila yapigwa tarehe...!

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu leo imesogeza mbele hukumu ya kesi ya kuchapisha na kusambaza waraka wa uchochezi dhidi ya Rais Jakaya Kikwete inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila.

Kusogezwa mbele kwa hukumu hiyo kunatokana na hakimu, Ilvin Mugeta anayesikiliza kesi hiyo kuwa katika majukumu mengine ya kikazi na hivyo hukumu hiyo itasomwa Septemba 6, 2012.

Katika kesi hiyo Mtikila anadaiwa kuwa kati ya Januari 2009 na Aprili 17, 2010 jijini Dar es Salaam, kwa nia ya uchochezi, alisambaza kwa umma nyaraka zilizosomeka 'Kikwete kuuangamiza Ukristo', 'Wakristo waungane kuweka mtu Ikulu'.

Mtikila alikiri kuandaa waraka huo na kusambaza nakala zaidi ya 100,000 nchini, huku akidai kuwa waraka huo si wa uchochezi bali unahusu maneno ya Mungu.

Akiwa mahakamani hapo leo asubuhi, Mtikila amesema anaamini atashinda kesi hiyo kwani hayo yalikuwa ni maoni yake na kila raia ana haki ya kutoa maoni isipokuwa havunji katiba.

Kabla ya siku ya leo, Mchungaji Mtikila alifunga ushahidi baada ya kutetewa na mashahidi wawili badala ya kumi alioahidi kuwafikisha mahakamani hapo, “Mheshimiwa, nafunga ushahidi, ilikuwa nilete mashahidi 10, lakini wawili wanatosha kwa sababu wengine walikuwa maaskofu kutoka Mwanza ambao naamini wangekuja kueleza kile kile nilichoeleza. Nahofia kupoteza fedha za Serikali kwa kuwaleta mashahidi hao, kwani nao hawana kitu tofauti na mashahidi wengine,” alidai Mtikila.

Hakimu Mugeta alisema uamuzi wa Mtikila ni mzuri, asipoteze fedha za umma kama anaamini hivyo angesoma hukumu leo.

Mtikila ambaye ni shahidi wa kwanza wa upande wa utetezi, alidai kuwa, kesi hiyo ilifunguliwa kutokana na chuki zilizokuwapo kati yake na mchungaji mwenzake, lakini kwa upande wa Rais Kikwete hakumshitaki pamoja na kwamba alimpa nakala ya waraka huo unaodaiwa wa uchochezi.

Shahidi wa pili wa upande wa utetezi, Mpoki Bukuku kutoka Gazeti la Mwananchi, alidai mahakamani hapo kwamba, walichapisha habari yenye kichwa cha habari ‘Mtikila apiga kampeni Kanisani kumpinga Kikwete’. Pia alidai kwamba, gazeti hilo liliandika Mtikila achunguzwa na Polisi kwa kumwaga sumu, Rais Kikwete asichaguliwe mwaka 2010 na kuongeza kuwa habari hiyo iliripoti kilichotokea Mwanza na ilikuwa ya kweli kwa sababu kati ya polisi na Mtikila, hakuna aliyekanusha. Alidai habari hiyo, ilikuwa ikielezea mafundisho waliyokuwa wakitoa viongozi wa dini katika kongamano.

Mtikila, anadaiwa Aprili, 2010 mjini Dar es Salaam, alisambaza waraka anaodai wa kuunusuru Ukristo wenye lengo la kuangamizwa na Jihad ya Rais Jakaya Kikwete na kwamba Wakristo wajitoe muhanga kukomesha ugaidi.

Alidai waraka uliosambazwa, alisaini akiwa kama Mwenyekiti wa Kamati ya kuunusuru Ukristo na walichapa nakala 100,000, lakini aligoma kutaja mahali walipochapishia nakala hizo.

Maelezo yote hayo yalitolewa mahakamani kama kielelezo na SSP, Ibeleze Mrema aliyemuhoji Mtikila Aprili 14, 2010 na alipotakiwa kueleza chochote kuhusu kielelezo hicho, mshitakiwa alisema hana swali na akakubali kipokelewe na mahakama.

No comments:

Post a Comment