Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Wednesday, August 22, 2012

Tanzania na Malawi wajadili mgogoro wa mpaka ndani ya ziwa Nyasa...!



WATAALAMU wa mipaka kutoka Tanzania na Malawi wanakutana kujaribu kupata suluhu ya mgogoro wa mpaka kati ya nchi hizo ambao umedumu kwa miongo kadhaa.  Hivi karibuni mgogoro umeibuka upya baada ya Malawi kutoa kibali kwa kampuni ya Uingereza kufanya utafiti wa mafuta na gesi katika fukwe zote za Ziwa Malawi.

Mkutano huo unafanyika Malawi katika Mji wa Mzuzu, ukiwa ni mwendelezo wa mkutano kati ya mawaziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa nchi hizo, uliofanyika Dar es Salaam mwezi uliopita.  Azimio lililopitishwa katika mkutano huo wa awali, ni kuwataka wataalamu wa mipaka kukutana na kutoa mapendekezo yao. Wakati wa ufunguzi wa mkutano huu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Ephram Chiume alisema kuwa wananchi wa Malawi na Tanzania wana imani kubwa kuwa suala hili litapatiwa ufumbuzi wa kudumu bila kuwapo kwa mapambano.

Aliwataka washiriki waepuke lugha zitakazoleta kutokuelewana.  Alisema baada ya wataalamu kukamilisha mjadala wao watatoa ripoti yenye mapendekezo mazuri.  Ripoti hii itawasilishwa kwa mawaziri husika Jumamosi. Mawaziri  wataipitia, kuongeza machache kabla ya kuiwasilishwa  kwa viongozi wa nchi ambao ni Rais Joyce Banda wa Malawi na Jakaya Kikwete wa Tanzania. Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania, Selassie Mayunga amesema kuwa ana matumaini kuwa majadiliano yatakuwa ya amani na yatakayozaa matunda.

“Ninachoweza kusema ni kuwa maelezo ya Waziri wa Nchi za Nje wa Malawi, Mheshimiwa Chiume yalikuwa mazuri sana na yanatupa mwongozo wa jinsi ya kuendeleza majadala huu kwa mujibu wa mipaka ya kimataifa  kati ya Malawi na Tanzania katika Ziwa Nyasa.

Tuna imani kuwa majadiliano haya yatakuwa ni ya kindugu.”  Mzozo kati ya nchi hizi mbili uliongezeka mwaka jana wakati Rais wa Malawi, Bingu wa Mutharika alipotoa kibali kwa kampuni ya Surestream Petrolium kufanya utafiti wa gesi na mafuta katika Ziwa Malawi (Ziwa Nyasa). Hatua hii iliikasirisha Tanzania ambayo inadai kuwa ina haki ya kumiliki asilimia 50 ya Ziwa hilo, huku Malawi ikisema inamiliki ziwa lote.

Tayari Serikali ya Tanzania imeitaka Malawi kusitisha zoezi hilo hadi majadiliano yatakapofanyika. Malawi inajipa uhalali wa kumiliki ziwa lote kutokana na azimio kati ya wakoloni wa Uingereza na Ujerumani, lililotiwa saini mwaka 1890. Azimio hili baadaye lilithibitishwa na Umoja wa Nchi huru za Afrika ambapo Malawi walipata idhini ya kumiliki ziwa lote.

 Tanzania inapinga makubaliano haya ya kikoloni kuwa siyo ya kudumu kwani sheria nyingi za kimataifa zinaunga mkono suala la mipaka wa majini kati ya nchi mbili kuwa ni nusu kwa nusu kwa eneo la maji.


Stephen Maina, Mashirika

No comments:

Post a Comment