Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Friday, August 31, 2012

WAZIRI MKUU AMEWATAKA WAJUMBE WA KAMATI YA USHAURI YA MKOA WA KATAVI WAANDAE MPANGO WA MAENDELEO...!

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Katavi (RCC) waandae Mpango wa Maendeleo wa Mkoa ambao utawasadia kuwaongoza kuendesha mkoa huo mpya.
Waziri Mkuu ametoa changamoto hiyo leo (Ijumaa, Agosti 31, 2012) wakati akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo kwenye mkutano wa siku moja uliofanyika kwenye ukumbi wa Idara ya Maji mjini Mpanda. Waziri Mkuu aliizindua rasmi kamati hiyo leo.
Alisema RCC ni lazima ikae chini na kutazama wamejipanga vipi kuendesha mkoa huo mpya. “Lazima muandae Mpango wa Maendeleo wa Mkoa ambao utawiana na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano... Hili jambo haliepukiki, litasaidia kutengewa Bajeti kwa sababu tutakuwa tuko kwenye matakwa ya Mpango wa Taifa,” alisema.
Akigusia kuhusu ushirikishwaji wa maamuzi kuanzia ngazi ya chini, Waziri Mkuu alisema kwa vile ratiba ya RCC ni kukutana mara mbili kwa mwaka, wanaweza kuandaa mpangokazi na kisha wakaipeleka kwenye ngazi za wilaya ili ijadiliwe kuanzia huko.
“Ikibidi baadhi ya masuala mnaweza kuyapeleka kwenye ngazi ya mabaraza ya madiwani ili yaanze kujadiliwa huko, halafu yaletwe kwenye Kamati ya Ushauri ya Wilaya na hatimaye vikifishwe kwenye ngazi ya Mkoa,” alisema.
Akizungumzia kuhusu maendeleo ya mkoa huo mpya, Waziri Mkuu alisema wajumbe wa kamati hiyo wanapaswa kujiuliza hali ya maendeleo ilivyokuwa wakati wakiwa ni wilaya tu chini ya mkoa wa Rukwa na kisha wajipime wanataka kwenda wapi kwa sasa wakiwa ni mkoa mpya.
“Nawaomba sana mjiulize pato la mwananchi kwa mwaka (GDP) lilikuwaje wakati tukiwa chini ya Rukwa na kwa sasa tumeshakuwa mkoa mpya, je pato hilo kwa mwaka litakuwaje, nini kitasaidia kuongeza pato la huyu mwananchi... ni lazima tujipange vizuri ili tuonyeshe tofauti,” alisisitiza.
Akizungumzia kuhusu hali ya umaskini inayoukabili mkoa huo, Waziri Mkuu Pinda alisema anakerwa na hali ya umaskini wa kipato inayowakabili wakazi wa mkoa huo na kamwe hataki kusikia hali hiyo ikiendelea kuimbwa kila siku kwa sababu hakuna sababu ya kubakia kuwa maskini.

“Mkoa wa Katavi bado ni maskini... sitaki tuwe maskini kwa sababu hatuna sababu ya kuwa maskini. Na kama tutaendelea kuwa maskini, basi tutaponzwa na uwezo mdogo wa kufikiri wa wataalamu wetu,” alionya na kuongeza kuwa yeye anaamini kwamba: “Katavi bila umaskini inawezekana.”
Aliwataka wajumbe wa kamati hiyo kushirikiana bila kujali itikadi wala imani zao bali aliwataka waweke mbele suala la maendeleo ili kuweza kutoka hapo walipo kimkoa kwa kwani fursa walizonazo ni nyingi na wakazi wa mkoa huo ni wachapakazi sana.
Alimtaka Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Rajab Rutengwe kubuni utaratibu wa kuwagawa wajumbe wa kamati kwenye kamati ndogondogo za kisekta na kuwapangia majukumu ili iwe rahisi kufuatilia utekelezaji wa maamuzi wanayoyafikia kisekta.
“RC usingoje kuandikiwa kila kitu... kazi ya kusukuma maendeleo inataka ubunifu. Wagawe wajumbe kwenye kwenye kamati ndogo za kisekta lakini cha msingi uwape mjumbe mmoja kutoka kwenye sekretarieti ili awasaidie kuwaongoza,” alisema.

No comments:

Post a Comment