Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Saturday, August 18, 2012

LOWASSA APINGA SERA YA JK YA "KILIMO KWANZA"...!

WAKATI Serikali ya Rais Jakaya Kikwete ikitoa kipaumbele kwa kilimo na kutangaza mpango wa kilimo kwanza, Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa amepingana na dhana hiyo kwa kusema elimu ndiyo inayopaswa kuwa kwanza na baadaye kilimo.

Lowassa alitoa wito huo wakati alipokuwa akikabidhi michango ya harambee ya wafugaji wa jamii ya Wamasai katika Kijiji cha Kiegea kusaidia ujenzi wa Shule ya Msingi Ujirani ambapo alialikwa kuwa mgeni rasmi kama kiongozi wa jamii hiyo nchini.

Lowassa ambaye anatamba kwa kuasisi mpango wa shule za kata, alisema elimu ni muhimu zaidi kabla ya kilimo, hivyo alitoa changamoto kwa wananchi wa kata mpya ya Mkundi ya jamii hiyo ya wafugaji kuanza ujenzi wa shule ya sekondari ya kata.

“'Ni aibu kata hii kutokuwa na shule ya sekondari wakati kila kata nchini ina shule ya sekondari ambako hivi sasa angalau kuna usawa kwa watoto kugusa elimu ya sekondari,” alisema na kuongeza kuwa atakuwa tayari kurudi kwenye kata hiyo Januari mwakani kuongoza harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa sekondari.

“Niko tayari kuja Januari kuongoza harambee ya kuchangisha fedha, ni aibu, kwakweli sijafurahishwa na hali yenu hapa, mnatakiwa nyinyi wenyewe msimame kidete kujiletea maendeleo, njooni Monduli mjifunze jinsi wafugaji wenzenu walivyoweza kutumia mifugo yao kujenga shule na nyumba za walimu,” alisema Lowassa.

Katika hilo, alimtaka kila mfugaji kutoa ng’ombe au mbuzi mmoja kwa ajili yakuchangia elimu kwenye kata yao na kumuomba mkuu wa wilaya kutumia sheria zilizopo kumkamata na kumtia ndani yeyote atakayekaidi wito huo.

Katika harambee hiyo, Lowassa alichangia mabati 500 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa madarasa ya shule hiyo ya msingi ya Ujirani yenye wanafunzi 414, na walimu wawili tu; mmoja wa kuajiriwa na mwengine wa kujitolea.

Wananchi wa eneo hilo walichanga ng’ombe watano kwa ajili ya kuendeleza shule hiyo, idadi ambayo Lowassa aliipinga akisema kuwa wananchi hao wana idadi kubwa ya mifugo hivyo wanatakiwa watoe zaidi.

Hii ni mara ya pili kwa Lowassa kupingana na serikali katika suala la vipaumbele vya taifa.

Hivi karibuni Waziri Mkuu huyo mstaafu alishupalia suala la ajira kwa vijana kwamba ni bomu linalosubiri kulipuka, kauli ambayo ilijibiwa kwa nguvu na serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

No comments:

Post a Comment